Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Huwa wanasema sehemu yenye hazina kubwa sana hapa duniani siyo kwenye migodi ya madini, bali kwenye makaburi.

Hiyo ni kwa sababu makaburi yamelaza watu waliokuwa na ndoto kubwa sana. Ndoto ambazo kama zingetimizwa, zingeleta mapinduzi makubwa sana hapa duniani.

Lakini kwa bahati mbaya sana, ndoto hizo hazikuweza kutimizwa na matokeo yake ni dunia kunyimwa fursa ya kunufaika na matokeo mazuri ambayo yangeweza kupatikana.

Zipo sababu nyingi zinazofanya watu kufa na ndoto zao kubwa, lakini inayoongoza ni watu kuishia njiani, hasa pale wanapokutana na ugumu.

Hiki ni kitu ambacho kimekuwa kinaonekana kwa wengi wanaoshindwa kupata mafanikio makubwa. Wanakuwa na malengo na matamanio makubwa ya mafanikio. Wanakuwa na msukumo wa kuianza safari na wanaianza kweli.

Lakini baada ya muda wanaiacha safari hiyo na kwenda kuanza safari nyingine. Ndani ya kipindi kifupi wanajikuta wamefanya na kuacha vitu vingi, huku wakiwa hawana mafanikio wanayoweza kuyaonyesha.

Tatizo siyo kwamba watu hawa hawawezi kupata mafanikio, tatizo wanaogopa na kukimbia ugumu wanaokutana nao kwenye safari ya mafanikio. Kila wanapoanza jambo wanakuwa na matumaini makubwa. Lakini ugumu unapoingia, matumaini yanazimika na wanaona jambo hilo haliwezekani tena.

Hicho ni kitu ambacho sitaki kitokee kwako wewe rafiki yangu, kwa sababu nimeshajiamulia kwamba mafanikio yako wewe ni wajibu wangu mimi.

Na ndiyo maana nakuambia kitu kimoja, unapaswa kufurahia pale unapokutana na ugumu kwenye safari yako ya mafanikio. Najua utashangaa, iweje ufurahie ugumu wakati unachotaka wewe ni urahisi?

Kuna sababu kubwa mbili za kufurahia ugumu kwenye safari ya mafanikio.

Moja ni ugumu ndiyo kipimo cha kwa kiasi gani unataka unachotaka. Asili ina uwezo wa kukupa chochote unachotaka. Lakini huwa kwanza inahakikisha mtu anakitaka kweli kitu kabla haijampa. Na hapo ndipo ugumu unapoingia.

Unapokutana na ugumu kwenye safari yako ya mafanikio ni ishara nzuri kwamba asili inakupima umejitoa kiasi gani kupambania kile unachotaka. Hilo ni jambo la kufurahia, maana ni kiashiria eneo hilo lina mafanikio.

Ogopa sana kitu chochote unachofanya halafu kisiwe na ugumu wowote. Ni mtego mbaya sana huo, kama kuona choo kwenye ndoto.

Mbili ni ugumu unapunguza ushindani. Kwa sababu watu wengi hawajajiandaa kwa ugumu, wanapokutana nao wanaacha kile walichokuwa wanafanya. Hivyo kadiri kitu kinavyokuwa kigumu, ndivyo wengi wanavyoacha kukifanya.

Sasa wewe huoni kwamba kama watu wengi wanaacha kufanya kitu, ushindani kwenye kitu hicho unakuwa mdogo? Zoezi la asili kupima kama kweli watu wanamaanisha, linawaondoa wale ambao ni waigizaji tu, ambayo hawajajitoa kweli kupata wanachotaka. Hivyo ushindani unakuwa mdogo.

Ogopa sana kitu kinachoweza kufanywa na kila mtu, thamani yake huwa siyo kubwa na ushindani ni mkali. Unapoona kitu kinaachwa na wengi kwa sababu ya ugumu wake, jua hapo umekutana na kitu sahihi, hivyo kifanye.

Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza kwa kina zaidi kwa nini unapaswa kuendelea na safari yako ya mafanikio hata pale mambo yanapoonekana kuwa magumu. Hiyo ni hali utakayokutana nayo sana kwenye safari yako ya mafanikio. Unahitaji silaha sahihi ya kupambana na hali hiyo, silaha unayoipata kwenye Barua hiyo.

Isome barua hapa; #BZK004; Jinsi Ya Kupata Msukumo Wa Kuendelea Kuishi Kusudi Lako Hata Matokeo Yanapokuwa Tofauti.

Rafiki, ugumu siyo mwisho wa safari, bali ni mlango wa kuonyesha kama kweli una tiketi ya safari hiyo. Furahia unapokutana na ugumu, kwa sababu unapima matamanio yako na kuwaondoa wengi kitu kinachopunguza ushindani.

Penda kufanya magumu na utaweza kujenga mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.