Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kwa namna nimesoma vitabu na kupitia mafunzo mbalimbali ya mafanikio, sikuwahi kudhani kuna mtu aliyeandika kwa kina kuhusu mafanikio na sijawahi kukutana na kazi zake kabisa.

Lakini hivi karibuni hilo limetokea, nimekutana na kazi za Art Williams, ambaye amefundisha na kuandika kwa kina sana kuhusu mafanikio, fedha na biashara, maeneo matatu ambayo ndiyo tumechagua kuyafanyia kazi kwa kina hapa.

Kitu cha kwanza nilichokutana nacho kumhusu yeye ni hotuba aliyoitoa mwaka 1987 kwenye mkutano wa watangazaji wa vipindi vya dini. Hotuba hiyo aliita DO IT na ilijaa hamasa na msukumo mkubwa kwa watu kuchukua hatua na kuacha kutoa visingizio.

Baada ya kutazama hotuba hiyo, nilitafuta kama ana vitabu ameandika na kukuta ana vitabu zaidi ya vitano alivyoandika kwa kina kuhusu falsafa hiyo ya kufanya. Nimevipata vitabu hivyo mara moja na kuanza kuvisoma na mambo aliyoandika ni ya kina sana kwenye hii safari.

Kwenye barua hii naenda kukushirikisha masomo ya msingi kutoka kwenye hotuba ya DO IT, ambayo tunapaswa kuyaelewa na kuyafanyia kazi ili tuwe watu wa kuchukua hatua na siyo tu kupanga na kusema. Kuchukua hatua hata kama ni ndogo sana kuna nguvu kuliko mipango na maneno mengi.

Safari Ya Mafanikio Ya Art Williams

Kabla ya hotuba yake, Art Williams alitambulishwa kwa wasifu wa safari yake ya mafanikio. Alianza kama kocha wa timu ya mpira ya shule za sekondari, kazi aliyoipenda sana, lakini ilimlipa kiasi kidogo.

Alitafakari kwa kina na kuona kazi hiyo haitaweza kumfikisha kwenye maisha ya ndoto zake, ndipo akaamua kuingia kwenye biashara ya kuuza bima za maisha (Life Insurance). Alianza mwenyewe na baadaye kujenga timu kubwa.

Ndani ya miaka 10 aliweza kujenga biashara kubwa sana, akiwa na timu kubwa na kuweza kuyapiku mashirika makubwa ya bima kwa kufanya mauzo makubwa kuliko mashirika hayo.

Mpaka kufika mwaka huo 1987 alikuwa na timu ya wafanyakazi 150,000 na alikuwa anafanya mauzo ya dola bilioni 100 kwa mwaka. Hayo yalikuwa ni mauzo makubwa kuliko kampuni mbili kubwa za bima ya maisha kwa wakati huo, Prudential and New York Life kwa pamoja.

Hebu fikiria rafiki, mtu anaingia kwenye biashara ambayo hakuwa anaifanya kabisa na ndani ya miaka 10 anapiga hatua za kuyazidi makampuni makubwa yaliyokuwa sokoni kwa miaka mingi. Ni dhahiri kwamba mtu huyo kuna vitu anavyojua, ambavyo vilimtofautisha na watu wengine.

Na vitu hivyo ndiyo amevishirikisha kwenye hotuba yake, ambavyo naenda kukushirikisha hapa na jinsi tunaweza kuvifanyia kazi kwenye safari yetu ya mafanikio, fedha na biashara.

1. Mambo Ya Msingi Ya Kupata Ushindi Kwenye Biashara.

“Ushindi kwenye biashara unatokana na mambo ya kawaida, kwanza tafuta hitaji ambalo wateja wanalo, kisha leta suluhisho na lipeleke sokoni. Na kama unataka kupata ushindi mkubwa zaidi, ni lazima uwe na upekee, uwe na kitu kinachokutofautisha wewe na washindani wote. Na kilicho muhimu zaidi kwenye ushindi wa biashara ni kuwa na uimara wa akili, usioyumbishwa na chochote. Unaweza kufanya asilimia 99 ya mambo yote kwa usahihi, lakini kama utakosa sifa hiyo moja, ya uimara wa akili, haitawezekana kabisa kushinda.”

