Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa wanalalamika jinsi ambavyo mambo ni magumu, lakini kwenye ugumu huo huo kunakuwa na watu wanaopiga hatua kubwa.
Kumekuwa na malalamiko ya ushindani mkali kwenye kila eneo, lakini kwenye ushindani huo huo, kuna watu wanaibuka washindi.
Kila unapowaangalia wale wanaoshinda na wanaoshindwa, huwezi kuona tofauti kubwa kwa nje. Wengi wanaonekana kufanya yale wanayopaswa kufanya, lakini inapokuja kwenye matokeo, tofauti inakuwa ni kubwa.
Je kuna bahati ambayo wachache sana ndiyo wanaipata huku wengi wakiikosa? Ndiyo, bahati huwa ipo, lakini sasa, huwa inakuwa umesambazwa kwa wote. Yaani bahati ambayo mtu anaipata kwenye safari ya mafanikio, ni bahati ambayo ilikuwa wazi kwa wote. Kwamba hata mwingine angeweza kuipata, lakini anayeipata ni anayekuwa eneo hilo la bahati kwa wakati huo wa bahati.
Kwa magumu na ushindani mkali uliopo kwenye mambo tunayofanya, tunahitaji mkakati utakaotuhakikishia chochote kinachopatikana tunanufaika nacho. Na hapo ndipo unapokuja mkakati wa kukataa kufa kirahisi kama njia ya kudumu kwa muda mrefu kwenye kile unachofanya na kupata matokeo makubwa.
Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia jinsi tunavyoweza kuwa wabishi sana kwenye kile tunachofanya, ili tuwe kwenye nafasi nzuri ya kunufaika na bahati zinazopatikana na kuleta mafanikio makubwa.

1. Jua Ambapo Ukienda Utakufa Na Usiende Hapo.
Charlie Munger alikuwa na kanuni yake rahisi sana ya namna bora ya mtu kupata chochote unachokuwa unataka. Kanuni hiyo ni kugeuza kile ambacho mtu unakuwa unataka, badala ya kujiuliza unapataje kitu, unajiuliza unakikosaje, ili ugeuze kukosa kuwe kupata.
Hii ni kanuni yenye nguvu, kwa sababu kila mtu tayari ana mambo yanayomzuia kupata anachotaka au yanayopoteza kile anachotaka. Hivyo kwa kujua yale yanayokuzuia au kukurudisha nyuma, unaweza kuyaepuka na ukapata unachotaka.
Kwa chochote unachofanya, unapaswa kujua ni vitu gani ukifanya utakuwa umejiondoa kabisa kwenye kitu hicho, kisha epuka kufanya vitu hivyo. Hiyo ndiyo dhana nzima ya kujua ambapo ukienda utakufa na kuepuka kwenda hapo.
Kila kitu kina mambo ambayo yanapaswa kuepukwa sana ili mtu uweze kudumu kwenye kitu hicho kwa muda mrefu. Na sababu kubwa ya wetu wengi kushindwa imekuwa ni kujikuta wamekwama na hawawezi kuendelea na kitu kwa muda mrefu zaidi.
Ukiweza kuepuka yale ambayo yanakutoa kwenye mchezo mapema, na ukaweza kuucheza mchezo kwa muda mrefu zaidi, ni lazima utapata ushindi unaotaka. Wewe pambania kitu kimoja tu, kuhakikisha hakuna kitu chochote ambacho kinakutoa kwenye mchezo ambao upo.
Bahati inahusika sana kwenye mafanikio makubwa, lakini bahati inawakuta wale ambao wapo kwenye uwanja wa mapambano, wale ambao hawajafa na kuondoka mapema.
Ni uwanja gani wa mapambano ambao umeuchagua wewe? Umejipangaje kuhakikisha kwamba hakuna kinachokuondoa mapema kwenye uwanja huo? Hilo ndiyo jambo kubwa kwako wewe kupambania ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
2. Kuwa Unayetisha Ili Kifo Kisikusogelee.
Maisha huwa yanataka mikwara sana, kama mtu unataka upate unachotaka. Ukikaa kinyonge, kila kitu kinakuonea, kila kitu kinakukwamisha. Ila ukiwa anayetisha, unaondoa vikwazo vingi ambavyo vinakosa uthubutu wa kuja kwako.
Ukiwa mtu ambaye unapigika kirahisi, kila kitu kitataka kukupiga. Ikiwa mtu ambaye kila kinachojaribu kukupiga kinakutana na wakati mgumu, unaogopeka. Hiyo ni kanuni ya asili, kinyonge kinaonewa, chenye nguvu kinaogopwa.
Hivyo hakikisha unajenga nguvu ambazo zitawatisha wale wote wanaotaka kukuangusha au kukukwamisha. Wafanye watu waogope kupambana na wewe moja kwa moja, kwa kuona hilo litakuwa hatari kubwa kwao.
Hata kama kweli huna nguvu hizo, wewe fanya kila kinachowezekana kuwafanya watu waamini una hizo nguvu. Fanya maigizo na maonyesho yoyote utakayoweza ili watu waone wazi kwamba una nguvu kubwa na hupaswi kuchukuliwa kirahisi.
Na hili wala halihitaji wewe uwadanganye watu, linataka wewe ujue unachotaka na kukiendea kwa msimamo bila kukwamishwa na chochote. Na ukiwa umejizuia usiweze kuondolewa kwenye mchezo, utaweza kufanya kwa muda mrefu zaidi na hilo litawatisha wengi wasijaribu kukukwamisha.
Kwa kujulikana kama mtu ambaye lazima utapata kile unachotaka na hakuna kitakachokukwamisha, vikwazo vidogo vidogo vinaondoka vyenyewe. Maana watu wanajifunza haina haja ya kukuzuia, kwa sababu utapata tu unachotaka. Hivyo hata ambao wangekuwa kikwazo, wanakupa ushirikiano ili usiwasumbue.
Kuna namna unaweza kujiweka na watu wakakuheshimu na kukupa unachotaka na kuna namna ukijiweka watu wanakudharau na kukukwamisha. Wewe unajua namna ipi ni sahihi kwako, jiweke hivyo.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK106; Kataa Kufa Kirahisi Kama Unataka Mafanikio Makubwa