Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Nataka nikiri kwako kwamba nimebadilika. Najua hiyo siyo ‘breaking news’ kwako, kwa sababu unanijua, huwa najifunza kila wakati na nabadilisha na kuboresha yote ninayoyafanya. Lakini mabadiliko ninayokuambia hapa ni makubwa sana kiasi cha kuhitaji kutoa taarifa.

Kwa kipindi kirefu nimekuwa nahubiri sana umuhimu wa watu kuwa na biashara, kama njia huru ya kuingiza kipato na isiyobughudhiwa na mtu yeyote. Hiyo ni kwa sababu kupitia biashara, mtu anaweza kuwa huru kwa kadiri anavyotaka yeye.

Njia nyingi za kuingiza kipato, ikiwepo kuajiriwa na kujiajiri, zina ukomo mkubwa kwenye uhuru. Kwanza kabisa kipato chako kinategemea ufanyaji wako moja kwa moja, usipofanya, huingizi kipato. Na mbaya zaidi, kipato hicho kina ukomo, hata ufanye nini, huwezi kuvunja ukumo huo kwa urahisi na haraka. Kama umeajiriwa, mshahara unachukua muda kuongezwa. Na kama umejiajiri, unalipwa kwa kazi na/au muda na unalipwa wewe. Kwa kuwa una ukomo wa muda wa kufanya kazi, kipato chako pia kinakuwa na ukomo.

Kwa upande wa biashara, kunakuwa na uhuru mkubwa. Kwenye kipato, hakitegemei ufanyaji wako, hasa ukishaweza kujenga mifumo na timu. Na kwa sababu unaweza kutumia watu wengi, kipato chako hakiwezi kuwa na ukomo.

Kwa mantiki ya kawaida, nani asiyetaka kuwa huru kiasi hicho, akaingiza kipato kisicho na ukomo na akawa huru kupangilia muda wake mwenyewe? Ni mpaka unapogundua kwamba binadamu siyo viumbe wa mantiki ndiyo unaelewa kwa nini wengi wanakuwa tayari kupoteza uhuru huo wa kipekee.

Nikirudi kwenye mabadiliko yangu rafiki, nilichobadilika ni siamini tena kwamba kila mtu anapaswa kuwa na biashara. Kwa sasa naamini ni watu wachache sana wanaopaswa kujihusisha na biashara kwa namna yoyote ile. Walio wengi wanapaswa kutafuta kazi ya kuajiriwa au kujiajiri watakayofanya na maisha yao kuweza kwenda.

Na ieleweke, hakuna ubaya wowote kwenye chochote ambacho mtu anachagua kufanya, kama tu hakivunji sheria. Ambacho najaribu kuwaepusha nacho watu ni kujidanganya na biashara wakati hawapo ‘siriazi’ na biashara. Kutokuwa kwao siriazi kunapelekea washindwe kufanikiwa, halafu wanaanza kuwa mabalozi wabaya kwa wengine kuhusu biashara.

Hebu fikiria, wewe una shule, umeweka walimu wazuri, wanafundisha vizuri, lakini mwanafunzi hazingatii masomo. Anafeli mtihani wake wa mwisho na kusema shule haifundishi. Utachukuliaje hilo? Hivyo sasa ndivyo mimi ninavyoumia pale ninapoona mtu anawakatisha wengine tamaa kuhusu biashara, kwa sababu yeye alishindwa. Na ukiangalia alivyofanya mpaka akashindwa, ungeshangaa kama angeweza kufanikiwa.

Hayo ndiyo mabadiliko kwa upande wangu, kwa sasa siamini wala kushawishi kila mtu kuingia kwenye biashara. Na kiashiria cha kwanza kwa mtu ambaye hapaswi kuingia kwenye biashara ni swali linalofuata hapo chini.

Swali Moja Linaloashiria Mtu Hapaswi Kuhangaika Na Biashara.

“Ni biashara gani inayolipa, ambayo haitanibana sana na itanipa faida kubwa ndani ya muda mfupi?”

Zamani nilikuwa nikisikia swali hilo kutoka kwa mtu napata hamasa kubwa. Naona tunakaribia kuvumbua mfanyabiashara mpya na atakayeleta mapinduzi. Nilikuwa na shauku kubwa ya kushauri na kutoa nafasi ya kufundisha na kusimamia.

Ni mpaka nilipoona matokeo mengi ndiyo nikafunguka macho kwamba hilo ni swali ambalo ni bendera nyekundi. Kwa Kiingereza wanaita ‘red flag’, ukiona, kimbia, ni hatari.

