Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kwa nje, mafanikio yanaweza kuonekana ni kitu rahisi tu. Ukisoma au kusikiliza hadithi nyingi za mafanikio, zinaonyesha mtu alianzia chini, akaweka juhudi na kupata mafanikio makubwa. Hadithi hizo huwa zinatoa hamasa kubwa, kwa kuwafanya watu wayatamani mafanikio ambayo wengi wanayo.
Licha ya hadithi za mafaniko kuwa nyingi, licha ya vitabu na mafunzo kutolewa. Pamoja na shuhuda na mahojiano ambayo watu wengi waliofanikiwa wamekuwa wanayatoa, bado wanaofanikiwa wameendelea kubaki wachache.
Wengi sana wanaotamani kufanikiwa wamekuwa hawafanikiwi. Ni kitu ambacho kimekuwa kinawashangaza wengi, mimi pia nikiwepo. Lakini baada ya kufuatilia kwa undani, nimeweza kujionea dhahiri kwa nini inakuwa hivyo.
Watu wengi sana wanatamani mafanikio wanayoyaona kwa nje, ila hawapo tayari kuvumilia mateso yanayowafikisha watu kwenye mafanikio hayo. Yaani ni kama wanasema wanataka wapewe mafanikio ambayo wengine wanayo, lakini wasipitie mateso ambayo hao waliofanikiwa wameyapitia.
Hicho ni kitu kisichowezekana kabisa, na ndipo ambapo wengi wamekwama.

Hujayataka Mafanikio Kweli.
Kwenye kitabu cha All You Can Do Is All You Can Do, kilichoandikwa na Art Williams, ameshirikisha hadithi moja yenye funzo kubwa sana kuhusu mafanikio na mateso. Anamwelezea Gary Player aliyeshinda mashindano mengi ya kimataifa ya mchezo wa golf.
Mara kwa mara watu walikuwa wanamwendea Gary na kumwambia; “Ningetoa chochote nilichonacho kama ningeweza kupiga mpira wa gofu kama wewe.”
Siku moja, Gary akiwa amechoka na kuvurugwa, alisikia mtu akimwambia; “Ningetoa chochote nilichonacho kama ningeweza kupiga mpira wa gofu kama wewe.”
Safari hii hakuweza tena kunyamaza wala kujibu kwa upole. Badala yake alisema ukweli ambao unadhihirisha kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa. Alijibu;
“Hapana, usingefanya hivyo. Unachosema ni kwamba ungependa kupiga mpira wa gofu kama mimi kama jambo hilo lingekuwa rahisi. Je, unajua unapaswa kufanya nini ili uweze kupiga mpira wa gofu kama mimi?
Unapaswa kuamka saa kumi na moja alfajiri, uende uwanjani, na upige mipira elfu moja ya gofu. Mkono wako unaanza kuvuja damu, unaenda kuosha damu mkononi, unafunga bandeji, kisha unarudi tena uwanjani na kupiga mipira mingine elfu moja. Hicho ndicho kinachohitajika ili kupiga mpira wa gofu kama mimi.”
Rafiki, hivi unapata msisimko kama ninaoupata mimi wakati unasoma hilo jibu? Kwa sababu hiyo ndiyo sababu pekee kwa nini wachache sana wanafanikiwa huku wengi wakitamani kufanikiwa ila wanashindwa.
Nani asiyejua kwamba mchezaji anapaswa kucheza, mwandishi anapaswa kuandika na muuzaji anapaswa kuuza? Kila mtu anajua. Lakini je, nani yuko tayari kuteseka kwa kufanya hayo mpaka apate mafanikio makubwa anayoyataka? Hapo ndipo tofauti inapoanzia na ndipo tunapaswa kufanyia kazi kama tunataka kujabadili maisha yetu.
Kwenye barua hii tunaangalia mambo ya msingi sana kufanyia kazi ili tuweze kuyakubali mateso yaliyopo kwenye safari ya mafanikio na kufanikiwa kwa uhakika.
Soma barua hiyo hapa; #BZK059; Usionee Wivu Mafanikio, Onea Wivu Na Mateso Pia.