Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Mafanikio ni rahisi kuyasema na kuyapanga, lakini ni magumu mno kuyapata. Hiyo ndiyo sababu pamoja na wengi kutaka mafanikio, wachache sana ndiyo wanaoyapata.
Na siyo kwamba wachache hao wanaoyapata mafanikio wana bahati sana au wana upekee ambao wengine hawana. Watu wote wanapitia mambo yale yale kwenye safari ya mafanikio.
Hakuna safari ya mafanikio ambayo haikutani na magumu na changamoto. Watu wote wanaianza safari ya mafanikio kwa malengo na mipango mizuri. Lakini wanapoanza utekelezaji, ndiyo wanakutana na uhalisia, ambao hawakuwa wanaujua.
Kila anayeianza safari ya mafanikio, anafika hatua ambayo anaona hawezi na wala hakuna sababu ya kuendelea tena na safari hiyo. Kila mtu anapokutana na magumu na changamoto, anajua kabisa kwamba lazima avuke hayo ndiyo afanikiwe. Na hilo linafundishwa sana, lazima mtu upambane, ung’ang’ane ndiyo ufanikiwe.
Lakini kuna hii pointi ambayo huwa haizungumziwi sana. Pointi ambayo mtu anafikia na kuwa na ushahidi wa kutosha kwamba hana tena sababu ya kuendelea. Pointi ambayo mtu anaona amefanya kila kilichokuwa ndani ya uwezo wake na hakuna namna anaweza kuendelea tena.
Hii ndiyo pointi ambayo wengi hukata tamaa na kuacha kufanya. Na hiyo ndiyo pointi inayowatofautisha wale wanaopata mafanikio makubwa na wanaobaki kawaida. Siyo kwamba wanaofanikiwa huwa hawafikii pointi hiyo ya kukata tamaa.
Kila anayekuwa kwenye safari ya mafanikio anafikia hiyo pointi, lakini wanaofanikiwa wanaendelea japo kidogo tu. Na huko kuendelea kidogo tu ndiko kunakoleta mafanikio makubwa sana. Ni pointi moja ndogo ndiyo inayowatofuatisha wanaofanikiwa sana na wanaoshindwa.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza jinsi na wewe unavyoweza kuendelea japo kidogo tu pale unapofika kwenye hatua ya kukata tamaa. Utatoka hapa na mkakati wa kukuwezesha kuvuka nyakati ngumu sana za maisha yako na kuendelea kufanya, kitu kitakachokupa matokeo unayoyataka.

1. Ni Sawa, Lakini Siyo Leo
Tumese umefanya kila kilicho ndani ya uwezo wako kufanya, lakini hujapata matokeo. Umeambiwa ng’ang’ana na wewe umeng’ang’ana kweli kweli, lakini hakuna kinachosogea. Umefika hatua ambayo unaona kabisa huwezi kuendelea tena. Huna tena unachoweza kufanya ili kuendelea na safari yako ya mafanikio. Una kila sababu ya kukata tamaa na kuacha.
Jiambie ni sawa kabisa, kubali kwamba unapaswa kuacha, lakini jiambie siyo leo. Ndiyo, jiambie utakata tamaa, ila siyo siku ya leo. Jipe siku moja tu ya kuendelea kufanya, jipe siku moja ya kuendelea kuning’inia hapo bila kuachilia. Siku moja tu ya kuendelea kama ambavyo umeweza kuendelea kwa muda wote mpaka kufika hapo.
Halafu siku moja itapita, utaingia kwenye siku nyingine. Unajiambia tena kuacha kutakuja, lakini siyo siku hiyo. Unapambana kuivuka hiyo siku, ukiwa bado umesimama na siyo kuanguka.
Unajua nini kinakuja kutokea? Utajikuta umeenda kwa siku nyingi na umeendelea kufanya bila kuacha. Na kizuri zaidi, utajikuta umeshavuka ugumu uliokuwa unakutana nao na kupata matokeo ya tofauti. Hivyo ndivyo watu wote wanaofanikiwa sana wanaenda, siyo kwa bahati, bali kwa kuendelea bila kuacha.
Mara nyingi kinachokukatisha tamaa ni kuangalia muda mrefu ujao wa kuendelea na ugumu na kuona huwezi. Lakini unapoacha kuangalia huo muda mrefu na kuiangalia siku moja tu, mambo yanabadilika. Siku moja tu ya kuteseka, hakuna anayeishindwa hiyo. Kwa hiyo mapambano yako yanakuwa ni ya siku moja tu, kupambana kuendelea kwa siku moja. Ukizikusanya siku moja moja nyingi, unakuwa na maisha kamili ya mafanikio.
2. Ingekuwa Rahisi Kila Mtu Angefanya
Angalia jinsi ambavyo watu wengi wanaanza kitu, lakini wanaomaliza kwa kufanikiwa ni wachache sana. Na hao wachache ndiyo wanaopata matokeo makubwa. Wengi wanaoishia njiani hawapati matokeo kabisa.
Kila unapofika wakati ambapo unaona huwezi kuendelea tena, jikumbushe wachache ambao huwa wanapata matokeo. Na utagundua hatua uliyofikia ndiyo inayowatenganisha wachache wanaofanikiwa na wengi wanaoshindwa.
Ni lazima ukubali kwamba kila mtu anafikia hatua hiyo unayofikia wewe, na wachache wanaovuka wakiwa imara ndiyo wanaopata zawadi yote iliyopo. Sasa hapo ni wewe kuchangua, kama umetoka mbali kote uje uishie hapo, au kama utaendelea na ukaipate zawadi hiyo.
Unapokutana na ugumu ambao unaona ndiyo mwisho wa safari yako, jiulize kama ulidhani itakuwa rahisi kwa kila mtu. Ulijua kabisa haitakuwa rahisi. Sasa huo ndiyo ugumu uliojua utakutana nao, ugumu ambao wengi hawapo tayari kuuvumilia. Je unakubali kuwa kwenye hilo kundi la wengi? Ambao pia hawatafanikiwa?
Kitu chochote ambacho kila mtu anaweza kukifanya huwa hakina thamani. Unapokutana na ugumu, jua huo ni mchujo wa kuwaondoa wengi. Usikubali kukaa kwenye huo upande wa wengi na kuchujwa. Wewe upo kwa ajili ya ushindi, hakuna chochote kitakachokukwamisha kuupata huo ushindi.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK090; Tumia Sababu Hizi Kuendelea Hata Pale Unapokuwa Na Kila Sababu Za Kukata Tamaa