Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Naamini umekuwa unahudhuria misiba mbalimbali. Kwenye kila historia ya marehemu, huwa wanaeleza sababu au chanzo cha kifo. Hata kama hakitaelezwa kwa undani sana, lakini lazima watu wataambiwa maisha ya mtu huyo yalifikaje ukingoni.

Kwenye taaluma ya utabibu, sisi madaktari tunapaswa kuandika cheti cha kuthibitisha mtu kufa. Na kwenye cheti hicho, tunapaswa kuandika sababu au chanzo cha kifo.

Kwa kuhudhuria kwako misiba, nina imani hujawahi kusikia KAZI NGUMU ikitajwa kama sababu ya kifo. Katika vyanzo vya kifo vinavyotambulika kitabibu, kazi ngumu siyo moja ya vyanzo hivyo.

Kwenye historia za marehemu tunasikia vyanzo vingi, kama ajali, magonjwa, umri na kadhalika. Lakini kazi ngumu, au kufanya kazi kwa juhudi sana, hutakuja kusikia hilo.

Kitu cha kushangaza ni inapokuja kwenye maisha yetu ya kila siku, watu wamekuwa wanachukulia kazi ngumu kama adhabu, kama kitu ambacho kinaweza kuathiri maisha yao.

Watu wanakwepa sana kazi ngumu, wakiona itawaathiri kiafya. Lakini ni watu hao hao utawakuta wanachukua hatari kwenye maeneo mengine ya maisha yao bila hata kujali.

Ukimwambia mtu unafanya kazi masaa mengi kwa siku, atakuambia siyo nzuri kiafya. Lakini utakuta mtu huyo huyo akitumia vilevi, akiendesha kwa mwendo wa kasi na kujiweka kwenye mazingira ambayo yanahatarisha sana afya yake.

Tunachoweza kuona hapo ni watu hawapendi tu kazi ngumu na kuamua kuipa sura mbaya ya hatari kiafya. Lakini mengi ambayo yana hatari kweli kiafya, watu wanayafanya bila hata kujiuliza.

Kwenye barua hii tunaenda kujadili mambo mbalimbali ambayo yatatuonyesha umuhimu wa kazi ngumu na kwa nini siyo hatari kama wengi wanavyochukulia.

1. Kwa Nini Kazi Ngumu Haiwezi Kukuua.

Rafiki, sababu rahisi na inayoeleweka sana ya kwa nini kazi ngumu haijawahi kutajwa kwenye sababu za kifo nimeipata kwenye kitabu cha ALL YOU CAN DO IS ALL YOU CAN DO, kilichoandikwa na Art Williams. Art alianza maisha kama kocha wa mpira, baadaye akaja kuwa mfanyabiashara kwenye mafanikio makubwa sana.

Kwa maisha yake yote, alikuwa akiamini sana kwenye kuweka kazi kwa juhudi kubwa. Falsafa yake kubwa ilikuwa ni FANYA TU (JUST DO IT) na ilimpa matokeo makubwa. Kwenye kitabu kuna mfano ameutoa kuhusu kuweka kazi kwa juhudi na kwa nini hakuwezi kumuua mtu. Anaandika;

“Nilikuwa nawaambia wachezaji wangu wa mpira wa miguu kwamba haiwezekani kufa kwa sababu ya kufanya kazi kwa bidii. Wakati wa likizo, tulikuwa na kambi ya mazoezi, na tulifanya mazoezi mara tatu kwa siku. Niliwaambia:

“Vijana, mtatoka nje kwenye jua kali, mtafanya kazi, kocha atawakaripia, na mtahisi kama mnakaribia kufa. Lakini mtakapohisi hivyo, endeleeni kufanya kazi. Kwa sababu Mungu ameweka mfumo fulani kichwani mwenu ambao utawafanya mzimie kabla hamjafa. Na kama mtazimia, tutawapeleka kwenye chumba cha mapumziko, tutawaogesha, tutawapa vidonge vya chumvi, na mtakuwa tayari kwa mazoezi yanayofuata.

