Rafiki yangu Mpendwa,
Maisha yana mitego sana. Pamoja na kuonyesha kwamba tunataka kupata mafanikio makubwa, bado sisi wenyewe tumekuwa tunajihujumu kwenye kuyapata hayo mafanikio.
Sisi kama binadamu, huwa tunataka kupendwa na kukubalika na watu wengine. Na ili watu hao watupende na kutukubali, tunaona inabidi tufanye vile ambavyo hao wengine wanataka.
Lakini sasa, kufanya yale ambayo wengine wanatutaka tufanye, inakua kinyume kabisa na mafanikio tunayoyataka. Mafanikio yanataka tufanye vitu vya tofauti, ambavyo havijazoeleka na watu wengine.
Tunapofanya vitu hivyo vya tofauti, watu wanatupinga, wanatuona tunakosea au tuna kiburi na mengine ya aina hiyo.
Hiyo ndiyo njia panda ambayo wengi wamekuwa wanajikuta na inakuwa kikwazo kwao kufanikiwa.
Unajua kabisa tabia ulizonazo hazitakupa mafanikio unayoyataka, lakini unapoamua kubadili tabia hizo, watu wako wa karibu wanaona unajitenga nao. Mfano kuacha starehe ambazo umekuwa unashirikiana na watu wa karibu.
Unajua kabisa kufanikiwa kifedha unahitaji kwenye kila kipato uweke akiba na uwekeze. Lakini una watu wengi wa karibu ambao wanakutegemea kifedha, na huwezi kuwaridhisha wote. Lakini unajikuta huwezi akiba wala kuwekeza, ili uwasaidie wengi kadiri ya unavyoweza.
Ili tufanikiwe ni lazima tufanye mambo ambayo hayatawafurahisha wengi wanaotuzunguka. Sasa tutafanyaje wakati tunataka pia watu hao watupende na kutukubali?
Kwenye hii #BaruaYaKocha nimekushirikisha mwongozo rahisi kwako kufanya maamuzi kwenye huo mtego wa kutaka kupendwa na watu na kupata mafanikio makubwa.

1. Ukitafuta Kupendwa, Unaishia Kudharauliwa.
Ni mara ngapi umefanya vitu ambavyo wengine wanataka ufanye, ukiamini kwa kufanya hivyo watakukubali na kukupenda, lakini matokeo yake yanakuwa ni kudharauliwa?
Unaweza ukawalaumu watu kwenye hilo, lakini ndivyo asili yetu binadamu ilivyo. Huwa hatuthamini kitu chochote ambacho ni rahisi. Ndiyo maana hata vitu ambavyo watu wanavipata kirahisi, huwa wanaishia kuvipoteza. Mtu akiokota fedha ataitumia tofauti na ile aliyopata baada ya kufanya kazi kwa jasho.
Unawajua watu ambao wamekuwa wanafanya kila ambacho wengine wanawataka wafanye. Wamekuwa hawaleti ubishi wala ‘ukorofi’ kwa chochote wanachoambiwa au kupingwa. Wanakubaliana na kila mtu, ni watu wa amani.
Niambie watu hao huwa wanaitwaje. Majina yote ya ajabu, ‘bwege’, ‘fala’, ‘zombi’ na mengine. Siyo kwa sababu watu hao wana tatizo lolote, bali kwa sababu binadamu hatuna uwezo wa kuthamini vitu ambavyo vinakuwa rahisi.
Na sisi binadamu tuna haki kabisa ya kudharau chochote kinachokuwa rahisi, kwa sababu pia hakiwezi kuhimili kwa muda mrefu. Fikiria mtu kaja kwako na wazo fulani kubwa tu, ukamwambia hilo wazo haliwezekani, achana nalo kabisa. Na yeye akasema sawa, naachana nalo. Akaja na wazo jingine tena, ukamwambia ni baya na haliwezekani, akakubali. Utamzingatia kwa kiasi gani mtu wa aina hiyo? Unaweza kumwamini kwenye jambo lako, kwamba ataweza kulipambania?
Kuwa makini sana na kufanya mambo ili kuwafurahisha wengine, unajiharibia wewe mwenyewe, unatengeneza kudharauliwa. Ni bora kusimamia kitu fulani, ambapo kuna watu hawatafurahishwa, lakini watakuheshimu kwa kile unachosimamia.
2. Heshima Inadumu Kuliko Upendo.
Unapotaka makubwa, lazima ufanye makubwa. Na unapofanya makubwa, wanaokuzunguka hawatakuacha salama. Watakuonyesha jinsi ilivyo vigumu na hatari kwa hicho unachofanya. Watakupa mifano ya wengi ambao nao walitaka makubwa kama wewe.
Ukikubaliana nao na kuacha, wataachana na wewe na kuendelea na mambo yao mengine. Ukiwakatalia na ukaendelea, watazidisha ukali wao kwenye kukukatisha tamaa. Watakupa mpaka vitisho mbalimbali, lengo ni wewe uache hicho kikubwa unachofanya.
Ikiwa utaendelea licha ya yote hayo, watakuchukia. Watakuchukia kwa sababu hawaelewi inakuwaje uwe na uthubutu wa kufanya vile unavyotaka wewe licha ya kukatazwa na wengine. Watakuchukia siyo kwa sababu yako, bali kwa sababu wao walitamani wangeweza kufanya kama wewe, ila hawawezi.
Uzuri sasa, mwisho wa chuki huwa unakuwa ni heshima kubwa. Kwa sababu, licha ya wao kukuchukia wazi wazi, wewe unakuwa umeendelea kufanya. Na kwa kuendelea kufanya unayapata matokeo makubwa uliyokuwa unayataka. Na kwa matokeo hayo, wanakuheshimu. Wanaona ulikuwa sahihi. Na wengine wanasema walijua utapata matokeo hayo.
Wengine wataenda mbali na kusema walikusaidia kuyapata matokeo hayo. Hayo wala yasikuumize, wewe ulichokuwa unataka ni matokeo, na umeshayapata au utaenda kuyapata. Utakachopata cha ziada ni heshima ambayo watu watakuwa nayo kwako kwa kupata matokeo hayo.
Na heshima inatosha kabisa. Kwa sababu heshima inadumu kwa muda mrefu kuliko hata upendo. Tumeona njia ya upendo inaishia kwenye dharau. Lakini njia ya chuki inaishia kwenye heshima.
Kitu kizuri ni kwamba heshima inakuwa ni matokeo na siyo lengo la wewe kufanya. Wewe umefanya kwa sababu ya hatua unazotaka kupiga. Kwa kufanya kwako na kupata matokeo, watu wanakuheshimu. Ni kama umepata bonasi hivi, ambayo lazima uifurahie.
Tatizo la kutaka kupendwa inakuwa ndiyo lengo. Unajikuta hufanyi kitu kwa sababu ya matokeo ya kitu hicho, bali unafanya kwa sababu unataka kupendwa. Matokeo yake ni unadharauliwa na hupati matokeo.
Sasa si bora tu ufanye unachotaka, ambapo watu hawatakupenda, lakini utapata matokeo na kama bonasi, watakuheshimu kwa matokeo hayo?
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK095; Wakikuheshimu Inatosha, Kupendwa Jipende Mwenyewe.