Maisha ya mwanadamu ni mpangilio wa hatua mbalimbali ambazo mtu huzipitia katika vipindi mbalimbali. Mtu anazaliwa, anaanza kukaa, halafu anatembea, anakua na kufikia kipindi cha kuanza shule, anafikia ujana, anaendelea kukua na kumaliza shule. Akimaliza shule anaingia kwenye ulimwengu wa kazi, anaanza maisha ya familia na anaendelea kukua na kuwa mtu mzima, baadae anakuwa mzee na anakufa.

Kila mtu anapitia hatua hizo kwa aina tofauti, kuna ambao labda hawataenda shule, au wataenda shule kwa kipindi kifupi. Kuna ambao labda hawataanza familia au watachelewa kuanza familia na kuna ambao labda hawatafanya kazi. Na pia kuna ambao watakufa mapema kabla ya kufikia uzee. Lakini kwa vyovyote vile kila mmoja atapitia hatua mbalimbali kuanzia kuzaliwa mpaka kufa.

Katika hatua hizi za maisha kuna mambo mengi sana ambayo tunafundishwa na mengine tunajifunza wenyewe. Mambo mengi tunafundishwa kupitia familia, jamii, mfumo wa elimu na elimu nyingine zisizo rasmi. Mambo haya ambayo tumekuwa tunafundishwa yametusaidia kwa kiasi kikubwa sana kwenye maisha yetu. Pia kuna mambo ambayo hatupati nafasi ya kufundishwa katika sehemu yoyote ile. Haya ni mambo ambayo tunajifunza wenyewe na mara nyingi huwa tunajifunza mambo haya kupitia njia ngumu, yaani unashindwa kwanza ndio unapata somo kwamba kitu fulani hakifanyiki kama ulivyofikiri awali.

Katika mambo ambayo tunafundishwa na katika mambo ambayo tunajifunza, kuna jambo moja muhimu sana ambalo tunalikosa. Yaani kuna jambo moja muhimu sana kuhusu maisha ambalo hatupati nafasi ya kufundishwa na wazazi, jamii wala mfumo wa elimu. Na mbaya zaidi bado hatupati nafasi ya kujifunza jambo hilo kwa njia ngumu kama tunavyojifunza mambo mengine. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba jambo hili ni muhimu sana kwenye maisha yetu na ndio linafanya maisha kuonekana ni magumu sana kuliko ambavyo yangetakiwa kuwa.

Je ni jambo gani hilo? Utapata nafasi ya kulijua hapa na jinsi unavyoweza kulitumia kurahisisha maisha yako ili yawe bora zaidi.

Kabla hatujalijua jambo hilo, hebu fikiria mfano huu; Unapozaliwa na kuanza kukua, hasa pale aunapokuwa shuleni umekuwa ukiaminishwa kwamba kama utasoma kwa bidii na ukafaulu vizuri basi utapata kazi nzuri na maisha yako yatakuwa mazuri sana. Ukaliamini hilo, ukasoma kwa bidii sana ukiamini kwamba pale tu masomo yatakapoisha na ukaanza kazi basi maisha yako yatakuwa mazuri sana. Shida zote ambazo ulikuwa unazipata zitaisha na sasa utawezakufurahia maisha. Lakini je ni nini ambacho kinatokea baada ya kumaliza masomo na kuingia kwenye kazi? Mambo yanakuwa tofauti na ulivyofikiri mwanzo, matatizo yanakuwa tofauti na yale uliyokuwa unapata mwanzo. Unapata kazi ambayo huenda huipendi, bosi wako anakusumbua, haelewi anakuona kama vile hufanyi kazi. Au watu unaofanya nao kazi hamuendani, kila siku ni kusumbuana, majungu mtindo mmoja na kila ukikazana kufanya kazi yako vizuri wanakuona kama una kihere here. Au unafanya kazi kwa bidii sana, lakini kipato hakitoshelezi mahitaji yako, unaingia kwenye madeni na hivyo unajikuta kila unapopokea mshahara unakwenda kulipa madeni na kuanza tena kukopa siku chache baadae.

Unajiangalia katika mambo yote haya na kuona labda wewe una bahati mbaya, labda wewe ulipangiwa kuwa na maisha magumu. Unajaribu kufanya biashara lakini pia unaingia kwenye hasara, watu unaofanya nao biashara wanakudhulumu, au wafanyakazi wanakuibia, au hawafanyi kazi kwa bidii.

Unajifunza nini kwenye mambo hayo au mengine yanayotokea kwenye amisha yako kila siku? Hilo ndio somo muhimu sana ambalo unapaswa kujifunza kuhusu maisha.

Na somo hilo ni kwamba MAISHA SIO RAHISI NA HAYATAKUWA RAHISI KAMWE. Huu ni ukweli ambao hakuna mtu amewahi kukuambia. Na hata hatua mbalimbali za maisha unazopitia zimekuwa zikikufundisha hili lakini bado hujaweza kuling’amua. Maisha sio rahisi na wala hayatakuwa rahisi siku za usoni.

