Rafiki yangu Mpendwa,
Ni bahati mbaya sana tumekuwa tunatumia muda wetu mwingi kujiandaa kuishi kuliko kuyaishi maisha yenyewe. Na hilo limesababishwa na mazoea ambayo tumekuwa nayo tangu utotoni.
Tukiwa wadogo kabisa tulikuwa tunajiandaa kuanza shule. Tukiwa shuleni tukawa tunajiandaa kwenda ngazi za juu za elimu. Tukiwa ngazi za juu tukawa tunajiandaa kupata kazi au kuingia kwenye biashara.
Baada ya kuanza kazi au biashara tukaanza kujiandaa kuanza maisha. Na tangu hapo maisha yenyewe yamekuwa nadra kuyaishi, kwa sababu kila wakati kuna kitu tunajiandaa nacho. Kujiandaa kuanza familia, kujiandaa kusomesha watoto, kujiandaa kujenga mali na uwekezaji.
Mwisho tunafika hatua ya kujiandaa kustaafu, tukidhani ndiyo maisha yataenda kuanza. Hata kwa wale wanaofikia kustaafu, wanajikuta wakijiandaa kufa.
Ni jambo la kusikitisha sana kwamba tumepewa maisha yaliyokamilika, lakini tunachangua kuyapoteza kwenye maandalizi yasiyokamilika.
Ninachosema ni imetosha sasa, huhitaji tena kufanya maandalizi yoyote, huhitaji kusubiri siku yoyote ya kimiujiza ndiyo uanze kuishi maisha unayotaka. Upo huru sasa hivi kuanza kuyaishi maisha yoyote unayoyataka.
Kwenye hii #BaruaYaKocha, nimejiamulia kukupa wewe rafiki yangu ruhusa ya kuyaishi maisha yako. Na kwa sababu watu wengi wanaokuzunguka hawajawahi kuthubutu kuanza kuyaishi maisha yako, wakiona wewe umethubutu watakuuliza nani kakuruhusu. Na wewe usiwe na hiyana, wajibu nimeruhusiwa na Kocha wangu. Na wakitaka kujua zaidi kuhusu hilo, waambie wajiunge na #BaruaZaKocha na kuanza kwa kusoma barua hii.

Karibu sasa tuangalie kwa nini uko huru kuyaishi maisha yako kwa namna unavyotaka wewe.
1. Siku Moja Unayoisema Ndiyo Sasa.
Siku moja nitakuwa mtu wa maana ….
Siku moja nitakuwa tajiri mkubwa ….
Siku moja nitakuwa na biashara kubwa ….
Siku moja nitakuwa na nidhamu kali ya mafanikio …
Hivyo ndivyo umekuwa unajiambia, na kujikuta unabaki kwenye hali ya kujiandaa kuishi badala ya kuanza kuishi kikamilifu.
Unavyoisema hiyo siku moja, ni kama vile unamaanisha;
Siku moja utakuwa na mikono mitatu ….
Siku moja utakuwa na macho ya mbele na nyuma ….
Siku moja utaweza kuruka angani kama ndege ….
Sijui unaona ninachotaka uone hapo?
Unajua kabisa, vile ulivyo sasa ndivyo utakavyokuwa kesho na siku nyingi zijazo.
Hakuna kikubwa kitakachobadilika kwako kwa sababu umesubiri kibadilike.
Kitu pekee cha kubadilisha, na ambacho kitabadili kabisa maisha yako ni fikra ulizonazo.
Kwa bahati nzuri sana, fikra zozote unazokuwa nazo ndizo zinazokuwa uhalisia wako.
Unapojiambia siku moja utakuwa hivi au vile, akili yako inakuwa na msimamo kwamba bado hujawa tayari kupata unachotaka.
Kwa kubadilisha tu na kusema kile unachotaka ndicho ulichonacho sasa, akili yako inabadilika na kukuletea fursa za kutimiza hicho unachojiona unacho sasa.
2. Unaweza Kujiamulia Kufanya Vitu.
Kitu kimoja ambacho nimekuwa sielewi kuhusu wewe rafiki yangu ni jinsi unavyojichelewesha kupata unachotaka.
Unajua kabisa ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako. Unayo picha kamili ya kile unachotaka na mpango wa kuifikia picha hiyo.
Ila sasa, cha kushangaza, unasubiri. Hutaki kuanza kufanya kile ambacho kitakupa matokeo unayoyataka. Unajiambia bado hujawa tayari, unajiambia kuna mambo unayasubiri.
Mambo gani hasa? Nini ambacho unadhani kitakuwa tayari zaidi ya kilivyo sasa?
Ukitaka kusubiri mpaka kila kitu kiwe kama unavyotaka ndiyo uanze, kamwe hutakuja kuanza. Kwa sababu kila wakati kuna kitu ambacho kitakuwa hakipo sawa.
Ndiyo maana unatakiwa kujiamulia tu kuanza kufanya vitu. Hata kama hujui huko mbele mambo yataendaje, wewe anza kufanya. Hatua moja itafungua hatua nyingine na haitakuchukua muda utaanza kuona matokeo uliyokuwa unayataka.
Kuanza kufanya hakukuhakikishii kupata unachotaka, lakini kutokuanza kunakuhakikishia kwamba hutapata unachotaka. Kipi bora kwako, uanze na uwe kwenye nafasi ya kuweza kupata, au usianze na usiwe na nafasi ya kupata kabisa?
Jiamulie kufanya vitu, fanya na utaona jinsi ya kuendelea kufanya mpaka upate matokeo unayoyataka.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK092; Hiyo Siku Moja Ndiyo Sasa