Hilo swali lina vitu vitatu ambavyo haviwezi kabisa kuwepo kwenye biashara, na hata vikiwepo, haviwezi kwenda pamoja.

Kitu cha kwanza ni kutokujua biashara gani ya kufanya. Hii ni hatari kubwa kwa sababu utaangukia kwenye biashara ya aina yoyote na ambayo haitokani na uimara wako. Ni sawa na kwenda kucheza mpira wa kikapu kwa sababu umeambiwa unalipa, wakati wewe ni mfupi. Kama umeelewa, umeelewa.

Kitu cha pili ni biashara kutokukubana. Hii siyo tu hatari, bali pia ni dharau. Yaani mtu ambaye hajawahi kufanya kabisa biashara, anadhani anaweza kufanya biashara kama kitu cha mchezo hivi. Masihara hayo ndiyo yamewapoteza wengi sana.

Kitu cha tatu ni faida kubwa ndani ya muda mfupi. Hapo kwanza nicheke. Watu wasio kwenye biashara, wangejua kwamba waliopo kwenye biashara hawajui hata faida ni nini, wangetulia tu na mambo wanayofanya.

Ukiyatafakari hayo kwa kina, unajionea wazi kwa nini watu wengi sana hawapaswi kabisa kujihangaisha na biashara. Kwa sababu hawana maandalizi na kujitoa kwa kiasi kinachohitajika.

Kama bado upo kwenye maswali ya aina hiyo, lakini kweli una msukumo wa kuwa kwenye biashara, sijakupa hukumu ya maisha kwamba huwezi biashara. Ninachokuambia ni hujawa tayari bado, hivyo kama utaendelea kujijenga, utayapata majibu sahihi na kufanikiwa.

Ugumu Wa Biashara Ni Urahisi Wake.

Kichwa cha barua hii ni Kwa Jinsi Biashara Ilivyo Ngumu . . . swali ni je huo ugumu wa biashara uko wapi hasa? Maeneo mengi nimekuwa nakuambia biashara ni rahisi, na kila mtu anaweza kufanya. Lakini hapa tena naonekana kugeuka na kusema biashara ni ngumu. Unaona kama sieleweki?

Utanielewa tu, na yote yako sahihi. Ni kweli biashara ni rahisi, halafu pia ni ngumu. Na ugumu wa biashara ni huo urahisi wake. Yaani biashara inakuwa ngumu kwa watu wengi, kwa sababu ni rahisi sana.

Wacha nikuelezee biashara kwenye aya moja; Unapaswa kuwa na thamani, ambayo ni suluhisho la tatizo ambalo watu wanalo na wapo tayari kulipia kulitatua. Unapaswa kuwa na njia ya kuwafikia wenye tatizo hilo na kuwashawishi walipie suluhisho ulilonalo. Wale wanaokubali kulipia, unapaswa kuhakikisha wamepata suluhisho na limewasaidia. Unapaswa kuhakikisha pesa inayoingia ni nyingi kuliko inayotoka. Na unahitaji watu utakaowafundisha na kufanya hayo yote ili kila kitu kisikutegemee wewe.

Sasa hebu niambie, unahitaji shahada ya kitu gani ndiyo uweze kuelewa na kufanya mambo hayo ya msingi? Ni rahisi kabisa, yanaeleweka na yanafanyika. Na hilo sasa ndiyo tatizo lenyewe. Kwa jinsi biashara inavyokuwa rahisi kufanya, ndivyo watu wanakosa utulivu na kujikuta wakihangaika na mambo mengi yasiyokuwa na tija.

Na hilo ndiyo kusudi la barua hii, siyo kukuzuia wewe kufanya biashara, bali kukurudisha kwenye urahisi wa biashara kwa kuachana na mambo yanayofanya biashara kuwa na ugumu usio na lazima.

Kwenye barua hii nimekushirikisha maeneo matano ambayo kwa uzoefu wangu, hasa baada ya kufanya kazi kwa karibu na watu wengi waliopo kwenye biashara, nimeyaona yakiongeza ugumu kwenye biashara za wengi. Kama umejitoa kisawasawa kuingia na kufanikiwa kwenye biashara, ni lazima uachane nayo kabisa.

Soma barua hiyo hapa; #BZK057; Kwa Jinsi Biashara Ilivyo Ngumu, Nitakushangaa Sana Ukiwa Unahangaika Na Mambo Haya.