Kila hatua unayopitia kwenye maisha ina changamoto zake. Wakati unazaliwa na ukiwa mchanga kabisa ulikuwa na changamoto ambazo ulizipita ndio ukakua. Wakati unasoma ulikuwa na changamoto ambazo ulizivuka ndio ukamaliza masomo yako. Na hata sasa kwenye maisha yako ya kazi au biashara kuna changamoto nyingi ambazo utazipitia kila siku. Ndivyo maisha yalivyo na huwezi kukwepa hilo.

Kila mmoja anapitia changamoto hizi. Japo kwa nje unaweza kuona watu wengine maisha yao ni mazuri kuliko ya kwako. Unaweza kuona mtu anaishi kwenye nyumba nzuri, anaendesha gari zuri na kuonekana kuwa na kazi au biashara nzuri ambayo inampendeza. Lakini ukipata nafasi ya kuishi kwenye maisha ya mtu huyo ndio utaujua ukweli halisi wa maisha yake, unaweza kukuta gari anayoendesha ni ya mkopo ambayo inamfanya kipato chake kikatwe kwa sehemu kubwa sana, au ni mbovu kiasi kwamba kila mara inamhitaji kufanya matengenezo kitu ambacho kinamgharimu sana. Unaweza kukuta nyumba anayoishi ina migogoro mingi, au haelewani na mume au mke wake. Au watoto ni watundu, wengine wanatumia mihadarati.

Kwa vyovyote vile maisha ya kila mtu yana changamoto zake.

Ufanye nini sasa?

Kwa hiyo kama maisha sio rahisi na hayatakuwa rahisi ndio nikubwali maisha yangu yawe hovyo kila siku? Hapana, huna haja ya kufanya maisha yako kuwa hovyo kila siku. Unapaswa kujua hili ili kuweza kuishi maisha yako kulingana na hali halisi.

Kwanza ishi maisha yako kwa kipindi ambacho upo. Jua kabisa kila hatua ya maisha yako ina changamoto zake. Na jua kwamba kwenye kutatua changamoto hizi ndio maisha yanakuwa na maana. Usifikiri kwamba changamoto hizi zitapita zenyewe au zikishaisha ndio maisha yako yatakuwa mazuri. Zikiisha changamoto hizo zitakuja changamoto nyingine. Hivyo tatuz changamoto unazopitia kwenye kila hatua.

Pili jua kwamba furaha hailetwi na mtu au kitu. Tumewahi kulijadili hili kwenye makala; hii ni haki yako ya msingi ya kuzaliwa. Usifikiri kwamba ukifikia kitu fulani kwenye maisha yako ndio utakuwa na furaha. Usifikiri kwamba ukshakuwa na fedha nyingi ndio utakuwa na furaha, au usitegemee mume au mke wako ndio atakuletea furaha. Furaha ni kitu ambacho kinatakiwa kuanza na wewe bila ya kutegemea hali ya nje. Furahia kila hatua unayopitia kwenye maisha yako. Hakuna siku utaamka ndio ukutane na kibao kwamba leo umeifikia furaha.

Tatu chukua hatamu ya maisha yako. Maisha unayoishi ni yako, usikubali kuiga ya mtu mwingine yeyote na wala usikubali kudanganywa na mtu mwingine yeyote. Weka malengo na mipango kwenye maisha yako na yafanyie kazi ili uweze kufikia kile ambacho una uwezo wa kukifikia. Jijengee tabia ambazo zitakuwezesha kuvuka changamoto unazokutana nazo kwenye maisha ya kila siku.

Chukua hatua sasa, sio kesho na wala sio baadae, ni sasa. Amua kubadili maisha yako.

Naamini kila mtu ana uwezo mkubwa sana ulioko ndani yake ambao kama akiweza kuutumia anaweza kubadili maisha yake na kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa.

Naamini kwamba kila mtu amezungukwa na fursa nyingi sana ambazo kama akiweza kuzitumia anaweza kuboresha maisha yake.

Ninafanya kazi na watu kuwawezesha kutumia uwezo wao mkubwa na fursa zinazowazunguka kuboresha maisha yako na kufikia mafanikio makubwa. Karibu tufanye kazi pamoja, Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA na kisha niandikie kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Pia karibu kwenye semina ya siku 21 ya kuufanya mwaka 2015 kuwa bora kwako. Semina itafanyika kwa njia ya mtandao na itaanza tarehe 05/01/2015. Mwisho wa kujiunga ni tarehe 31/12/2014. Wahi sasa ili upate nafasi hii muhimu ya kuboresha maisha yako. Kujiunga tuma ada tsh elfu kumi pamoja na jina na email yako kwenye namba 0717396253/0755953887.

Nakutakia kila la kheri katika kuboresha maisha yako.

TUPO PAMOJA.

Usisahau kutoa maoni yako na ushuhuda wako jinsi ambavyo AMKA MTANZANIA imebadili maisha yako. Bonyeza hapa na ujaze fomu, maoni yako ni muhimu sana.

kitabu-kava-tangazo4322