Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya sababu zinazopelekea watu wengi kukwama kwenye maisha ni kushindwa kujua ni nini hasa kinachowakwamisha.
Kama inavyojulikana, kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua. Hivyo kwa kutokujua kile ambacho kinawakwamisha, watu wamejikuta wanahangaika sana na mambo yasiyokuwa sahihi.
Kwa mtu kutokufanikiwa kabisa kwenye kipindi chote cha maisha yake siamini kama inatokana na ujinga, uzembe na kutokuwa na uwezo peke yake. Naamini kuna hujuma zinakuwa nyuma ya kushindwa kwa kila anayepambana kufanikiwa ila anashindwa.
Kwa bahati mbaya sana, watu wengi wanaoshindwa hawajui kama kuna hujuma zinazowapelekea kushindwa. Hivyo wao wanaendelea kukazana kufanikiwa, huku hujuma za kuwarudisha nyuma nazo zikiendelea kuwa kubwa.
Matokeo yake ni watu kuchoka sana na kuamua kukata tamaa, kwa kuona hakuna namna wanaweza kufanikiwa.
Hivyo sivyo inavyopaswa kuwa, ndiyo maana nimekuwa nakupambania sana wewe rafiki yangu, kwa sababu najua ipo ndani ya uwezo wako kabisa.
Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia huo upande wa hujuma ambazo zimekuwa zinakukwamisha kupata mafanikio makubwa licha ya juhudi kubwa sana ambazo unaendelea kuweka. Ni vitu vidogo sana ambavyo ukivifanyia kazi unakuwa umeachilia breki kali zinazokukwamisha.

1. Ni Vigumu Sana Kushindwa Kwa Msimamo.
Siku za karibuni nilikuwa naangalia mahojiano ya Grant Cardone kwenye podcast moja na akasema kitu ambacho kimenifikirisha na kunisukuma kukuandikia barua hii. Alikuwa anaelezea baadhi ya mambo yanayofanywa na serikali na kupelekea kushindwa kutekeleza mambo rahisi na ya msingi kabisa.
Cardone akasema; “Siamini kama unaweza kukusanya uzembe kwa msimamo kiasi hicho. Ni lazima kuna makusudi.”
Ukisoma au kusikia kwa haraka, unaweza kuona ni malalamiko mengine tu juu ya kushindwa kwa mifumo ya kirasimu. Lakini unapotafakari kwa kina na kuyaangalia maisha yetu binafsi, unaona vitu vinaanza kuungana.
Kiuhalisia, unahitaji akili kubwa sana ili uweze kukosea kwa msimamo mara zote. Kwa sababu katika hali ya kawaida, mtu anayefanya jambo lolote kwa muda mrefu, kuna mahali atafika na kupatia.
Kama ulivyo usemi kwamba hata saa mbovu huwa sahihi mara mbili kwa siku, ndivyo ilivyo kwenye maisha, hata aliye mzembe kabisa, kuna wakati atafanya kwa usahihi.
Hilo linafanya tuhoji kwa nini mtu aishi maisha yake yote katika hali ya kushindwa, wakati kila siku anaonekana akipambana sana kufanikiwa.
Kitendawili ambacho kwa wengi kimekuwa hakieleweki, cha watu wanaokuwa kwenye mazingira ya aina moja, baadhi kufanikiwa na wengine kushindwa, kinapata majibu sasa.
Wale wanaoshindwa ni kwa sababu ya hujuma. Zinaweza kuwa hujuma za ndani yao wenyewe au za nje, lakini ni lazima kuna hujuma. Kwa sababu, haiwezekani kabisa wakashindwa kwa kipindi chote licha ya kuonekana wakiweka juhudi kubwa.
2. Asili Ya Binadamu Inakataa Kabisa Mtu Kubaki Chini Wakati Wote.
Ukimwambia mtoto mdogo asishike moto kwa sababu ataungua, anaweza kukusikiliza. Lakini hatakuamini, ataona labda unamnyima tu mchezo unaoweza kuwa mzuri kwake. Hivyo atakachofanya ni kuushika moto, halafu ataungua. Na tangu hapo atajifunza kutokushika tena moto, kwa sababu unaunguza na kuunguza kunauma.
Hiyo ndiyo asili ya binadamu, kujifunza kutokana na matokeo ya kitu na kisha kubadili tabia ili kuzuia maumivu yasijirudie. Ni asili hiyo ya binadamu ndiyo imetufanya tuwe hai mpaka leo.
Fikiria jinsi ambavyo maisha ya kushindwa yanavyoumiza na kudhalilisha, halafu mtu awe na maisha hayo kwa kujirudia rudia miaka nenda miaka rudi! Ni kitu ambacho kiuhalisia kinakataa kabisa.
Kwa asili, tayari umeshajifunza na kuboresha maeneo yote yanayokukwamisha na kukupa maumivu. Eneo lolote linalojirudia rudia kukukwamisha, ni kwa sababu ya hujuma ambazo zinakuwa zinaendelea kwenye eneo hilo.
Na kama hutazitambua hujuma hizo na kuziondoa, utahangaika sana lakini hutafanikiwa. Na hapo ile kauli ya kila unapopata ufunguo wa mafanikio kuna mjinga anabadilisha kitasa, itaonekana kuwa ya kweli. Vile tu kitasa chako kinakuwa ni hujuma mpya zinazokurudisha pale unapokuwa umeanzia.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK104; Ni Hujuma, Hakuna Ujinga Wenye Msimamo Kiasi Hicho