Ukiangalia matatizo uliyonayo, na malengo yako kwenye maisha jibu rahisi unalopata ni ukipata kiasi fulani cha fedha baasi, matatizo bai bai. Au unafikiri ukiweza kulipwa ama kutengeneza kiasi fulani kwa mwezi matatizo kwako ndio mwiko!!

pesa

  Kabla hujajiridhisha na jibu kwamba matatizo yote yanatokana na kukosa fedha fikiria hivi kwanza. Umewahi kugundua kwamba watu wengi huwa wanaishiwa fedha sawa licha ya kuwa na vipato tofauti? Kwa mfano wafanyakazi wengi kila inapokaribia mwisho wa mwezi(kuanzia tarehe ishirini na) wanakuwa ‘wamefulia’, yaani anaepata laki moja, milioni moja na hata milioni tano kwa mwezi bado wote wanaimba wimbo ule ule unapfika mwisho wa mwezi!!

broke

  Kama sasa hivi unapata laki tano kwa mwezi, unaweza kufikiria ukipata milioni mbili kwa mwezi ndio maisha yatakuwa sawa, ila kuna anaepata hiyo milioni mbili na bado mambo yanazidi kuwa magumu kwake.

  Kwa maana hii basi fedha sio tatizo, yaani kama sasa hivi unapata fedha kidogo ila matatizo hayaishi basi hata ukipewa fedha nyingi kiasi gani ndio utakuwa umezidishiwa hayo matatizo. Fedha sio tatizo, tatizo kubwa ni wewe, na tatizo kubwa ni tabia zako linapokuja swala la fedha.

  Kuna baadhi ya tabia ambazo watu wengi wanazo na tabia hizo zinaleta matatizo mengi ya kifedha. Baadhi ya tabia hizo ni;

1. Manunuzi yasiyo ya msingi na yasiyo ya ratiba. Kuna watu wakishakuwa na fedha tu mfukoni chochote kitakachopitishwa mbele yake na kushawishiwa kununua anajikuta ameshanunua. Hii tabia wanayo sana kinadada/mama. Umewahi kufatwa na mtu anaefanya biashara akakushawishi kununua kitu anachouza na ukajiridhisha kununua ila unafika nyumbani na kugundua umefanya makosa kununua hicho kitu? Hiyo ni tabia ambayo inabidi uiangalie ili kuepuka matumizi mabovu ya fedha. Nunua vitu kutokana na mahitaji na sio kwa sababu umeona.

kununua

2. Kununua vitu ili kunekana wa daraja fulani. Kuna watu wengi sana wanaonunua vitu ambavyo havina uhitaji mkubwa kwenye maisha yao ila kutaka tu nao wavimiliki, kwa mfano simu za bei ghali, magazi ya bei ghali na nguo za bei ghali. Kama kuna uwezekano wa kupata kitu bora kwa bei ambayo sio kubwa sana na kikaweza kutimiza mahitaji yako basi nunua hicho. Kama wewe ni mtafutaji ni muhimu sana kuelewa hili ili kutojikuta kwenye wakati mgumu.

3. Hesabu mbaya za fedha. Kuna watu ukiwauliza gharama zao za maisha kwa mwezi mzima ni shilingi ngapi hata hawajui, labda na wewe ni mmoja wao! Kwani wewe kwa mwezi unatengeneza shilingi ngapi na matumizi yako ni shilingi ngapi? Watu wengi hawana bajeti ya matumizi yao yote kwa mwezi hivyo hujikuta wanatumia tu fedha mpaka zinapokwisha na mambo yanaanza kuwa magumu.

4. Tabia zilizokomaa(uteja), kuna watu ni wateja wa tabia fulani ambazo zinagharimu fedha nyingi sana, baadhi ya tabia hizo ni uchezaji kamari, unywaji wa pombe, utumiaji wa madawa na starehe mbalimbali. Kamari na michezo mingine inayofanana na hiyo(kama promosheni za mitandao ya simu) ni tabia ambazo zinawagharimu watu fedha nyingi sana. Unywaji wa pombe na starehe hizi ndio tatizo sana, kuna watu wameshajijengea tabia kwamba hawawezi kulala mpaka wanywe bia kadhaa. Hushangai baa kila siku zinaongezeka mitaani!!

addictive

5. Kuingia kwenye madeni bila ya kujua vizuri gharama za madeni hayo. Uelewa mdogo kuhusu mambo ya fedha hasa viwango vya riba umewafanya wengi kuchukua mikopo bila kujua gharama halisi za mkopo huo. Mwishowe mtu anakuja kuumia kwenye kulipa.

  Hizo ni baadhi tu ya tabia zinazokusababishia matatizo, na sio fedha. Badili kwanza tabia yako ndipo utamani kungeza kipato chako. Ukijaribu kuongeza kipato kabla ya kubadili tabia matatizo yatakuwa makubwa zaidi  ya uliyonayo kwa sasa.