Kila kitu kinachofanyika kwenye maisha yetu kinaanzia na malengo na kisha mipango madhunuti ya kufikia malengo yetu. Malengo ni muhimu sana kwenye maisha ya kila mtu. Kama bado hujajua umuhimu wa malengo soma; malengo, unatoka wapi, uko wapi na unakwenda wapi.

  Kwa kuwa malengo ni muhimu sana kwenye maisha yako, zoezi la kuweka malengo pia ni muhimu sana. Hivyo unapokwenda kuweka malengo fanya kwa umakini na kwa kufikiria kwa kuwa ni kitu muhimu sana. Nunua kijitabu maalumu utakachoandika malengo yako, maana usipoandika ni vigumu sana kuyafikia(soma; ni muhimu sana kuandika)

  Unapoweka malengo ni lazima uhusishe kila sehemu ya maisha yako. Usiweke malengo ya fedha tu, au kazi tu. Kila sehemu inayohusu maisha yako ni lazima uiwekee malengo(soma; maisha ni zaidi ya kuwa na fedha nyingi.)

  Kwa kuwa mwaka 2014 ndio unakuwa mwaka wa mabadiliko makubwa kwenye maisha yako, utaweka malengo yote ya maisha yako sasa, ya muda mfupi na ya muda mrefu. Weka malengo ya miezi, mwaka mmoja, mpaka miaka ishirini ijayo.

malengo2

  Kuna sehemu kuu tatu kwenye maisha yako ambazo ni lazima uwekee malengo.

A. Malengo yako binafsi.

  Haya ni malengo yanayokuhusisha wewe na maendeleo yako binafsi kama binadamu. Weka malengo ya maendeleo yako binafsi kutokana na maswali yafuatayo;

1. Wewe ni nani, unataka kuwa nani na unajiona wapi miaka ishirini au zaidi ijayo?

2. Unataka kupata elimu kiasi gani na ni vitu gani vipya unataka kujifunza?

3. Unataka kufanya kazi gani ama unataka kufikia kiwango gani kwenye kazi unayofanya sasa?

4. Mahusiano na familia, unataka kuwa na familia ya aina gani na mahusiano yako na familia yako au wale uwapendao unataka yawe ya aina gani?

5. Unataka kutoa mchango gani na mabadiliko gani kwenye jamii inayokuzunguka?

6. Unataka kuleta mabadiliko gani kwenye kazi unazofanya?

7. Afya, unataka kuwa na afya ya aina gani, mwili wa aina gani?

8. Imani, una malengo gani kuhusu maisha yako ya kiimani(kiroho)? Ni vipi unaweza kuyaboresha?

9. Unataka kuzungukwa na watu wa aina gani? Kuwa na marafiki wa aina gani?

10. Matumizi ya muda na nidhamu binafsi. Unapanga kuutumiaje muda wako? Ni nidhamu gani umekosa kwenye maisha yako na unahitaji kuizingatia?

11. Ni vitu gani inabidi ubadili kwenye maisha yako ili uweze kufikia malengo yako? Ni vipi vipya inabidi uanze kufanya na ni vipi vya zamani inabidi uache kufanya?

B. Malengo ya vitu.

  Haya ni malengo unayoweka kwa vitu unavyotaka kumiliki kwenye maisha yako. Jiulize ni vitu gani unataka kumiliki kwenye maisha yako na kwa kiwango gani? Unataka kumiliki nyumba ngapi? Magari mangapi? Viwanja au mashamba mangapi? Ni vitu gani vingine unavyohitaji kumiliki kwenye maisha yako?

C. Malengo ya kifedha na kiuchumi.

  Haya ni malengo yanayohusisha fedha na uchumi wako. Andika malengo yako kwa kufuata maswali haya;

1. Unahitaji kutengeneza kiasi gani cha fedha kwa siku, mwezi na hata mwaka kutoka kwenye shughuli zako unazofanya? Kama unahitaji kukokotoa soma; hii ndio thamani ya muda wako.

2. Ni vitega uchumi gani unavyotegemea kuwa navyo kwenye maisha yako? Unahitaji kuwekeza kwenye nini?

3. Unategemea kufanya kazi kwa kipindi gani na unategemea kustaafu lini ukiwa umeshajiwekea vitega uchumi vya kutosha?

4. Unategemea kuikomboa vipi jamii inayokuzunguka kifedha na kiuchumi?

5. Ni mabadiliko gani unayohitaji kufanya kwenye mapato na matumizi yako ili uweze kufikia malengo yako?

  Hayo hapo juu ni maswali yatakayokusaidia kujiwekea malengo ya maisha yako ya muda mfupi na hata muda mrefu. Unaweza kuongeza maswali mengi zaidi ya hapo kulingana na maisha yako maana wewe ndiye unayajua maisha yako vizuri zaidi.

  Hata kama kwa sasa hujui ni jinsi gani utafikia malengo uliyoandika usiwe na wasiwasi, andika kwanza na kuwa makini unapoandika. Baada ya kuandika malengo hayo weka muda unaohitaji kuyatimiza mbele ya kila lengo. Kama ni mwaka au miaka miwili au kumi weka mbele ya lengo.

  Kama umeweza kuandika malengo yako vizuri kwenye kitabu chako umeweza kupiga hatua kubwa sana ya kuyafikia malengo yako. Kilichobaki ni mipango ya kutimiza malengo hayo ambayo utaendelea kuipanga na kujifunza muda unavyokwenda.

  Endelea kutembelea mtandao wako wa AMKA MTANZANIA ili kuendelea kujifunza na kujihamasisha na kuweza kupata mbinu mbalimbali za kufikia malengo yako.