Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Hisabati ni moja ya masomo yasiyopendwa na wengi wakati wapo shuleni. Wengi huwa hawafaulu somo hili, na hapa hatutaangalia sababu za hilo.
Na katika kuonyesha kwamba hisabati ngumu hazina manufaa sana kwenye maisha, watu huwa wanauliza kama utani ni lini mtu ametumia kanuni za hisabati kwenye maisha ya kawaida. Kanuni kama za kigawe kidogo cha shirika na kigawe kikubwa cha shirika zilionekana kama za kutusumbua tu.
Wengi huona wakishajua GAZIJUTO, yaani kujumlisha, kutoa, kuzidisha na kugawanya inawatosha kufanya hesabu muhimu za maisha ya kila siku. Na hilo lina ukweli kwenye maisha duni na ya chini.
Kwa maisha ya mafanikio makubwa ambayo mtu unakuwa unayataka, kuna hisabati ambazo lazima uzijue na uzikokotoe ili uchukue hatua sahihi zitakazokupa matokeo unayotaka.
Rafiki, unazikumbuka hesabu za KIPEO na KIPEUO? Au hayo majina tu yanakuchanganya! Aisee, kumbe ni hesabu fulani hivi muhimu sana kwenye safari ya mafanikio. Na hesabu hizo zinaeleza kwa nini watu wengi sana ‘hawatoboi’ kwenye maisha licha ya kuweka juhudi kubwa.
Kwenye hii #BaruaYaKocha nimekueleza kwa lugha rahisi sana kuelewa hesabu hizo na jinsi ya kuzitumia ili upate mafanikio makubwa unayotaka. Hata kama hukupenda kabisa hisabati, leo utaelewa vizuri na kuweza kuchukua hatua sahihi.

1. Kanuni Ya Price; Kipeuo Cha Juhudi Zinazowekwa Ndiyo Kinazalisha Nusu Ya Matokeo Yanayopatikana.
Kabla sijakueleza hii kanuni, nikukumbushe kipeo na kipeuo ni nini.
Kipeo (Power/Exponent) ni kuzidisha namba kwa yenyewe idadi fulani ya mara. Mfano: 2³ (soma: mbili yenye kipeo cha tatu) maana yake ni 2 × 2 × 2 = 8. Hapa, 8 ni jibu la kipeo.
Kipeuo (Square Root/Root) ni kitendo cha kutafuta namba ambayo ikizidishwa kwa yenyewe (mara ngapi kulingana na kipeuo husika) inatoa namba ya awali. Mfano: Kipeuo cha pili cha 9 (√9) ni 3, kwa sababu 3 × 3 = 9.
Mwisho wa kukumbushana hisabati, sasa turudi kwenye kanuni ya Price.
Mwaka 1963, mwanafizikia aliyeitwa Derek J. de Solla Price alikuwa anatafiti kuhusu machapisho ya kisayansi, akitaka kuelewa kwa nini baadhi ya watafiti walikuwa wanafanya vizuri kuliko wengine.
Alichogundua ni kwamba nusu ya machapisho ilikuwa imefanywa na kipeuo cha watafiti waliokuwa kwenye tasnia husika. Kwa mfano kama tasnia ina machapisho 500 na watafiti 100, nusu ya hayo machapisho yaani 250 (500/2) yalitoka kwa kipeuo cha watafiti, yaani 10 (√100).
Kinachoonekana hapo ni matokeo makubwa sana yanatokana na juhudi chache zinazokuwa zimewekwa.
Na hiyo ndiyo kanuni ya Price, inayosema; ‘Nusu ya matokeo inatokana na kipeuo cha juhudi zinazowekwa.’
Mifano zaidi ya kuelewa kanuni hii;
- Kama kampuni ina wafanyakazi 100, ni wafanyakazi 10 tu wanaozalisha nusu ya matokeo yanayopatikana.
- Kwenye mauzo yaliyofanyika kwa wateja 25, wateja 5 wanakuwa wamechangia nusu ya mauzo yote.
- Kwenye timu ya watu 9 wanaofanya kazi, ni watatu pekee wanaofanya kazi kubwa.
Kanuni hiyo inafanya kazi kwenye kila eneo, ambapo kuna juhudi na matokeo. Ni juhudi chache sana zinazochangia matokeo makubwa.
Na kanuni kwa ufupi ni: √n = mchango kwenye matokeo makubwa, ambapo n ni jumla ya juhudi zote zinazowekwa.
Unaweza kupima kanuni hiyo kwenye maisha yako binafsi na maeneo mengine na namba zitakuwa zinakaribia hizo mara zote.
2. Uwezo Ni Kitu Adimu Kuliko Inavyodhaniwa.
Kwa kanuni hiyo ya Price, unaweza kuona jinsi ambavyo matokeo makubwa yanazalishwa na watu wachache sana. Na kadiri watu wengi wanavyohusika kwenye kitu, ndivyo ambavyo wachache sana ndiyo wanakuwa na mchango mkubwa.
Kwa kuona hivyo, tunaweza kudhani kundi kubwa la watu ni wavivu na wazembe. Lakini ukweli ni kwamba kinachotofautisha matokeo ni uwezo kuliko hata juhudi. Wale wanaochangia matokeo makubwa wanakuwa na uwezo tofauti na wanaochangia kidogo.
Kuna vitu vinne vinavyohitajika kwenye kupata matokeo;
Cha kwanza ni ujuzi, lazima mtu awe anajua jinsi ya kufanya kile anachofanya.
Cha pili ni msimamo, lazima mtu afanye kwa msimamo bila kuacha ndiyo apate matokeo.
Cha tatu ni fursa, lazima mtu atafute na kutumia vizuri fursa zinazopatikana ili kupata matokeo.
Cha nne ni bahati, ndiyo, lazima mtu akutane na bahati kwenye ufanyaji wake ndiyo apate matokeo makubwa.
Ni pale vitu hivi vinne vinapoungana kwenye mwelekeo mmoja ndiyo matokeo makubwa yanapopatikana. Yaani mtu kuwa na ujuzi, akafanya kwa msimamo, akazitumia fursa na kukutana na bahati.
Watu wengi huwa wanakuwa na kimoja au viwili kati ya hivyo vinne, na ndiyo maana wanaishia kupata matokeo ya kawaida.
Wachache sana wanaokuwa na vyote vinne ndiyo wanaozalisha matokeo makubwa sana.
Na hiyo ndiyo maana kadiri watu wanavyokuwa wengi, ndivyo wachache sana wanachangia matokeo. Kwa sababu siyo wengi ambao wanaweza kuwa na vyote vinne kwa pamoja.
Uzuri ni kwamba, vyote vinne vipo ndani ya uwezo wako, wajibu wako ni kuchagua kufanyia kazi kitu sahihi, kisha kujenga vitu hivyo. Na kama unajiuliza unawezaje kujenga bahati, nikukumbushe bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa. Hivyo ukiwa na maandalizi sahihi, ukawa unazifanyia kazi fursa na ukafanya kwa msimamo bila kuacha, utakutana na bahati.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK109; Sababu Za Kihisabati Kwa Nini Watu Wengi ‘Hawatoboi’ Kwenye Maisha