Rafiki, sijui kama huwa unasisimka kama mimi pale unaposikia baadhi ya kauli zinazokuonyesha kwamba umekuwa sahihi kwa mengi unayofanya na kuamini. Hayo maelezo ambayo Art alikuwa anawapa vijana wake, ndiyo ukweli kuhusu safari ya mafanikio.

Ameeleza kwa nini kazi ngumu haiwezi kukuua, kwa sababu akili zetu zina mfumo wa kuzima kabla hujafa, na kuzima kwenyewe ni kuzimia. Kuzimia ni njia ya akili kukuambia kwamba mwili umechoka, upumzishe. Kama ambavyo ukitumia sana kifaa cha kielektroniki kinaganda, mfano kompyuta, simu au tv, ndivyo na mwili pia unavyokuwa.

Sasa nikuulize swali, kama simu yako imeganda kwa sababu ya kuitumia sana, ndiyo unaacha kabisa kuitumia? Jibu ni hapana, unaipumzisha, kisha baadaye unaiwasha na kuendelea kuitumia.

Hicho ndicho Art aliwaeleza vijana wake, kwamba hata kama watazimia, siyo mwisho. Watapewa huduma, watapumzika na wataendelea na mazoezi. Sasa hebu niambie ni kwa namna gani mtu anayefanya hivyo anaweza kushindwa?

2. Ukweli Ni Kwamba Hatufanyi Kazi Kwa Juhudi Kama Tunavyodhani.

Hili sikusemi wewe rafiki, bali tunajisema wote. Ukilinganisha na maana halisi ya kufanya kazi kwa juhudi kubwa, sisi ni kama hatufanyi kazi kabisa. Kama unabisha, nikuulize swali moja; Ni lini mara ya mwisho umezimia kwa kufanya kazi sana?

Mimi binafsi sijawahi kuzimia kwa kufanya kazi. Na naamini hicho ni kiashiria kwamba bado sijaweka kazi kwa juhudi kubwa kiasi cha kujihurumia. Licha ya kuona naweka kazi sana na nachoka, ni kujifariji tu. Kuchoka halisi ni pale akili inapouzima mwili kabisa.

T. S. Eliot ana nukuu inayosema; “Ni wale tu watakaothubutu kwenda mbali zaidi, ndiyo watakaojua ni mbali kiasi gani wanaweza kwenda.” Kwa kipimo hicho, tunaweza kweli kusema tunajua ni juhudi kiasi gani tunaweza kuweka? Wakati hata hatujawahi kuzimia?

Ambacho inabidi tukubaliane hapa ni kama hujawahi kuzimia kwa sababu ya kufanya kazi kwa juhudi sana, bado hujajua ni juhudi kiasi gani unaweza kuweka kwenye kazi.

Hivyo tuache kulalamika tunafanya kazi sana, maana bado hata hatujajua juhudi kiasi gani za kazi zinahitajika. Kwa kifupi, tumekuwa tunajihurumi sana inapokuja kwenye kazi. Tumekuwa laini na wavivu. Mwili ukituambia tumechoka, tunausikiliza na kufanya. Tunajidanganya kwa maneno yetu wenyewe.

Ukweli kwamba tumechoka na hatuwezi kuendelea tena ni pale tunapozimia. Kama hatujazimia, bado hatujaweka juhudi zote tunazoweza kuweka. Hivyo kama hatupati matokeo, siyo kwa sababu imeshindikana, bali kwa sababu hatujafanya kiasi cha kutosha.

Kwenye #BaruaYaKocha kuna mambo mengine matatu muhimu sana unayopaswa kujua na kuzingatia kwenye kufanya kazi kwa juhudi ili kujenga mafanikio makubwa.

Isome barua hiyo hapa; #BZK060; Sababu Ya Kifo Ambayo Hutawahi Kuisikia; KAZI NGUMU.