Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Nitaendelea kukukumbusha kama unasahau, kwamba kazi yangu ni wewe. Mafanikio yako, yaani kupata kila unachotaka kwenye maisha yako, ndiyo wajibu ambao nimejipa.
Ndiyo maana unaona kwenye kila #BaruaYaKocha ninayokuandikia, inalenga wewe kupata zaidi ya unavyopata sasa, kwenda zaidi ya hapo ulipo sasa.
Hilo siyo tu kwamba linawezekana, bali ndiyo namna pekee ya kuishi maisha yako hapa duniani. Hata wewe mwenyewe tu ukiangalia, maisha yanakuwa na maana gani kama hutapata kile unachotaka? Tena ambacho kipo ndani ya uwezo wako kabisa kupata?
Hapo ndiyo mimi nimechagua kununua ugomvi na wewe, kuhakikisha huridhiki na unachopata sasa, ambacho najua, na wewe unajua ni tofauti kabisa na kile ulichokuwa unataka.
Na kama hutakimbia, kama utaendelea kusoma barua hizi, licha ya kuwa kali kwako, utapata msukumo wa kufanya tofauti na unavyofanya sasa, na hapo utapata matokeo ya tofauti na unayopata.
Ndiyo maana kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukuonyesha upande mwingine wa kukuwezesha wewe kupata kila unachotaka kwenye maisha yako.

1. Lakini Je, Inawezekana Kila Mtu Kupata Kila Anachotaka?
Umewahi kusikia zile kauli zinazosema siyo kila mtu anaweza kufanikiwa? Kauli hizo huwa zinawekwa kama vile mafanikio yana uhaba, hivyo wakishapata baadhi, yanakuwa yameisha na hakuna mengine tena.
Ni kawaida yetu binadamu kufikiria hivyo, kwa sababu tunakosa maono makubwa ya kuona jinsi kulivyo na utele wa kila kitu. Dunia haijawahi kuwa na uhaba wa kitu chochote kile. Uhaba wowote unaouona ni wa kutengenezwa, kwa watu kufikiri kuna uhaba.
Uzuri ni kwamba, tumekuwa tunajionea sisi wenyewe, jinsi ambavyo dunia inabadilika na kuwa bora kila siku. Teknolojia mpya zinagunduliwa kila siku na kufanya maisha yetu binadamu kuwa bora. Na wakati huo pia wavumbuzi wa teknolojia hizo wakipata mafanikio makubwa.
Steve Job amewahi kusema; “Kila kitu kinachokuzunguka unachokiita maisha, kimetengenezwa na watu ambao hawakuwa na akili sana kuliko wewe, unaweza kuvibadili, kuvishawishi na unaweza kujenga vitu vyako na wengine wakatumia.”
Kama mafanikio yote unayoona wengine wameyapata, siyo kwamba wana akili sana kukuzidi wewe. Hivyo hata wewe unaweza kuyapata, tena makubwa kuliko wao.
Unachohitaji ni kujua njia ya kuyapata, ili uitumie kupata mafanikio hayo.
2. Njia Pekee Ya Kupata Kila Unachotaka.
Ukorofi ndiyo njia pekee ya kupata kila unachotaka kwenye maisha yako. Sasa kabla hujatoka hapa na kwenda kuanza kuwasumbua watu ili upate unachotaka, sikiliza, ni ukorofi kwako mwenyewe.
Kwa kifupi, kama unataka kupata chochote unachotaka, lazima uwe mkorofi sana kwako wewe mwenyewe. Lazima uwe mkali kwako, usijionee huruma kwa namna yoyote ile. Kwa sababu maisha yako yanakosa maana kama hupati kile unachotaka.
Mimi naweza kuwa na uhakika kuhusu jambo moja kwako, hujapata kila unachotaka kwa sababu unajionea huruma sana. Na wakati mwingine wanaokuzunguka ndiyo wanakuhadaa ujionee huruma.
Unawajua watu waliofanikiwa kuhusu wewe, na unajua wanafanya mambo kwa ukubwa na ukali kuliko wewe. Wewe unajionea huruma na kujifariji kwamba maisha yako yana furaha kuliko ya waliofanikiwa na wanaoonekana kujitesa.
Wakati wengine wanatafuta vitu rahisi vya kufanya, wewe nenda kwenye vitu vigumu. Wakati wanatafuta njia ya mkato, wewe tafuta njia iliyo ndefu zaidi.
Wengi wanapokutana na maumivu na kuacha, wewe endelea licha ya maumivu hayo. Hakuna matokeo makubwa yanayokuja kirahisi, lazima uwe mkali, lazima uwe mkorofi, lazima utake hasa.
Kinachofanya wengi wasipate wanachotaka ni kutokuwepo kwa madhara ya kutokupata wanachotaka. Kila kitu ambacho kina madhara usipokipata, huwa unahakikisha unakipata.
Iwapo utajiweka kwenye nafasi ya kuwa na madhara makubwa kama hutapata unachotaka, utajisukuma na kukipata. Hivyo ndivyo saikolojia ya binadamu inavyofanya kazi.
Kutaka tu kitu hakutoshi kukufanya ukipate, lazima utake kitu hicho kuliko kingine chochote, lazima ukitake kuliko unavyoyataka maisha yenyewe.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK113; Hii Ndiyo Njia Pekee Ya Kupata Kila Unachotaka Kwenye Maisha Yako