Sina mengi ya kuongeza hapo rafiki, mambo yote ya msingi kwenye biashara tumekuwa tunashirikishana; kuwa na thamani (bidhaa/huduma), kupata wateja (usakaji), kuwashawishi wanunue (ukamilishaji), kuwafanya warudi kununua (uhudumiaji), kusimamia vizuri fedha (ukusanyaji) na kuwa na watendaji bora (timu).

Kitu kikubwa ambacho Art Williams ametuongezea hapa ni huo uimara wa akili. Na yupo sahihi sana, ukiangalia biashara zilivyo na changamoto, bila uimara wa kiakili ni rahisi sana kushindwa na kukata tamaa.

Ukiangalia watu wote ambao wameshindwa kwenye biashara, siyo kwa sababu hawana uwezo, bali kwa sababu walielemewa na biashara hizo. Kuanzia utendaji wa ndani mpaka ushindani wa nje.

Kitu muhimu cha kutoka nacho hapa ni kuhakikisha tunajenga uimara wa kiakili, kufanya akili zetu ziweze kuhimili kila tunachokutana nacho na kukivuka. Ushindi mara zote huwa upo upande wa pili wa ugumu ambao mtu anakutana nao.

2. Kuwa Na Shauku Kubwa.

“Ni lazima uwe na shauku. Watu hawawezi kukufuata au kukuamini kama upo hasi, umepoteza matumaini na kukata tamaa. Watu huwa wanawafuata watu walio chanya, walio na shauku na wenye matumaini. Karibu kila mtu anaweza kuwa na shauku kwa miezi miwili au mitatu. Wachache wanaweza kuwa na shauku kwa miama miwili au mitatu. Lakini washindi huwa wanakuwa na shauku kwa miaka 30, au muda wowote unaohitajika kupata ushindi.”

Rafiki, shauku ni kitu tumekuwa tunaimba hapa mara kwa mara, ni kwamba haiwezekani kabisa kupata ushindi mkubwa kama huna shauku. Hivyo tunapaswa kufanya kila linalohitajika kuhakikisha tumejijengea shauku kubwa ndani yetu.

Kuna kitu kimoja ambacho Art amesisitiza hapa, ni kwa muda kiasi gani tunapaswa kuwa na hiyo shauku? Ukiangalia, wengi sana huwa wanakuwa na shauku kwa siku mpaka miezi michache. Mtu anasoma kitabu, anahudhuria mafunzo na kutoka akiwa na shauku kubwa, lakini baada ya muda anarudi kwenye mazoea yake.

Washindi wa kweli wanakuwa na shauku kwa miongo mingi, maana hakuna ushindi unaopatikana kwa muda mfupi. Yaani shauku inakuwa siyo kitu cha kuvaa na kuvua, bali inapaswa kuwa kama ngozi yako. Unapaswa kuwa na shauku kubwa kwa kipindi chote cha maisha yako, bila kujali unapitia nini.

Hili ni somo kubwa sana tunalopaswa kutoka nalo hapa. Tusiwe na shauku za mihemko, bali tuwe na shauku za kudumu, wakati wote ili tuweze kupata ushindi tunaoutaka.

3. Rudi Kwenye Ndoto Zako.

“Ni lazima urudi kwenye ndoto zako. Tilibadili mchungaji wa kanisani kwetu wiki chache zilizopita. Kitu cha kwanza mchungaji wetu mpya alisema ni hiki; ‘Inaonekana kila mtu amekuja kanisani leo kumwona tumbili akifanya maonyesho. Lakini nataka niwaambie kitu kimoja, kwa kanisa kufanikiwa, ni lazima kuwe na ndoto. Kama huna ndoto, ni mfu.’”

“Kuwa na ndoto ni kuamini inawezekana. Nilipokuwa kocha wa mpira, nilikuwa na fimbo ofisini kwangu. Nilikuwa na sheria moja, mchezaji yeyote aliyesema ‘Siwezi…’ mchezaji mwingine alimleta ofisini kwangu na nilimtandika viboko vitatu. Ilinichukua takribani mwezi kuondoa hizo fikra za kushindwa kwenye timu yangu.”

“Watoto wangu Art Jr. na April walipokuwa wadogo na wanaanza kujifunza maneno, kila mara waliposema ‘siwezi…’ niliwapa adhabu ya kufanya pushapu tatu.”

“Hakuna lolote litakalokushinda kufanya kama unalitaka kweli.”

Rafiki, hapa Art amepiga mengi sana, lakini la msingi ni kurudi kwenye ndoto, kile ambacho tumekuwa tunakitaka sana kwenye maisha yetu. Kisha kuamini kwamba inawezekana kukipata.

