Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kwenye hadithi za kale za Ugiriki, tunaelezwa kuhusu Heracles aliyefanya kosa na kupewa adhabu na mfalme Eurystheus. Adhabu aliyopewa ilikuwa ni kuua joka kubwa lililokuwa na vichwa tisa. Heracles aliona hiyo ni kazi rahisi, akabeba silaha yake na kwenda kukabili joka hilo. Cha kushangaza, kila alipokata kichwa kimoja cha joka hilo, vichwa viwili viliota.
Akaona labda anachokosa ni kasi ya kukata vichwa hivyo, lakini kila alipoongeza kasi, ndivyo vichwa zaidi viliongezeka. Ni mpaka alipopata akili kwamba hata aongeze kasi kiasi gani, hawezi kushinda, hivyo akatafuta mbinu ya kuzuia vichwa zaidi visiote. Ndipo akagundua akichoma pale alipokata kichwa, vichwa vingine haviwezi kuota. Na hilo ndiyo lililompa ushindi.
Kupitia hadithi hii, kuna mambo mengi sana ambayo tunaweza kujifunza na kuyatumia kwenye safari yetu ya mafanikio. Kwa sababu kile alichopitia Heracles, ndicho tunachopitia kila siku kwenye hii safari tuliyochagua.

Dhaifu (Fragile), Imara (Robust) Na Inayoimarishwa Na Changamoto (Antifragile)
Nassim Taleb, kwenye kitabu chake kinachoitwa Antifragile, ameeleza kwamba watu, mifumo, taasisi na hata mataifa yamegawanyika kwenye makundi matatu.
Kundi la kwanza ni dhaifu, hivi ni vitu ambavyo vinaangushwa na changamoto ambazo vinapitia. Kitu kinakuwa dhaifu kiasi kwamba kinapokutana na changamoto, kinakwama na kuanguka.
Kundi la pili ni imara, hivi ni vitu vinavyoweza kustahimili changamoto ambazo vinapitia. Vitu hivi vinahimili changamoto ambazo vinakutana navyo bila kukwama na kuanguka.
Kundi la tatu ni inayoimarishwa na changamoto, ambavyo ni vitu vinavyokuwa imara zaidi pale vinapokutana na changamoto. Vitu hivi vinabaki vikiwa imara zaidi pale vinapopitia changamoto na magumu.
Kwa haraka haraka, unaweza kudhani kuwa imara ndiyo kuzuri, kwa sababu hakuna kinachokuangusha. Lakini kuna changamoto ambazo zinaweza kulegeza hata vitu ambavyo ni imara sana.
Hali ambayo inaweza kutusaidia kwenye safari yetu ya mafanikio, ni kuwa kwenye hali ya kuimarika kwa changamoto ambazo tunakutana nazo. Kwa sababu safari yetu ya mafanikio ina changamoto na vikwazo vingi, tutanufaika sana kama tutageuza changamoto hizo kuwa njia ya kujiimarisha zaidi.
Badala ya changamoto tunazokutana nazo kutulegeza na kutuangusha, zinatufanya kuwa imara zaidi na kutupa nguvu ya kuendelea kupambana. Kwa kifupi tunachukua tabia zote mbili tulizojifunza kwenye hadithi tuliyoanza nayo hapa. Tunakuwa na sifa ya joka ya kuota vichwa viwili kila kinapokatwa kimoja. Na pia tunakuwa na sifa ya Heracles ya kugundua wapi tunakwama na kufanya kwa ubora zaidi.
Karibu ujifunze jinsi ya kutumia changamoto unazokutana nazo kwenye safari ya mafanikio kukuimarisha ili kuendelea na safari hiyo na kuyapata mafanikio makubwa kwa uhakika.
1. Furahia Pale Watu Wanapokukataa, Kukupinga Au Kukukatisha Tamaa.
Moja ya vitu vinavyowakwamisha watu wengi kuchukua hatua zitakazowapa mafanikio ni kukataliwa, kupingwa na kukatishwa tamaa na wengine. Hilo linatokana na hali yetu sisi binadamu ya kupenda kukubalika na wengine. Pale inapotokea watu hawakubaliani na sisi, tunaona tuko upande ambao siyo sahihi.
Kwa sababu mafanikio makubwa ni kitu ambacho hakipo kwa wengi, hawatakubaliana na wewe kwa safari unayokuwa umeichagua. Watakukataa, watakupinga na kukukatisha tamaa kwa hicho unachokuwa umechagua kufanya.
Badala ya kuumizwa na hilo na kukata tamaa, unapaswa kulifurahia na likuhamasishe zaidi. Kama ambavyo joka liliota vichwa viwili kwa kila kimoja kilichokatwa, ndivyo wewe unapaswa kuwa na shauku zaidi ya kupata mafanikio pale wengine wanapokukwamisha.
