Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kuna wakati ukijiangalia jinsi unavyoweka juhudi kubwa ila unapata matokeo madogo, halafu ukawaangalia wengine ambao hawaweki juhudi kubwa kama wewe ila wanapata matokeo makubwa, unaona kuna namna wao wana bahati ila wewe huna.

Rafiki, nataka kukuhakikishia kabia ya kwamba hisia zako ziko sahihi. Ni kweli kabisa wengine unaowaona wanapata matokeo makubwa kuliko wewe, wamekutana na bahati fulani fulani, ambazo wewe hujakutana nazo.

Angalau sasa umejisikia vizuri, si ndiyo? Vizuri, sasa nikupe ukweli ambao utaharibu hiyo kujisikia vizuri ambayo umekuwa nayo. Ukweli huo mchungu, lakini muhimu kwako kujua ni kwamba hata wewe, kama ungetaka, ungepata bahati kama wao.

Ndiyo, namaanisha kwamba hata wewe ungeweza kupata bahati na ukapata matokeo makubwa kama ya wengine. Tatizo lako ni hujachukua hatua sahihi ambazo zinaweza kukupa bahati hiyo unayohitaji ili ufanikiwe.

Na mimi nikiwa rafiki yako, ambaye mafanikio yako ni wajibu wangu, sina budi kukupa njia ya kuhakikisha unapata bahati nzuri na inayokupa mafanikio makubwa.

Na habari njema ni kwamba, ipo kanuni ya bahati. Ndiyo, ni kanuni ambayo ikifanyiwa kazi, matokeo yanapatikana kwa uhakika. Kama zilivyo kanuni za hisabati, kanuni ya bahati ni ya uhakika kabisa.

Kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukupa kanuni hiyo na jinsi ya kuifanyia kazi ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

1. Kanuni Ya Bahati.

Bahati siyo kitu cha kubahatisha kama wengi wanavyofikiria. Bali ni kitu kinachoweza kutengenezwa, kupangiliwa na kufanywa kitokee. Ili kupata bahati, ni muhimu sana mtu kujua kanuni inayoleta bahati. Kanuni hiyo ipo, na ipo wazi kwa yeyote anayetaka kuitumia.

Kanuni ya bahari ni kama ifuatavyo;

BAHATI = FANYA X TANGAZA

Ikiwa na maana kwamba bahati inatokana na kufanya na kutangaza kile unachofanya.

Kwa kanuni hiyo, ambayo inahusisha kuzidisha na siyo kujumlisha, unapoongeza kimoja, matokeo yanakuwa makubwa. Na unapoongeza vyote viwili, matokeo yanakuwa makubwa zaidi.

Na hilo linaeleza vizuri kwa nini baadhi ya watu wanaonekana kuwa na bahati sana kwenye maisha kuliko wengine. Kila unapowaangalia hao wanaoonekana kuwa na bahati sana, wanafanya kwa ukubwa vitu hivyo viwili. Wanafanya kwa ukubwa, au vitu ambavyo ni muhimu na wanahakikisha watu wengi zaidi wanajua kuhusu kile wanachofanya.

Watu wengi ambao wangeweza kupata mafanikio makubwa wamekuwa wanajikwamisha wao wenyewe kwa kufanya kwa udogo au kufanya vitu visivyokuwa muhimu na kushindwa kutangaza kwa kiasi kikubwa.

Hapo ndipo wewe unakwenda kubadili kabisa maisha yako na matokeo ambayo umekuwa unapata. Kwa sababu unaenda kufanya unachofanya kwa ukubwa na ubora na utapiga kelele sana ili kila mtu ajue na kuvutiwa kufanya kazi na wewe.

Kuanzia leo wewe ni mtu mwenye bahati zaidi haoa duniani, kwa sababu unaenda kufanya zaidi na kutangaza zaidi.

2. Fanya Kwa Ukubwa Sana.

Bahati inaanzia kwenye kile unachofanya na kwa kiwango unachofanya. Tunajua kabisa kwamba matokeo huwa hayaji tu, bali huwa yanasababishwa. Na yanasababishwa na ufanyaji wa vitu fulani.

Bahati yako inaanzia kwenye kuchagua kufanya vitu ambavyo vina thamani na manufaa kwa watu wengine. Angalia yale ambayo watu wengine wanahangaika nayo, kisha fanya kile ambacho kitawasaidia kwenye mambo hayo wanayokwama.

Kadiri unavyochagua kufanya kitu kinachowasumbua watu wengi, ndivyo unavyokuwa kwenye nafasi ya kupata bahati kubwa zaidi. Iwe ni kazi au biashara, hakikisha unatoa suluhisho ambalo watu wanalihitaji sana ili maisha yao yawe vile wanavyotaka.

Ukishachagua kilicho muhimu kufanya, unapaswa kukifanya kwa viwango vikubwa sana ndiyo uweze kupata matokeo makubwa. Hakuna kitu utakachofanya na ukawa wewe mwenyewe ndiye unayefanya, kuna wengi nao watakuwa wameona fursa unayoiona wewe.

Ili uwe na bahati kuliko hao wengine wanaofanya unachofanya, lazima ufanye kwa viwango ambavyo wao hawapo tayari kufanya. Unapaswa kufanya kwa ukubwa sana na kwa ubora ambao watu hawajazoea kuona. Ni kwa kutoa kitu ambacho hakijazoeleka ndiyo unaongeza nafasi yako ya kupata bahati.

Kwa vyovyote vile, hakikisha unachofanya kuna namna ni wewe tu unayeweza kufanya hivyo. Hata kama kila mtu anafanya, hakikisha kuna kitu ambacho watu wanakipata kwako na hawawezi kukipata kwa wengine. Hivyo ndivyo unavyotengeneza bahati kubwa, ya kuwafanya watu waje na wabaki kwako licha ya kuwa na mbadala wa hicho unachofanya.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK112; Tumia Kanuni Hii Kutengeneza Bahati Kubwa Kwenye Maisha Yako