Mwaka 2013 umefika tamati na kama tulivyoona kwenye makala Umefanya nini 2013 ni muda muafaka wa kila mmoja wetu kufanya tathmini ya mambo yalivyokwenda mwaka huu 2013.

  Na mimi kwa upande wa mtandao wa AMKA MTANZANIA napenda nifanye tathmini ndogo ya mwaka 2013 ulivyokwenda kwa mtandao huu.

amka

  Kabla ya yote naomba nitoe shukrani za dhati kwa wasomaji wote wa blog hii. Msomaji yeyote wa blog hii namwita MTANZANIA ALIYEAMKA kwa sababu kuna kitu fulani umejifunza kutokana na makala mbalimbali zilizopo kwenye blog hii. Nipende kukushukuru sana wewe mtanzania uliyeamka. Wewe ndiye uliyechangia mafanikio yaliyofikiwa na blog mpaka sasa.

  Nilianzisha blog hii tarehe 31/03/ 2013 kwa lengo kuu la kujisaidia mimi mwenyewe na wale wanaonizunguka kuwa na maisha bora kwa kuchukua hatua juu ya maisha yao. Kwa miezi mitatu iliyofuata niliandika makala tatu tu, hiyo ilisababishwa na kutokujipanga vizuri na pia kukosa wasomaji wa kutosha.

  Kwanzia mwezi julai ndio naweza kusema blog hii imekuwa hai kila siku mpaka leo hii. Angalau kila siku(siku tano za wiki) nimeweza kuandika na kuweka makala moja.

  Blog hii imetoka kuwa na watembeleaji chini ya hamsini kwa siku mpaka sasa ambapo ina watembeleaji zaidi ya elfu moja kwa siku.

  Watu wengi mmekuwa mkiniandikia barua pepe na kunipigia simu kunieleza jinsi makala mnazosoma kwenye blog zinavyowasaidia. Nimeweza kukutana na watu wengi na kukuza mtandao wangu kupitia blog hii.

  Nimepata mawazo mengi mapya, changamoto na ushauri mzuri kutoka kwa wasomaji walioniandikia.

  Pia nimeweza kupata fedha kutokana na kuuza bidhaa mbalimbali kupitia blog hii na pia kushauri watu ana kwa ana kuhusu mambo mbalimbali wanayofanya.

  Mafanikio yote haya yametokana na wewe msomaji wa blog hii. Kwa kusoma, kuwashirikisha wengine na pia kuniandikia umekuwa ukinitia moyo kutaka kuandika zaidi.

  Mwaka umeisha, na mwaka 2014 kuna mipango mingi mikubwa kwenye blog hii hivyo endelea kuitembelea na washirikishe marafiki zako nao watembelee.

 

  Mambo muhimu ambayo ni vyema ukayafahamu kuhusu blog hii(kama ulikuwa hujui)

1. Blog hii mpaka sasa inaendeshwa na mtu mmoja tu ambae ni mimi Makirita Amani. Kwanzia kudesign na kufanya marekebisho kwenye muundo wa blog, kuandika mpaka kusambaza makala nafanya mwenyewe. Watu wengi wanapowasiliana na mimi hufikiri tupo timu kubwa inayofanya mambo yote hayo. Nategemea kuwa na timu kubwa sana baadae ila kwa sasa bado nipo mwenyewe.

2. Makala zote unazozisoma kwenye blog hii nimeziandika mwenyewe na sio kukopy kutoka sehemu nyingine. Hii ni makala ya 184 kuandika ndani ya miezi sita. Kuwekuwa na baadhi ya watu ambao sio waaminifu wamekuwa wanachukua makala kwenye blog hii na kuweka kwenye blog zao.

3. Nimefanya marekebisho makubwa kwenye blog kuelekea 2014. Tumetoka kwenye www.amkamtanzania.blogspot.com na kwenda www.amkamtanzania.com . Pia nimefanya mabadiliko makubwa kwenye muundo wa blog. Hivi sasa kushare makala, kukoment na kulike inakuwa rahisi sana kwako msomaji. Pia makala zote kwenye blog nimezipanga kwenye makundi husika hivyo inakuwa rahisi kwako kutafuta makala unazopendelea. Kwa mfano kama unataka kuhamasika unakwenda kwenye hamasika, kama unataka kusoma kuhusu mafanikio unakwenda kwenye mafanikio.

  Nikushukuru tena kwa kuwa pamoja na niombe tuendelee kuwa pamoja na walete wengine wengi zaidi.

  Kwa siku hizi chache zilizobakia tutajikita zaidi kwenye makala za kuweka na kutimiza malengo, kwa sababu wengi wetu hii ni changamoto kubwa.

  Nakutakia kila la kheri kwenye sikukuu hizi.

  Tafadhali sema lolote kwenye maoni hapo chini kama tuko pamoja.