Tunakubaliana kwa pamoja kwamba hakuna kitu kinachoweza kufanyika bila mipango. Kila kitu unachofanya kwenye maisha yako unapanga kukifanya labda kwa kujua au kutokujua. Hata kuamka kitandani leo ilikuwa mpango, kuenda kwenye shughuli zako pia ulikuwa mpango.
Kila mtu anaweza kuweka mipango midogo midogo ya maisha ya kila siku ila wengi tunashindwa kuweka mipango mikubwa na ya muda mrefu ya maisha yetu.
Ni muhimu sana kuwa na mipango mikubwa ya maisha yako, na mipango hiyo iwe ya muda mfupi na ya muda mrefu. Ni muhimu sana kuwa na malengo kwenye maisha yako, kujua kwa nini unaishi na ni vitu gani unafanya kwenye maisha yako.
Kwa mfano nikikuuliza maisha yako yatakuwaje miaka ishirini ijayo ni vigumu kunijibu, miaka kumi ijayo pia hujaifikiria, miaka mitano nayo unaona ni mingi kuipangilia. Nikikuuliza mwaka mmoja au miwili ijayo kwa shida sana ndio unaweza kuniambia unayaonaje maisha yako.
Kushindwa kujua maisha yako yatakuwaje miaka kumi au ishirini ijayo ni kutokana na kukosa malengo na maisha yako. Ni kweli huna uhakika wa miaka hiyo mingi inayokuja ila kuipangilia hakuna unachopoteza, na kama utakuwepo utatimiza mengi zaidi.
Hakuna kinachoweza kufikiwa bila ya kuwa na malengo na mipango. Hebu fikiri kama kwenye mchezo wa mpira wa miguu kusingekuwa na magoli tungehesabu vipi ushindi? Kama nahodha wa meli hana ramani na uelekeo anaweza kuipeleka meli wapi? Mifano hii ya uhalisia ya kwenye maisha inaonesha ni jinsi gani ilivyo muhimu kuweka malengo kama tunataka kufika mbali na kama tunataka kufanya makubwa.
Ni muhimu kuweka malengo kwa sababu huwezi kufanya kila kitu. Kuna vitu vingi sana vinavyohusiana na shughuli unazofanya, na huwezi kufanya kila kitu. Ili kuchagua vipi vya kufanya na vipi vya kuacha ni lazima uwe na malengo. Kwa mfano kama unawinda ndege na kuna kundi la ndege, je utalenga kundi zima au utamlenga ndege mmoja? Kama ni mwindaji unayejua uwindaji ni lazima utamlenga ndege mmoja hata kama wapo mia moja. Hivyo ndivyo ilivyo kwenye uwekaji wa malengo kwenye maisha. Kwakuwa huwezi kufanya kila kitu ni muhimu kuchagua utafanya nini na kwa wakati gani.
Huenda umekuwa unaweka malengo kila mwaka na kila wakati ila inakuwa ngumu kwako kuyatimiza. Hii inatokana na makosa unayofanya wakati unaweka malengo yako.
Unaweza kuwa unaweka malengo ambayo hayakuhamasishi ama hayasukumi kufanya mambo makubwa.
Unaweza kuwa unaweka malengo madogo sana hivyo hayakufanyi ufanye mambo makubwa kulingana na uwezo wako.
Huenda unaweka malengo makubwa sana au huweki mipango na mikakati mizuri ya kufikia malengo yako.
Au unaweka malengo bila ya kuweka tarehe ya kuwa umefikia malengo hayo. Yaani malengo yako yanakuwa hayana mwisho hivyo hakuna kinachokusukuma. Kwa mfano unaweka malengo kwamba mwaka 2014 utanunua gari ni tofauti sana na ukiweka malengo kwamba mpaka kufikia mwezi wa sita mwaka 2014 utakuwa umenunua gari.
Hapa tumeona faida za kuweka malengo na baadhi ya vitu vinavyotuzuia kufikia malengo tunayojiwekea. Kwenye makala itakayofuata tutaona jinsi ya kuweka malengo na kuweza kuyafikia.
Fanya mabadiliko makubwa mwaka 2014 kwa kuanzia na mabadiliko ya jinsi unavyoweka malengo yako. Fanya 2014 kuwa mwaka wa mageuzi kwenye maisha yako.