Kama ambavyo alitumia nguvu nyingi kuondoa fikra za kushindwa kwa wachezaji na watoto, ndivyo tunavyopaswa kufanya kwetu wenyewe. Zipo njia nyingi za kujiadhibu ili kuondoa fikra za kushindwa. Moja ya njia hizo ni kuvaa raba bendi kwenye mkono wako na kila unapofikiria haiwezekani, unavuta na kujinasa kiasi cha kupata maumivu. Ukifanya hivyo, akili yako itajifunza mara moja kuachana na fikra hizo.

Kadhalika unaweza kuwaambia wanaokuzunguka wakutoze gharama fulani kila unapotumia neno ‘siwezi…’ au ‘haiwezekani…’. Hiyo itafanya usijidanganye kwa fikra hizo zisizo sahihi.

Unaweza kujiuliza kwa nini kwenye hili eneo la ndoto, kilichosisitizwa zaidi ni kuondoa fikra za ‘siwezi…’ Ukweli ni kwamba, kila mtu ana ndoto, huwezi kuwa hai na ukawa huna ndoto. Tatizo ni fikra zetu ndiyo zinatukwamisha, kuamini ndoto zetu haziwezekani. Tukiweza kuondoa hizo fikra za kushindwa na kutowezekana, tutaweza kufikia ndoto zozote tulizonazo, hata kama zinaonekana ni kubwa kiasi gani.

4. Kuwa Na Unachosimamia.

“Watu wamechoshwa na watu wasio na msimamo na wale wasio na ujasiri wa kusema ukweli. Wengi walipo kwenye biashara wamepata sifa mbaya. Wanaonekana kuwa kusema chochote, kuuza chochote na kufanya chochote ili tu kupata faida. Kama unataka kushinda, kuwa na kitu unachosimamia.”

Rafiki, alichoeleza Art hapa, japo kwa ufupi ni sababu kubwa inayopelekea wengi kushindwa lakini imekuwa haisemwi. Watu kukosa msimamo na kujikuta wakihangaika na kila wanachoona kinaweza kuwapa matokeo.

Hilo ndiyo limepelekea wengi kujaribu kila aina ya biashara, kukimbizana na fursa mpya kila wakati na bado hawafanikiwi. Wengi wameonekana walaghai kwa sababu ya kuwa tayari kusema chochote kitakachowaridhisha wengine. Wanaahidi chochote ili tu watu wawape kile wanachotaka. Matokeo yake ni kushindwa kutimiza yale wanayoahidi.

Ni muhimu sana tuchague eneo ambalo tutasimamia na kukaa kwenye hilo kwa muda mrefu. Matokeo ni lazima tutayapata, japo inaweza kuchukua muda. Lakini hilo ni afadhali kuliko kuhangaika na mambo mengi na kuishia kushindwa.

5. Kuwa Tayari Kutokueleweka.

“Kama unataka kushinda, kuwa tayari kutokueleweka. Njia pekee ya kueleweka na wengine ni kuwa wa kawaida. Niite chochote, lakini kamwe usiniite wa kawaida.”

Ukifikiria jinsi ambavyo watu wanapenda kujiweka kwenye kundi la ‘watu wa kawaida…’ unajionea wazi kwa nini watu wengi hawapati ushindi wanaoutaka.

Na inaweza kueleweka kibinadamu, watu wanapenda kukaa kwenye kundi la watu wa kawaida kwa sababu wanataka kueleweka na wengine. Ukishapambana tu kufanikiwa, huwezi kueleweka. Fikra zako na matendo yako yatakuwa tofuati kabisa na kundi kubwa la wanaokuzunguka. Hawataweza kukuelewa kabisa.

Kama huwezi kuwa tayari kutokueleweka, unakuwa umepishana na mafanikio makubwa. Kwa kuwa wengi wanaishi kwa kuigana, wewe utakapoamua kuishi kwa ndoto zako, utaonekana wa ajabu. Lakini ni wajibu wako kusimama kwenye kilicho sahihi, hata kama upo mwenyewe.

Kwenye #BaruaYaKocha kuna mambo 11 ya kujifunza kutoka kwenye hotuba hiyo ya Art Williams, yote ni muhimu kwako kuyajua na kuyafanyia kazi ili ufanikiwe.

Soma barua hiyo hapa; #BZK058; Wewe Fanya Tu (Just DO It)