Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Mtaalamu wa mahusiano Dr. John Gottman anasema kupitia uzoefu wake na tafiti nyingi alizofanya kwenye eneo la ndoa, anaweza kutabiri kwa uhakika kama ndoa itavunjika kwa kuangalia kitu kimoja tu. Anasema kama kunakuwa na dharau kwenye mahusiano, yaani mmoja wa wenza anamdharau mwenzake, au wote wanadharauliana, hayo mahusiano yanakuwa kwenye matatizo makubwa na yatapelekea kwenye talaka.

Hilo ni jambo ambalo halihitaji hata kusubiri utafiti ndiyo uweze kukubaliana nalo, huwa inaonekana wazi tu, pale ambapo watu hawaheshimiani, matatizo huwa mengi na mahusiano kuvunjika. Hii ni kwenye kila aina ya mahusiano, siyo tu ya ndoa.

Nimeitafakari dhana hii kwenye mahusiano kati yetu na mafanikio makubwa tunayopambana kuyajenga na kuona dharau inaweza kuwa moja ya vikwazo vikubwa. Wajibu wangu ni kuhakikisha wewe umefanikiwa, maana hayo ndiyo mafanikio yangu mimi. Hivyo chochote kinachoweza kuyazuia mafanikio yako, nahakikisha unakijua ili uweze kukiepuka.

Siyo Tu Kuwa Na Dharau, Bali Pia Kukosa Heshima Ya Kutosha.

Tatizo moja la dharau ni watu wanaweza kujiona hawana dharau, lakini bado wakashindwa kwenye jambo. Ni kweli wanaweza wasionyeshe dharau ya wazi wazi, lakini pia wakawa hawajaweka heshima ya kutosha kwenye kitu.

Kutokukipa kitu heshima ambayo kinastahili ni sawa tu na kuwa na dharau kwenye kitu hicho. Kwani hakuna kitu kinachoweza kuleta matokeo makubwa kama hakipati heshima kubwa ambayo kinastahili.

Hili ni muhimu sana kwenye mahusiano yetu na mafanikio makubwa tunayokazana kujenga. Tunaweza tusiwe na dharau za moja kwa moja kwenye mchakato mzima wa mafanikio, lakini kama hatutaupa heshima kubwa, bado itakuwa vigumu kwetu kuyapata.

Kwenye barua hii, tunaenda kuangalia maeneo matano ambayo tunapaswa kuacha kuyadharau na kuhakikisha tunayapa heshima kubwa na ambayo inastahili ili kufanikiwa.

Haya ni maeneo ambayo ukiona tu mtu anayadharau au hayapi heshima ambayo yanastahili, unajua wazi kabisa kwamba mtu huyo hawezi kupata mafanikio makubwa. Na hata kama atayapata mafanikio hayo, hataweza kudumu nayo kwa muda mrefu.

1. Jiheshimu Mwenyewe.

Kujiheshimu wewe mwenyewe ndiyo hitaji namba moja la mafanikio makubwa. Ni lazima ujiheshimu na kujithamini sana wewe mwenyewe. Kwa kufanya hivyo inapelekea kujiamini, kitu ambacho ni muhimu kwenye kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Safari ya mafanikio ina vikwazo na changamoto nyingi, ambapo itaonekana ni rahisi kuachana na safari hiyo kuliko kuendelea nayo. Kama hujiheshimu kwa kiwango kikubwa, inakuwa rahisi kwako kuachana na safari hiyo pale unapokutana na vikwazo.

Lakini pia, unawafundisha wengine jinsi ya kukuchukulia, kama hujiheshimu, watu wengine pia hawatakuheshimu. Hivyo ni muhimu sana kujiheshimu wewe mwenyewe, kama sehemu ya kuwafanya wengine nao wakuheshimu.

Unaweza kusema kwamba haujidharau, na unaweza kuwa sahihi kwamba hujionyeshi dharau za wazi wazi, lakini bado ukawa hujiheshimu kwa kiasi cha kutosha.

Kama kweli unajiheshimu, iweje unapanga vitu vya kufanya, lakini inapofika muda wa kuvifanya hufanyi? Kweli unajiheshimu kwa muda ulioweka kwenye kupangilia, halafu ifike wakati wa kutekeleza usifanye hivyo?

Kama kweli unajiheshimu, iweje unakatishwa tamaa na watu wengine na wewe unakubali kukata tamaa na kuacha? Kweli unayapa uzito maoni ya watu ambao hawajui nini unataka na hawana uwezo wa kipekee ulionao wewe?

Kama kweli unajiheshimu, iweje unakata tamaa pale unapochukua hatua na kupata matokeo ya tofauti na matarajio yako? kweli unajishimu kwa muda na nguvu ulizoweka kwenye kufanya na kuchagua kuzipoteza kabisa kwa sababu tu hujapata matokeo kwa mara ya kwanza?

