Rafiki yangu Mpendwa,
Jambo moja la kushangaza sana kwenye maisha ni chochote unachokuwa unakazana kufanya ili kupata matokeo fulani, huwa unaishia kukosa matokeo hayo.
Kama unakazana sana kufanya vitu ili watu wakupende, vitu hivyo hivyo unavyokuwa unafanya ndiyo vinawafanya watu wasikupende.
Kadhalika, unapokazana kufanya aina fulani ya vitu ili watu wakuamini na kukuthamini, ndivyo unafanya watu wazidi kukosa imani na wewe.
Kwa kifupi ni kitu unachokiwekea juhudi sana, kwa lengo la kupata matokeo ya aina fulani, hasa kutoka kwa watu wengine, kinaleta zaidi wasiwasi kwa watu hao.
Wanachokuwa wanajiuliza watu ni kama kweli mtu ana kitu hicho, kwa nini atumie nguvu kubwa kutuaminisha anacho?
Na tumejifunza kupitia watu wanaotuzunguka, wale wanaokazana kuonyesha ni waaminifu huwa ndiyo siyo waaminifu. Wanaokazana kuonyesha kwa nje kwamba wana furaha, kwa ndani hawana furaha.
Watu wamekuwa wanawasema sana wasanii kwenye hili, huwa wanajionyesha kwamba wana fedha nyingi na maisha ya viwango vya juu. Lakini wanapopata matatizo wanarudi kuomba michango kwa mashabiki wao.
Tunaliona hilo kwa wasanii kwa sababu wanaonekana na wengi. Lakini ndivyo lilivyo kwa kila mtu, chochote ambacho mtu anakazana sana kuonyesha, anakuwa hana.
Kwenye kushirikiana na watu wengine, unahitaji sana kuaminiwa na kuthaminiwa. Lakini kama ambavyo tumeshaona, ukitumia nguvu nyingi kuwaonyesha watu kwamba unapaswa kuheshimiwa, ni kama unawaambia hawapaswi kabisa kukuheshimu.
Hivyo hatuwezi kutumia njia hiyo ya kutaka kutoka kwa watu moja kwa moja. Badala yake tunahitaji kujenga aina ya maisha ambayo watu wakiyaona, wao wenyewe wanachagua kutuheshimu na kututhamini.
Yaani tunafanya mambo kwa ajili ya matokeo fulani tunayokuwa tunataka kuyapata, na kama kitu cha ziada, watu wanatuheshimu na kututhamini. Wakati tunafanya lengo haliwi kupata heshima, bali matokeo tunayokuwa tunayataka. Lakini, kupitia kupata matokeo hayo, heshima pia inakuja.
Kwenye hii #BaruaYaKocha nimekushirikisha mambo ya kufanya, ambayo lengo lake siyo kupata heshima na thamani moja kwa moja, lakini unapoyafanya, watu wanakuwa hawana budi bali kukuheshimu na kukuthamini.

1. Fanya Kile Ambacho Wengi Hawapo Tayari Kufanya.
Ukiwaangalia watu wanaopata mafanikio makubwa, wana tofauti moja tu na wanaoshindwa. Wanafanikiwa wanakuwa tayari kufanya mambo ambayo walioshindwa hawapo tayari kuyafanya. Na wanakuwa kabisa hawataki kuyafanya, lakini kwa sababu wanataka sana mafanikio, wanayafanya. Na kupitia kuyafanya ndiyo wanapata matokeo ya tofauti.
Ukiangalia kwenye tasnia yoyote ile, iwe ni kazi, biashara au sanaa, utaona watu wengi sana ambao wanaonekana kushindana. Wengi wakiona jinsi eneo lina watu wengi, wanahofia na kuona ushindani utakuwa mkali.
Lakini ukweli ni huu, kuna mtu mmoja tu ambaye ndiye huwa ni mshindani wa kweli kwenye tasnia yoyote ile. Haijalishi ni watu wangapia wapo, wawe ni mia, elfu au zaidi, anayeshindana hasa ni mmoja tu.
Ushindani wa kweli utatokea pale wewe utakapoamua kufanya ambacho wengi hawapo tayari kufanya. Na uzuri ni kwamba katika ngazi hiyo, utakuwa unashindana na mtu mmoja tu, ambaye ndiye amejitoa kweli.
Wengine wote, wapo tu kusindikiza kwenye huo mchezo, hawana hata mpango wa kupata ushindi. Wao wapo wapo tu na ndiyo maana hawapati matokeo. Sasa kama na wewe utaingia na ukawa upo upo tu, utakuwa umejipeleka kwenye kusumbuliwa.
Labda nikuchambulie mgawanyiko wa watu waliopo kwenye eneo lolote ili ujionee mwenyewe.
Sehemu kubwa kabisa ya watu wanakuwa wana hofu hata ya kuanza tu. Hawa wanakuwa watu wa mipango, kujiandaa, kujifunza, kufanya tafiti na mengine. Ila kuanza ndiyo kitu kinachowapa hofu kubwa.
Sehemu ndogo inayofuata wanaanza, lakini wakishindwa mara tatu wanaacha na kusema haifanyi kazi. Hawa wanaondolewa haraka na magumu na changamoto zinazokuwa kwenye ufanyaji.
Sehemu ndogo zaidi inayofuata ina watu wanaovuka kwenye magumu na changamoto, ila wanaenda kwa mwendo wa polepole sana kiasi cha kushindwa kuchangamkia fursa nyingi nzuri zilizopo kwenye kile wanachofanya. Wanakuwa wapo, lakini hawapati matokeo makubwa.
Sehemu ndogo zaidi zaidi ya wanaoenda kasi, wanasumbuliwa na fursa mpya zinazojitokeza. Hawakai kwenye kitu kimoja mpaka kikawapa matokeo makubwa. Hawa wanapata matokeo, lakini siyo makubwa sana kwa sababu ya usumbufu.
Na mtu mmoja, ndiyo, mmoja tu, ndiye anayekuwa mshindi hasa, anayepata matokeo makubwa. Kama na wewe utaamua kwamba unataka ushindi hasa, na kuvuka hizo sehemu za chini, hapo kileleni mtakuwa wawili tu, ambao ndiyo mmedhamiria kweli kufanikiwa.
Swali ni je kwa hicho unachofanya, unajiona ukiwa kwenye sehemu ipi? Kama unahofia hata kuanza, unadhani kuna atakayekuheshimu? Kama unaanza lakini unapokutana na magumu unaanza, unataka watu wakuthamini?
Nenda pale kwenye kilele, pambana hasa na utapata ushindi, huku pia heshima ikiwa kubwa. Maana wengi walioshindwa, watakuona wewe uliyeshinda unastahili heshima ya kipekee.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK105; Kama Kuna Watu Unataka Wakuamini Ila Hawakuamini, Fanya Mambo Haya