Rafiki yangu Mpendwa,
Kila mtu sasa analalamikia kitu kimoja, mambo mengi na muda mchache.
Kila mtu ana mambo mengi ya kufanya, lakini muda wa kuyafanya mambo hayo umekuwa mchache.
Yaani muda wa siku umebaki kuwa ule ule, lakini mambo ya kufanya kwenye siku yanaendelea kuongezeka.
Hata teknolojia mpya zinazokuja, ambazo zinaahidi kurahisisha majukumu yetu, zimeishia kuwa zinachukua muda wetu mwingi.
Kwa kifupi sasa hivi kila mtu yuko ‘bize’ kuliko ilivyowahi kudhaniwa. Hapo sasa tungefikiri watu wangekuwa wanapata matokeo makubwa kadiri ya wanavyotaka.
Lakini hilo ni tatizo jingine, licha ya watu kuwa bize sana, matokeo nayo yamekuwa nadra kupatikana. Watu wanafanya sana, lakini wanachopata ni kidogo mno ukilinganisha na walichokuwa wanataka kupata.
Hili limewafikisha watu wengi kwenye hatua ya kukata tamaa, na kuona labda matokeo makubwa na mafanikio siyo kwa ajili yao. Kwa sababu kila wakikazana kufanya, ndivyo wanavyozidi kukosa matokeo wanayoyataka.
Kitu kimoja ambacho umekuwa hujui ni kwamba, huo ‘ubize’ ambao unadhani ndiyo utakaokupa matokeo, ndiyo huo huo unaokuzuia kupata matokeo.
Ndiyo, namaanisha kwamba kinachokuzuia wewe kufanikiwa ni kuwa ‘bize’. Ina maana ukiacha kuwa bize, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata matokeo unayoyataka.
Sasa hilo halimaanishi kwamba usifanye chochote, bali uwe na mkakati sahihi kwenye mambo yote unayofanya.
Hilo ndiyo tutajadili hapa kwenye #BaruaYaKocha, ili uweze kutoka na mwongozo wa kutumia vizuri rasilimali muda uliyonayo kufanya makubwa.

1. Kila Unapojipa Muda Mwingi, Unapoteza.
Uzuri wa safari ya mafanikio ni tayari unajua nini unapaswa kufanya ili upate mafanikio unayoyataka. Ila tatizo linakuja kwenye kuanza kufanya kile unachopaswa kufanya.
Umekuwa unajipa muda mrefu sana kwenye kufanya mambo ambayo unajua unapaswa kuyafanya. Kuanza tu inakuchukua muda, unasubiri mpaka uwe tayari kwa kila kitu, jambo ambalo limekuwa halitokei.
Na hata ukifikia kuanza, unajipa muda mrefu sana wa kufanya kitu, kiasi kwamba unapoteza muda mwingi bila ya kuwa na tija.
Kama kweli unapata matokeo, kwa mambo yote muhimu ambayo unajua unapaswa kuyafanya, yafanye mara moja. Yaani pale unapojua kitu unachopaswa kufanya, hapo hapo fanya maamuzi na anza kufanya mapema iwezekanavyo.
Najua unaweza usielewe hili, kwa kuona itakuwa ni kukurupuka, kwamba umepata tu wazo na unafanya. Wacha nikupe jaribio moja la kufanya ili ujionee mwenyewe.
Kwa siku kadhaa, kila unapojikuta kwenye hali ya kufanya maamuzi juu ya kitu fulani, fanya maamuzi hayo hapo hapo. Hesabu mpaka tano na andika maamuzi ambayo umekuja nayo. Ndiyo, sekunde tano tu za kufanya maamuzi ndiyo unajipa. Kisha andika maamuzi hayo.
Baada ya hapo, jipe muda wowote unaotaka wa kufanya uchunguzi wa kina juu ya jambo hilo. Fanya maandalizi yoyote unayotaka. Kisha fanya maamuzi baada ya uchunguzi na maandalizi yako.
Sasa rudi ulinganishe maamuzi uliyofanya kwa sekunde tano na uliyofanya kwa kujipa muda mwingi kadiri ulivyotaka. Nakuhakikishia, tofauti itakuwa ni ndogo sana. Kumbe basi muda wote ambao umekuwa unajipa wa kujiandaa ndiyo ufanye maamuzi umekuwa unaupoteza.
Maamuzi tayari unakuwa nayo ndani ya sekunde 5 tu, au unakuwa huna kabisa. Hata ujipe muda mrefu kiasi gani, ni nadra sana maamuzi uliyochukua miezi kufikia yakawa tofauti na uliyoyapata ndani ya dakika 5.
Umeona hapo sasa kwa nini umekuwa hupati matokeo licha ya kuwa ‘bize’ sana. Kwa sababu unajipa ubize kwa mambo yasiyo na tija kabisa. Kama muda huo mwingi unaoupoteza kwenye maamuzi ambayo yalihitaji dakika tano tu.
2. Vipi Kama Maamuzi Ya Haraka Yatakuwa Na Makosa?
Najua umezoea sana kuwa bize kiasi kwamba huamini maamuzi ambayo umekuwa unachukua miezi kuyafanya ungeweza kuyafanya kwa sekunde 5 tu. Inaeleweka, huwezi kukubali hilo kirahisi.
Hivyo utakuja na utetezi kwamba japo ni kweli unaweza kufanya maamuzi ndani ya muda mfupi, vipi kama hayatakuwa sahihi? Hivyo unachukulia muda wote ambao umekuwa unapoteza kwenye kujiandaa na maamuzi kama kinga ya kutokukosea.
Sasa hapa nakukamata pande zote mbili;
Upande wa kwanza, ni mara ngapi umechukua muda mrefu kufanya maamuzi, na bado yakawa maamuzi ya kukosea. Mara ngapi umechunguza kweli biashara ya kufanya, na bado unapokuja kuifanya ikashindwa? Wewe hushangai watu wanapanga ndoa, wanakusanya michango ya watu, sherehe kubwa inafanyika na bado hawavuki mwaka wanaachana? Kujipa muda mrefu wa kufanya maamuzi siyo kinga ya kutokukosea.
Upande wa pili, ukifanya maamuzi kwa haraka na ukawa umekosea, si ni vizuri zaidi? Kwa sababu utaona makosa haraka na utafanya maamuzi mengine kwa haraka ili kurekebisha makosa hayo yaliyojitokeza. Yaani kilicholeta tatizo, kinakuwa pia ndiyo kinachotatua tatizo.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK094; Unakuwaje ‘Bize’ Na Matokeo Hayaonekani?