Nadhani umeanza kujionea mwenyewe hapo rafiki yangu, kwamba kushindwa kujiheshimu kwa kiwango cha kutosha ndiyo chanzo kikubwa cha kushindwa kupata mafanikio makubwa.

Mengine yote yatakayokukwamisha yanakuwa yamepata nguvu kwa sababu tayari wewe mwenyewe hujiheshimu. Unapojiheshimu sawa sawa, kwa kiwango sahihi, hakuna lolote linaloweza kukuyumbisha.

Wengine kukukatisha tamaa haiwezi kukusumbua pale unapokuwa unajiheshimu wewe mwenyewe. Kwa sababu unakuwa unayaheshimu zaidi mawazo yako kuliko vile wengine wanavyoyachukulia.

Unapojiheshimu, hukubali kuacha kile unachosimamia kwa sababu ya watu ambao hawawezi kujiheshimu hata wao wenyewe. Unapojiheshimu, hukubali kupoteza muda, nguvu na umakini uliotumia kuweka malengo na mipango yako. Unahakikisha unatekeleza uliyopanga, kwa sababu uliyapanga ukiwa na akili timamu kabisa.

Ukiona unashindwa kusimamia mambo yako mwenyewe, jua unachokosa ni kujiheshimu. Unapaswa kurudisha heshima hiyo kwako mwenyewe mara moja kabla hujawafundisha wengine nao kutokukuheshimu.

2. Waheshimu Wengine.

Mafanikio makubwa unayoyataka, yapo kwa watu wengine. Uwezo wako wa kuyapata unategemea uwezo wa kuwashawishi watu wengi wakupe kile walichonacho, ambacho ndiyo unakihitaji kwenye safari yako ya mafanikio.

Unahitaji wateja wa kukubali kununua chochote unachouza, iwe ni biashara au utaalamu ulionao. Unahitaji wafanyakazi wa kukusaidia majukumu kwenye kile unachofanya. Unahitaji washirika mbalimbali ambao utashirikiana nao kwenye safari yako.

Utapata ushirikiano mzuri kutoka kwa wengi unaowahitaji kama utawaheshimu. Pamoja na malipo mengine unayoweza kuwapa watu, kuwaheshimu ni moja ya vitu muhimu vitakavyoimarisha mahusiano yako na watu hao.

Kuwaheshimu wengine kunaanza na kuwachagua kwa usahihi. Siyo watu wote unaweza kuendana nao kwa namna unavyotaka wewe. Hivyo ni muhimu uanze kwa kuwachagua watu walio sahihi, kulingana na matokeo unayotaka kupata. Ukishakuwa na watu sahihi, unawaheshimu na kuwaamini, ili waweze kukuamini na kukupa unachotaka.

Usiwadharau watu kwa kuona unaweza kupata wengine, kuna nguvu kubwa kwa watu ambao wamekuamini na kukukubali na kuwa na wewe kwa muda mrefu. Tambua na thamini mahusiano ya aina hiyo, ili uweze kuyatumia kupata matokeo makubwa unayoyataka.

Kuwaheshimu watu kunahusisha kuwaelewa watu hao na kujali maslahi yao, kwa kujua wanachotaka na kuhakikisha unawapatia kupitia mahusiano mnayokuwa nayo. Pia inahusisha kuwa na matarajio sahihi kutoka kwa watu hao na kuepuka kutegemea vitu ambavyo hawawezi kukupa.

Kutambua, kuthamini na kushukuru ni vitu ambavyo vitaimarisha sana mahusiano yako na watu wengine. Ni vitu vinavyowafanya watu kujiona wa kipekee kwako na kuendelea kukuonyesha ushirikiano mkubwa na wa karibu.

Kuwaheshimu watu pia ni kutokuingilia mambo yao, hasa pale yanapokuwa hayakuhusu na hawajakuomba ujihusishe nayo. Mara nyingi huwa tunajiingiza kwenye matatizo na watu wengine kwa kuingilia mambo yao ambayo hayatuhusu na wala hawajatutaka kujihusisha nayo. Mfano kuanza kutoa ushauri kwenye mambo ya watu, ushauri ambao unakuwa hujaombwa kutoa.

Kuwaheshimu watu haimaanishi kutaka kukubalika na kila mtu, lakini inamaanisha kuepuka kutengeneza uadui na watu walio wengi. Kama watu unaona hakuna namna mnaweza kushirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili, ni bora kila mmoja akaendelea na mambo yake.

Mahusiano na watu ni eneo linalohitaji umakini mkubwa, kwa sababu ya asili yetu binadamu kuwa viumbe wa hisia na siyo mantiki.

Kwenye #BaruaYaKocha kuna maeneo mengine matatu ya ziada ambayo unapaswa kuyaheshimu ili ujenge mafanikio makubwa. Yajue maeneo hayo na kuyafanyia kazi.

Soma barua hapa; #BZK056; Usipoacha Hizi Dharau, Hutaweza Kujenga Mafanikio Makubwa.