Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kila mtu ambaye hajafanikiwa, na hapa mafanikio yakiwa ni kupata kile ambacho mtu anataka, ana sababu nzuri tu kwake kwa nini hajafanikiwa.
Hakuna ambaye hajafanikiwa na akawa hana sababu ambazo zinamridhisha yeye. Kila mtu atakueleza vikwazo mbalimbali ambavyo amekutana navyo na vikamzuia kufanikiwa.
Lakini sasa, siyo wao wenyewe wanaokuwa wamekutana na vikwazo hivyo. Wapo waliofanikiwa licha ya kukutana na vikwazo kama hivyo pia, na wakati mwingine vikwazo vyao vikiwa vikubwa zaidi.
Watu wamekuwa wanatumia kukosa fedha kama kikwazo kikubwa kwao kufanikiwa. Iwe ni kukosa mtaji wa biashara au kukosa kazi au kazi kulipa kidogo, pesa imekuwa kikwazo kwa wengi. Lakini wapo ambao walianzia chini kabisa, wakiwa hawana pesa, hawana kazi na wala hawana biashara, lakini wameweza kufanikiwa.
Inaweza kuonekana kama kuna bahati ambayo baadhi ya watu wanaipata na kufanikiwa licha ya vikwazo wanavyokuwa wamekutana navyo. Lakini kama ni bahati, huwa imesambazwa sawa kwa watu wote. Wanaonufaika na bahati ni wale ambao wanajua jinsi ya kuitega.
Kila mtu anaweza kufanikiwa licha ya vikwazo anavyokutana navyo. Kwa sababu vikwazo siyo mwisho wa safari ya mafanikio, bali ni sehemu ya safari hiyo. Wanaoshindwa wamekuwa wanaona vikwazo kama mwisho, na hivyo kuachana na safari wanapokutana navyo.
Wanaofanikiwa huwa wanaona vikwazo kama njia ya kufanikiwa, hivyo wamekuwa wanavitumia kupata kile wanachotaka.
Najua unaweza usielewe, iweje kinachokuzuia kiwe pia ndiyo njia? Na hilo ndiyo tunakwenda kujadiliana taratibu sana hapa kwenye #BaruaYaKocha. Baada ya barua hii, sitegemei tena wewe ushindwe na kitu chochote, kwa sababu utaweza kukaa kwenye safari yako ya mafanikio bila kusimamishwa na chochote.

1. Pata Mafanikio Unayoyataka Kesho.
Rafiki, leo nataka nikubaliane na wewe kwenye kitu kimoja, kwamba kuna njia ya mkato ya kufanikiwa. Nataka nikubaliane na wewe kwamba unaweza kulala masikini na kuamka tajiri, si ndivyo wengi wanavyopenda?
Sawa, basi twende na hilo. Inabidi kesho uwe umepata mafanikio makubwa unayoyataka. Ndiyo, kesho tu. Yaani ukiamka kesho, uwe umepata kila unachokitaka.
Swali ni je inawezekana? Jibu, hakuna mtego wowote hapo. Kama inawezekana, hongera, tayari umefanikiwa. Kama unayo njia ya halali ya kukuwezesha kupata kila unachotaka kesho, uko vizuri. Na mimi nitaomba unishirikishe njia hiyo.
Kama jibu ni haiwezekani kupata kila unachotaka kesho, ni jibu zuri pia. Na hapo ndiyo tunaweza kuanza kutofautiana, maana wewe unaweza kudhani ni jibu baya, kwa sababu hupati unachotaka.
Na mimi nakuambia ni jibu zuri, kwa sababu, sasa tuna mahali pa kuanzia. Kama haiwezekani kupata kila unachotaka kesho, nini kinachozuia hilo kutokea? Lazima kuna kikwazo, si ndiyo?
Tuseme unataka kujenga biashara yenye thamani kubwa na inayojiendesha bila kukutegemea. Kama bado hujaanza biashara, ni wazi hilo haliwezi kutokea kesho. Sasa swali ni nini kinachokuzuia kuwa na hiyo biashara kesho? Hapo ndipo safari yetu ya mafanikio inapoanzia.
2. Kabiliana Na Kile Kinachokuzuia Kuyapata Kesho.
Kama unaweza kupata mafanikio yako yote kesho, huna haja ya kuendelea kusoma hapa. Unapaswa kuwa unajiandaa kuyapokea na kuyafurahia. Kama huwezi kuyapata kesho, umeshajua ni nini kinachokuzuia kuyapata hiyo kesho.
Hicho sasa ndiyo unachopaswa kuanza kukifanyia kazi. Wajibu wako ni kukabiliana na kile ambacho kinakuzuia kupata mafanikio makubwa unayoyataka kesho. Sahau kwa muda kuhusu hayo mafanikio makubwa na pambana na kile kinachokuzuia kuyafikia kesho.
Kikwazo chochote kinachokuzuia kuyafikia mafanikio unayoyataka, siyo mwisho wa hiyo safari. Bali ni hatua ya kuvuka ili ufike kwenye kile unachokitaka. Na pia kikwazo hicho huwa kinawazuia wengi ambao hawajajitoa kweli kufanikiwa. Hivyo wewe ukiwa umejitoa hasa kufanikiwa na ukavuka kikwazo hicho, utakuwa kwenye upande mzuri.
Tukiendelea na mfano wetu wa kujenga biashara yenye thamani kubwa na isiyokutegemea, kama bado hata hujaanza biashara, kikwazo kikubwa kwako ni kuanza biashara. Hivyo una lengo la biashara kubwa, ila bado hata hujaianza, hivyo pambana kwanza na kuanza biashara.
Mengine makubwa na mazuri unayotaka yatokee kwa kuwa na biashara hayatawezekana kama kwanza huna biashara. Hivyo unapaswa kupeleka rasilimali zako zote kwenye kuanza biashara.
Kukabiliana na kinachokukwamisha ndiyo hatua pekee inayokuwa mbele ya kila mtu. Lakini wengi wanahangaika na mambo mengi yasiyokuwa na tija, badala ya kukabiliana na kile kinachowakwamisha. Ukijenga utamaduni wa kujua kikwazo na kushughulika nacho, hakuna kitakachokukwamisha kufanikiwa.
Soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK154; Jinsi Ya Kutumia Vikwazo Vinavyokuzuia Kufanikiwa Kuwa Njia Yako Ya Mafanikio