Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Inapokuja swala la pesa, wote tunaongea lugha moja. Kwa sababu pesa ndiyo kipimo cha thamani, kinachotuunganisha watu wote bila kujali tofauti zetu.

Lakini pia pesa ni kipimo muhimu cha mafanikio kwenye maisha. Japo kuna watu husema mafanikio ni zaidi ya pesa, lakini ni uhakika pesa haiwezi kukwepeka kwenye kupima mafanikio.

Kwa sababu pesa ni muhimu kwa ajili ya mambo mengine yote kwenye maisha kuwa vile ambavyo tunataka. Hata kama kuna vitu vingine tunavyohitaji zaidi, pesa inahitajika ili kuwezesha vitu hivyo kupatikana.

Kwa umuhimu huu wa pesa, ingepaswa kuwa ndiyo kitu ambacho kila mtu ana elimu ya kutosha kuihusu. Lakini cha kushangaza, pesa ndiyo kitu ambacho watu wengi hawana elimu ya kuwatosha.

Na kwa elimu ndogo ambayo imekuwa inapatikana kuhusu pesa, imeegemea upande mmoja zaidi, upande wa kutumia pesa. Waelimishaji wengi wamekuwa wanafanya kazi nzuri ya kuwapa watu elimu ya kuwa na bajeti, kuweka akiba na kufanya uwekezaji.

Hayo yote ni muhimu na mazuri, lakini yanawezekana pale tu mtu akishakuwa na pesa. Sasa, kupata pesa kwenyewe ni ‘kipengele’ kigumu ambacho watu wengi hawana elimu ya kutosha. Watu wamekuwa tu na mazoea ya kufanya kazi walipwe au kufanya biashara wapate pesa.

Watu wengi wanafanya kazi na biashara kwa juhudi kubwa, lakini bado pesa wanazopata haziwatoshelezi. Kinachosababisha hilo ni wengi kukosa elimu sahihi ya jinsi ya kupata pesa, ili waweze kuwa na aina ya maisha wanayotaka.

Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia njia tatu pekee za kupata pesa na jinsi ya kuzitumia kuongeza kipato ili kujenga maisha ya mafanikio unayokuwa unayataka.

1. Njia Ya Kwanza Ni KUTOZA FEDHA.

Hii ndiyo njia iliyozoeleka na inayotumika na wengi kwenye kupata pesa. Kwa njia hii, unawatoza watu fedha kwa kile ambacho unawapatia. Kwa walioajiriwa wanawatoza waajiri fedha ambayo wanalipwa kama mshahara, kwa ujuzi, muda na nguvu wanazotumia kutekeleza majukumu ya mwajiri.

Kwa wanaofanya biashara, wanawatoza wateja fedha ili wapate kile wanachotoa, iwe ni bidhaa au huduma. Njia hii inahusisha mabadilishano ya moja kwa moja baina ya pande mbili zinazohusika.

Hii ni njia ambayo kila mtu anaweza kuitumia kuingiza kipato, kupitia kile anachokuwa nacho na uwepo wa wengine wanaokuwa wanahitaji kitu hicho.

Pamoja na urahisi wa kutumia njia hii kupata pesa, ni njia ambayo inahitaji kazi kubwa endelevu ili kuendelea kupata pesa. Kama ni kazi, lazima mtu kufanya kazi ndiyo uweze kutoza. Kama ni biashara, lazima biashara iendelee kutoa bidhaa au huduma ndiyo iweze kutoza fedha.

2. Njia Ya Pili Ni KUONYESHA MATANGAZO.

Hii ni njia ya kupata pesa ambayo inahusisha kuwaonyesha watu matangazo ya vitu wanavyoweza kuwa wanavihitaji, kisha kulipwa na wale wanaotaka matangazo yao yaonekane.

Njia hii ina pande tatu; watu, mwenye watu na anayewataka watu. Anayepata pesa kupitia njia hii ni mwenye watu, ambaye anakuwa ametengeneza hadhira inayomfuatilia na inayomwamini. Anayewataka watu anakuwa na kitu anataka kupeleka kwa watu, lakini hana watu hao. Hivyo anakuwa tayari kumlipa mwenye watu ili awaonyeshe kile alichonacho.

Hii siyo njia iliyozoeleka na wengi, lakini ni njia yenye nguvu na matokeo makubwa. Ukiangalia makampuni makubwa duniani ambayo watu wanatumia huduma zao bure, wanapata pesa kwa kutumia njia hii.

Watu wamekuwa wanajiuliza mitandao ya kijamii inapataje pesa kama watu tunaitumia bure kabisa bila kulipia chochote. Na jibu ndiyo hilo, mitandao hiyo inakuonyesha wewe matangazo, na inalipwa na wale wanaotaka uone matangazo yao.

Watu wenye wafuasi wengi kwenye mitandao pia wamekuwa wanatumia njia hii kuingiza kipato. Watu wanapokuwa wanataka kuwafikia watu wengi, wanawatumia wenye wafuasi kuonyesha matangazo.

Pamoja na njia hii kuhitaji kazi kubwa kutengeneza hadhira kubwa, ni njia isiyohitaji kazi kubwa kuiendeleza. Ukishakuwa na hadhira kubwa, ni rahisi kuendelea kuikuza na kuendelea kutoza gharama kubwa zaidi kwa wanaotaka kuonyesha matangazo kwa hadhira yako.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK110; Njia Za Kupata Pesa Ni Tatu Tu, Acha Kujihangaisha Na Mengi Yasiyo Na Tija