Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Mafanikio huwa ni rahisi kuyapanga, kila kitu kinaonekana kwenda vizuri kama kinavyokuwa kimepangwa. Ni mpaka inapofika kwenye utekelezaji ndiyo uhalisia unakuwa tofauti kabisa na matarajio. Mambo yanakuwa tofauti kabisa na yalivyopangwa.
Safari ya mafanikio ya wengi huwa inaishia hapo kwenye uhalisia kuwa tofauti na matarajio. Na wanakuwa na sababu za msingi kabisa, ambazo zinaeleweka, za kwa nini wameshindwa kuendelea. Mambo yanakuwa magumu kuliko uwezo wao wa kuyakabili na kupata matokeo wanayokuwa wanayataka.
Inaweza kueleweka, na wakati mwingine kutia huruma kwa namna wengi wanavyokuwa wamekwamishwa na mambo wanayosema yapo nje ya uwezo wao. Sababu zinazokuwa zimewakwamisha zinakuwa ni kikwazo cha kweli na siyo kwamba wanadanganya.
Ila kuna tatizo moja, wapo watu wengine wengi wanaokuwa wamefanikiwa, licha a kukutana na hali hizo zilizowakwamisha wengi. Pamoja na ugumu wa yanayokwamisha, bado kuna watu wameweza kuyavuka na kujenga mafanikio makubwa, tofauti na matarajio ya walio wengi. Ni uwepo wa watu hao ndiyo unaotupa msukumo wa kuendelea kuyapambania mafanikio, bila ya kujali nini tunakutana nacho.

Hakuna Anayejali, Wewe Shinda Tu.
Bill Parcells akiwa kocha mkuu wa timu ya New York Giants alijikuta kwenye wakati mgumu. Kwani alikuwa na wachezaji wengi ambao walikuwa majeruhi, ambao ndiyo walikuwa tegemeo kwenye ushindi. Alifikiria jinsi kupata ushindi ilikuwa vigumu akiwa na wachezaji tegemeo, vipi wakati ambapo hao tegemeo hawapo?
Kwenye mazungumzo na Al Davis, ambaye alikuwa menta na rafiki yake, alimwambia; “Al, sina uhakika tunawezaje kushinda bila kuwa na wachezaji wetu bora. Nifanye nini?”
Al Davis akamjibu; “Bill, hakuna anayejali, wewe fundisha timu yako.”
Rafiki, hilo ni jibu fupi sana, lakini lililobeba suluhisho la mambo yote unayoona yanakukwamisha kupata mafanikio unayoyataka. Hakuna anayejali, wewe tekeleza wajibu wako.
Biashara ina ushindani mkali? Hakuna anayejali, wewe fanya biashara yako kwa mkakati sahihi.
Unataka kujenga utajiri na uhuru wa kifedha lakini unakoanzia ni pagumu? Hakuna anayejali, wewe ongeza kipato, dhibiti matumizi, weka akiba na wekeza.
Unatamani sana kufanikiwa lakini kila unapochukua hatua mpya unajikuta unarudi kwenye mazoea? Hakuna anayejali, wewe jijengee tabia na nidhamu sahihi ya mafanikio.
Rafiki, jibu hilo la hakuna anayejali, wewe fanya wajibu wako ni jibu bora kabisa kwako kulitumia kila unapojipa sababu za kushindwa. Kwa sababu, hata sababu ziwe nzuri kiasi gani, hakuna anayejali. Watu wanaangalia kama umeshinda au umeshindwa.
Kuliko kutumia muda na nguvu nyingi kuelezea sababu za wewe kukwama au kushindwa, ni bora kupeleka rasilimali hizo kwenye mambo yatakayokupa ushindi. Kwa sababu hakuna anayejali kuhusu sababu na visingizio unavyotoa.
Kwa lolote unalopanga, uhalisia utakuwa tofauti. Unapokutana na huo uhalisia usiutumie kama kikwazo, bali angalia nini unachoweza kufanya kuendelea na safari yako. Kwa sababu hiyo ndiyo muhimu zaidi.
Rafiki, tumeanza na sababu ya kushinda, kwamba hakuna anayejali kuhusu kitu kingine chochote. Lakini je vipi kuhusu huo ushindi wenyewe, ni nini hasa? Na upi mchakato sahihi kwetu kubapa ushindi huo? Hayo ndiyo tunayokwenda kuyaangalia kwenye barua hii.
Karibu ujifunze mambo ya msingi kuzingatia kwenye safari yako ya ushindi ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Soma barua hiyo hapa; #BZK061; Wewe Shinda Tu Mwanangu (Just Win Baby)