Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Dunia imepitia zama mbalimbali, na kila zama zilikuwa na ‘kitabu chake’. Kitabu cha kila zama ikiwa na maana ya namna ya kufanikiwa kwenye zama husika.

Kulikuwa na zama za mawe, ambapo walioweza kutumia vizuri mawe walipata mafanikio kuliko ambao hawakuweza.

Zikaja zama za chuma, ambapo walioweza kutengeneza na kutumia zana za chuma walipata matokeo makubwa kuliko wasioweza.

Zikaja zama za kilimo, ambapo waliomiliki ardhi kubwa na yenye rutuba wakawa wanapata matokeo makubwa kuliko wengine.

Zama za mapinduzi ya viwanda zilibadilisha kabisa maisha ya wengi, huku waliomiliki viwanda wakiwa ndiyo wanufaika wakubwa.

Zama za kompyuta zikawa na manufaa kwa wenye maarifa na taarifa na kuweza kuzifanyia kazi kwa haraka.

Zama za mitandao ya kijamii zinaifanya dunia kuwa kijiji na wale waliomiliki mitandao hiyo kuwa na mafanikio makubwa kwa kuweza kuwa na hadhira kubwa. Hata ambao hawakumiliki mitandao hiyo, kwa kuwa na hadhira kubwa wakawa na mafanikio.

Sasa tumeingia kwenye zama za Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), ambazo ni zama za tofauti kabisa na tulivyozoea. Moja ya kitu cha tofauti kwenye zama hizi ni kila kitu kuwa sawa kwa watu wote.

Kwa mara ya kwanza, dunia imeweza kuwa na usawa mkubwa kwenye upatikanaji wa maarifa na taarifa. Huko nyuma kuna watu waliofanikiwa sana kwa kuwa na taarifa ambazo wengine hawana.

Lakini kwenye zama hizi, maarifa na taarifa ziko wazi kwa watu wote. Yeyote anayetaka kujua chochote, iko ndani ya uwezo wake kujua.

Tulitegemea zama hizi ziwe za kuleta usawa kimafanikio, kwamba watu wote wafanikiwe kwa usawa. Lakini hilo halitokei, badala yake wachache wanapata mafanikio makubwa huku wengi wakiendelea kubaki kwenye hali duni.

Kubaki kwa matabaka ya kimafanikio hakusababishwi na ubaguzi au upendeleo wowote. Bali kunasababishwa na kuwepo kwa nguvu ya ushindani inayofanya kazi, lakini wachache ndiyo wanaoijua na kuifanyia kazi.

Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia nguvu hiyo ya ushindani na jinsi tunavyopaswa kuitumia ili tupate mafanikio makubwa kwenye zama hizi.

1. Kasi; Thamani Kuu Inayotawala Nyingine Zote

Kwenye zama hizi ambazo karibu kila kitu kimekuwa na usawa, kasi ndiyo kitu pekee kinachoweza kukutofautisha na wengine na kukupa matokeo makubwa ambayo wengine hawayapati.

Pamoja na teknolojia kuendelea kwa kasi kubwa, bado sisi binadamu hatuna mabadiliko makubwa na ya kasi kuendena na kasi ya teknolojia. Hivyo watu wamekuwa wanaendelea kufanya mambo yao kwa mazoea waliyonayo, wakati hali imebadilika kabisa.

Ili kupata mafanikio makubwa kwenye zama hizi, ni lazima uichague kasi kama thamani kuu inayotawala mambo mengine yote. Kwa kila jambo, hakikisha unaliendea kwa kasi kubwa kuliko ulivyozoea na kuliko wanavyofanya wengine.

Kwa kuwa na kasi kubwa na kuchukua hatua ambazo ni sahihi, na kufanya hivyo kwa muda mrefu bila kuacha, lazima utapata matokeo ambayo wengine wanayakosa. Hilo halitokani na upendeleo wowote, bali kwa kuweza kugusa mengi kwa kasi kubwa unayokuwa nayo.

2. Kasi Kwenye Maamuzi; Tumia Taarifa Za Msingi Kuamua.

Kipindi cha nyuma watu walichelewa kufanya maamuzi kwa kukosa taarifa za kutosha. Tulidhani kwa zama hizi ambazo taarifa zinapatikana kwa wingi na kwa urahisi, watu wangefanya maamuzi kwa haraka.

Lakini mambo yamekuwa tofauti kabisa, pamoja na kuwepo kwa taraifa nyingi, bado watu wanachelewa kufanya maamuzi. Kilichotokea ni uwepo wa taarifa nyingi umewapa watu ganzi ya kufanya maamuzi.

Kwa urahisi wa kupata taarifa, watu wamekuwa wanatumia kama kisingizio cha kutokufanya maamuzi. Kila wanapotafuta taarifa, wanaona bado kuna taarifa nyingi zaidi wanazohitaji, na hivyo kuahirisha kufanya maamuzi.

Hili limeshamtokea kila mtu, kuna kitu unataka kufanya, unaingia kwenye AI ili kupata taarifa na taarifa unazopata ni nyingi. Na kila mwisho wa taarifa AI inakuuliza kama unataka zaidi, unasema ndiyo, na hapo unaletewa taarifa zaidi.

Hilo linasababisha mtu ujikute ukiwa umekusanya taarifa nyingi sana kiasi cha kuchanganyikiwa, usijua nini cha kufanya. Na unapochanganyikiwa, unaona unahitaji taarifa zaidi, ambazo unazitafuta na zinazidi kukufanya uchanganyikiwe.

Ili kufanikiwa kwa kuwa na kasi kwenye zama hizi, lazima uanze na kasi ya kufanya maamuzi. Kwa kitu chochote unachotaka kufanya na hivyo kuhitaji kupata taarifa, jua ni taarifa zipi za msingi unazohitaji.

Ukishajua taarifa hizo za msingi, tafuta hizo kwanza na ukishazipata, fanya maamuzi mara moja. Hata kama maamuzi utakayofanya kwa taarifa za msingi hayatakuwa sahihi, utakuwa umepiga hatua kwenye kuyafanya kuliko kutokuyafanya kabisa.

Ukishajiona unaendelea kutafuta taarifa kwa muda mrefu bila kufanya maamuzi, jua unajikwamisha kufanikiwa kwa kukosa kasi inayohitajika kwenye zama hizi. Wenzako wanaofanya maamuzi kwa taarifa za msingi wanapiga hatua wakati wewe umeganda kwenye kukusanya taarifa zisizokuwa na mwisho.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK111; Nguvu Pekee Ya Ushindani Uliyonayo Kwenye Zama Hizi Za Akili Unde