Rafiki yangu Mpendwa,

Huenda umepambana sana kufanikiwa, lakini kila unachojaribu kufanya, unaishia kupata matokeo ambayo ni tofauti kabisa na matarajio.

Ukaona labda unayofikiria wewe hayana tija, ukaiga kile ambacho wengine wanafanya na wanapata matokeo, lakini bado wewe ukakosa matokeo kama ya hao wengine.

Unapofika hatua kama hiyo, ni rahisi kuamini maneno mengi ambayo umekuwa unaambiwa kuhusu wewe kushindwa kufanikiwa.

Umekuwa unaambiwa kwa sababu hukupata ufaulu mkubwa shuleni basi huwezi kufanikiwa. Ukaambiwa kwa sababu ya ulipotokea, mafanikio hayatawezekana kwako.

Mwanzo ulikuwa na nguvu ya kupuuza yote hayo na kufanya, ukiamini utawaonyesha kwamba unaweza licha ya yote waliyokutabiria.

Lakini baada ya kupigwa mieleka kadhaa na kuanguka, unaanza kuona kama yale uliyokuwa unaambiwa yalikuwa sahihi na wewe tu ndiye ulikuwa na kiburi.

Kabla hujakubaliana na wale waliokukatisha tamaa, nimekuandilia #BaruaYaKocha inayokuonyesha kitu kimoja tu, ambacho kipo ndani ya uwezo wako kukifanya na kikakupa mafanikio yoyote makubwa unayoyataka.

1. Huhitaji Akili Kubwa Kufanikiwa.

Albert Einstein aligundua moja ya kanuni ya kipekee kabisa kwenye fizikia, ambayo imeleta mapinduzi makubwa sana duniani. Jambo la kushangaza zaidi ni aligundua kanuni hiyo kwa nadharia tu. Wakati kanuni nyingi za kifizikia na kisayansi zimekuwa zikigunduliwa kwa kufanya majaribio, huyu mwamba alifikiria tu na kuja na hiyo kanuni.

Kwa vipimo vyovyote vile, Einstein alikuwa na akili sana. Wakitajwa watu wenye akili sana kuwahi kuwepo hapa duniani, jina lake lipo juu kabisa. Kwa uwezo wake huo unadhani alikuwa anawaambiaje watu kuhusu akili yake? Unadhani kwa usahihi kabisa kwamba angeweza kuwaambia watu yeye ana akili sana na wakakubaliana naye.

Lakini sivyo Einstein alivyojichukulia. Alipoulizwa kuhusu akili yake, alinukuliwa akisema; “Siyo kwamba nina akili sana, ni kwamba tu huwa nakaa na tatizo kwa muda mrefu zaidi.”

Rafiki, hebu tafakari kwa kina hiyo nukuu na uone jinsi ambavyo akili na matokeo ni vitu vya kutengenezwa kabisa. Siyo kwamba kuna watu wamezaliwa na uwezo wa kupata matokeo na wengine hawana.

Kinachowatofautisha wanaopata matokeo na wanaoyakosa ni muda wa kukaa na tatizo. Wakati wanaopata mafanikio wanakaa na tatizo moja kwa muda mrefu, wanaoshindwa wanajaribu tatizo kwa muda mfupi, wasipopata matangazo wanaenda kwenye tatizo jingine.

2. Turudi Kwako Kuhesabu Sasa.

Kuna kitu ambacho unapambana nacho sasa lakini hupati matokeo. Umejaribu kila namna lakini mambo hayaendi kama ulivyotarajia. Umefikiria sana, na kuwaangalia wengine ambao wanapata matokeo na kushawishika hicho siyo kitu chako.

Kabla hujaamini hivyo, hebu turudi na kuhesabu ni muda mrefu kiasi gani umekaa na hicho kitu. Kuwa tu mkweli kwako wewe mwenyewe, umefanya kitu hicho kwa muda gani sasa?

Halafu waangalie wale ambao unaona wanapata matokeo makubwa kuliko wewe. Angalia ni kwa muda gani wamekuwa wanafanya kitu hicho?

Sikuambii ujiangalie wewe na kuwaangalia wengine kwa lengo la kujilinganisha na kujipa faraja au kukata tamaa. Bali nataka uone jinsi kanuni ya Einstein inavyofanya kazi.

Kitu chochote ambacho hakikupi matokeo unakuwa hujakaa nacho kwa muda mrefu wa kutosha. Na wale ambao wanafanya kitu cha aina hiyo hiyo na kupata mayokeo makubwa, wamekaa nacho kwa muda mrefu.

Hata kama mlianza kufanya kwa pamoja, utagundua wewe kuna namna umekuwa na usumbufu unaopunguza muda wako kwenye kitu hicho. Wakati wenzako wameweka umakini wao wote kwenye kitu hicho.

Haiwezi kushangaza pale unapokosa matokeo na wengine wakayapata. Hakuna muujiza wowote. Jibu ni moja tu, anayekaa na tatizo kwa muda mrefu zaidi ndiye anayeweza kulitatua na kupata mafanikio makubwa.

Imetosha sasa wewe kuhangaika na matatizo mengi, chagua tatizo lako moja, ambalo unaona ukilitatua utaleta matokeo makubwa na ya tofauti. Komaaa na tatizo hilo mpaka ulitatue na utakuwa umejijengea mafanikio makubwa na ya kudumu.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK091; Huhitaji Akili Kubwa Sana Kufanikiwa Kama Utaweza Kufanya Kitu Hiki Kimoja