Furahi sana pale watu wanapokukwamisha kufanikiwa, kwa sababu unaenda kuwaonyesha kwamba wamefanya makosa makubwa sana kwa kutokukuamini. Badala ya kukubaliana nao na kuwafanya waone wako sahihi, hakikisha unafanikiwa ili kuwaonyesha kwamba hawakuwa sahihi.
Wengine huwa wanasema uwe na hasira zaidi pale watu wanapokukwamisha, lakini mimi nimetumia furaha. Hasira pia inaweza kukusukuma, lakini ukishapata matokeo, hasira inaisha na unaweza kuanguka. Lakini kwa furaha, haina mwisho, kadiri unavyopata mafanikio ndivyo unavyozidi kufurahia.
Muuzaji mmoja wa nyumba kwa nyumba alikuwa anakutana na hapana kwenye milango mingi aliyogonga. Karibu angekata tamaa, mpaka pale alipogundua kitu kimoja kilichomsaidia sana. Kila alipogonga mlango, kabla mtu hajamkataa na kufunga mlango, alimwambia; ‘Niambie tu hapana na nitakuwa nimeingiza elfu tano.’
Wengi walishangazwa na kauli hiyo na kumuuliza kivipi anapata elfu tano kwa kuambiwa hapana. Aliwaeleza kwamba kwa kila milango 10 anayogonga, 7 anaambiwa hapana na 3 anauza. Anapouza kwa watatu, anapata elfu 50, ambayo akigawa kwa milango 10 aliyogonga, kila mlango ni sawa na amepata elfu 5, iwe ameuza au hajauza.
Hebu tafakari hilo rafiki, uone kama kuna namna ya mtu anayefikiri hivyo anaweza kukatishwa tamaa na jambo lolote. Habari njema ni wewe pia unaweza kugeuza kukataliwa na wengine kama furaha itakayokupa mafanikio makubwa zaidi. Jua tu jinsi ya kutumia kukataa kwao kupata shauku ya kuwaonyesha wamefanya makosa makubwa.
2. Pata Msukumo Mkubwa Zaidi Kila Unapokwama Na Kuanguka.
Kuwavuka watu wanaokukwamisha haimaanishi njia ya mafanikio itakuwa imenyooka. Bado utakutana na vikwazo na changamoto nyingi zaidi, ambapo utapata matokeo ambayo ni tofauti kabisa na ulivyotarajia. Na hapo ni baada ya kufanya kila ambacho ulipaswa kufanya.
Matokeo ya aina hiyo huwa ni rahisi kukatisha tamaa, na kudhani huenda wale waliokukataa walikuwa sahihi. Pale unapopata matokeo mabaya, maneno ya waliokukatisha tamaa yanakujia. Unaona labda ni kweli huwezi au haiwezekani.
Lakini hupaswi kukubali safari yako ya mafanikio imalizwe na matokeo mabaya unayoyapata. Kwani hayo yataendelea kuwepo, kwa kadiri unavyochukua hatua za mafanikio.
Wajibu wako ni kuyatumia matokeo mabaya kama msukumo wa kufanya makubwa zaidi. Kama ambavyo Heracles aliendelea kupambana na joka licha ya kuota vichwa viwili kwa kila kimoja alichokata, ndivyo pia unavyopaswa kuendelea na safari yako licha ya matokeo mabaya unayopata.
Tambua kwamba matokeo siyo mwisho wa safari, bali ni sehemu ya safari yenyewe. Hivyo matokeo ni kama kiashiria kwako cha vitu gani vya kuboresha zaidi ili uweze kufika kule unakotaka.
Na zaidi, usikubali matokeo yakawa ndiyo yanabeba utambulisho wako, hicho ni kitu cha mpito tu, ambacho utakivuka na kupata mafanikio unayoyataka.
Kila unapokwama na kuanguka, amka ukiwa na msukumo wa kuendelea zaidi. Ona kila unachopitia kama maandalizi ya kupata ubingwa, ambao ni mafanikio unayoyataka.
Kama inavyosema mithali maarufu ya Kijapani; “Anguka mara saba, inuka mara nane”, wajibu wako ni kuhakikisha idadi yako ya kuinuka ni kubwa kuliko idadi ya kuanguka.
Kama kila unapoanguka unainuka tena, na tena na tena, hakuna namna chochote kinaweza kukuzuia kupata mafanikio makubwa unayoyataka. Kila unachokutana nacho kinakuwa kimekuimarisha zaidi kuliko kukudhoofisha.
Soma barua kamili hapa; #BZK055; Tumia Changamoto Kuwa Imara Zaidi Kwenye Safari Ya Mafanikio.