Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kuna vitu umekuwa unajiambia unavitaka, umekuwa unaviwekea malengo kila mara na kuvizungumzia kwa kila mtu. Umekuwa chanya sana juu ya vitu hivyo, ukivijengea taswira kamili kwenye fikra zako na kujiona tayari ukiwa navyo.
Lakini leo nataka nikupe habari ambazo zinaweza zisikufurahishe, ila hakuna namna, ni lazima uzisikie, na uzisikie kutoka kwa mimi rafiki yako, ninayekutakia mema kwenye mafanikio.
Tuwe tu wakweli rafiki, hutaki hicho unachosema kila mara kwamba unakitaka. Sikuambii hivi kukukatisha tamaa, au kutaka kukupa msukumo wa kutaka zaidi. Bali nakuambia kwa sababu ndiyo uhalisia wenyewe. Mdomoni unasema unataka hicho unachosema, lakini inapokuja kwenye matendo, ni tofauti kabisa na hicho unachosema unataka.
Unaweza kujitetea, kwa kutoa sababu na visingizio vinavyokukwamisha kuchukua hatua kwenye hicho unachosema unataka. Na kwa sababu na visingizio hivyo, unathibitisha kwamba hutaki hicho unachosema unataka.
Tuangalie mfano huu rahisi kabisa, mtu mwenye nguvu amekuzamisha kwenye maji na unashindwa kupumua, unafanya nini? Je utakubali tu kuzama kwenye maji mpaka kufa? Hilo halitatokea, utapambana kwa kila namna mpaka uokoe uhai wako. Hakuna sababu wala kisingizio chochote kitakachopata nafasi, ni kupambana mpaka upate pumzi.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio, unapokuwa unataka kitu kweli, unachukua hatua zinazohitajika ili kukipata. Huruhusu sababu au visingizio vyovyote kuwa kikwazo kwako kupata hicho unachotaka.
Ndiyo maana sasa, leo itabidi uchague moja, kuamua kweli unataka hicho unachosema unataka au kukubali kwamba umekuwa unajidanganya ili ujisikie vizuri.
Kwenye barua hii unaenda kuona jinsi ambavyo kujidanganya ni jambo lililozoeleka kwenye jamii zetu kiasi cha kuchukuliwa ni kitu cha kawaida. Hapo utaona kwa nini na wewe umekuwa unajidanganya, kisha kuchagua kama utaendelea kujidanganya au utakuwa mkweli kwako.

1. Mashindano Ya Vipaji Siyo Kwa Ajili Ya Kusaka Vipaji.
Kumekuwa na mashindano mengi ya vipaji, iwe ni kwenye muziki, michezo, maigizo na maeneo mengine. Watu wengi wamekuwa wanalalamikia mashindano hayo kwa kushindwa kutoa vipaji vingi kama ambavyo ingetegemewa. Pia wamekuwa wanalalamikia majibu ya baadhi ya majaji kwa washiriki wa mashindano hayo, wakiona ni ya kuwakatisha tamaa.
Huko nyuma nilikuwa mmoja wa watu waliodhani mashindano hayo yana changamoto nyingi. Ni mpaka nilipojifunza kwamba mashindano ya vipaji hayapo kwa ajili ya kuibua vipaji, bali kwa ajili ya burudani ya gharama nafuu.
Yaani, mashindano ya vipaji ambayo yamekuwa yanaendeshwa, hayapo kwa ajili ya kuibua vipaji vipya. Bali yapo kwa ajili ya kutoa burudani kwa gharama ambayo siyo kubwa. Hivyo kila kinachoendelea pale ni sehemu ya hiyo burudani. Na ndiyo maana hakuna matokeo makubwa yanayopatikana kwenye mashindano hayo.
Na sababu kubwa ni moja, watu wenye vipaji kweli, hawasubiri mashindano ndiyo wajue wana vipaji. Badala yake tayari wanakuwa wanatumikia vipaji vyao. Hata wale wanaoshinda kwenye hayo mashindano, siyo ambao walijaribu vipaji vyao kwa hayo mashindano, bali ambao tayari walikuwa wanafanyia kazi vipaji vyao, ila hawakupata fursa nzuri ya kuvionyesha.
Ni vigumu sana kwa mtu ambaye tayari ana shughuli nyingine anazofanya kuwa na kipaji kwa sababu tu ameshiriki shindano la vipaji. Wenye vipaji hawasubiri mashindano kuvionyesha, badala yake wanavionyesha wakati wote. Vipaji vyao vinakuwa ndiyo shughuli yao kuu.
Kama watu wanajidanganya kwa ngazi kubwa kama hii ya kusaka vipaji, unaelewa kwa nini ni rahisi kujidanganya kwenye malengo na mipango ambayo watu wanajiwekea lakini hawachukui hatua. Kwa sababu kujidanganya imekuwa kitu kinachopokelewa na walio wengi.
Kama unasema unataka kufanya biashara lakini huanzi, unataka kuandika lakini huanzi, unakuwa huna tofauti na wanaoshiriki mashindano ya vipaji. Hawapo ‘siriazi’ kwamba wanaonyesha vipaji, bali wanashiriki tu kwenye burudani rahisi kwao kupata nafasi ya kushiriki.
2. Ushindi Wa Kamari Ni Matumaini Ya Kushinda.
Kamari na michezo yote ya bahati nasibu imepangiliwa kwa namna ambayo watu wachache sana watapata ushindi, huku wengine wengi wakipoteza fedha walizoweka. Watu wamekuwa wanapoteza fedha nyingi kwenye hiyo michezo, lakini bado hawaachi kushiriki michezo hiyo. Kila anayecheza michezo hiyo ya kamari na kubahatisha, hata kama amewahi kushinda, ukikusanya kiasi alichopoteza ni kikubwa zaidi.
Unaweza kujiuliza inakuwaje watu wazima, ambao wanajua kabisa kamari na bahati nasibu kuna nafasi kubwa ya kupoteza kuliko kupata na bado wanacheza? Na jibu linarudi pale pale kwenye kujidanganya. Kinachowavutia watu kwenye kamari na bahati nasibu ni kujidanganya na ushindi.
Mtu anapokuwa ameweka dau lake na kusubiria ushindi, anakuwa na matumaini kwamba anaweza kushinda. Anakuwa anafikiria vitu atakavyofanya na fedha nyingi za ushindi atakazopata. Hali hiyo inamfanya mtu kujisikia vizuri sana. Pale matokeo yanapotoka na akawa amekosa, matumaini hayo yanayeyuka. Ili kupata tena matumaini ya aina hiyo, inabidi acheze tena. Hivyo anarudia kucheza mchezo huo na kufungua upya matumaini ya kupata ushindi mkubwa.
Huku ni kujisikia vizuri kwa kujidanganya kwamba unaweza kupata ushindi na ushindi huo ukabadili kabisa maisha. Huku kujidanganya na kusikia vizuri kumepelekea wengi kuingia kwenye uraibu wa michezo hiyo ya kamari na kubahatisha.
Hivyo pia ndivyo malengo na mipango ya wengi ilivyo. Wengi wanafurahia kuweka malengo na mipango, wanajiona kabisa wakiwa wamepata mafanikio na maisha yao kuwa mazuri. Lakini wanapojaribu kuchukua hatua, wanagundua mambo kwenye uhalisia ni magumu na ya kukatisha tamaa. Hilo linawafanya warudi kwenye malengo na mipango, ili waendelee kujisikia vizuri.
Kama hutaacha kujidanganya kwa kutafuta kujisikia vizuri kwenye malengo na mipango badala ya kuchukua hatua, utakuwa mtu wa mipango na maneno mengi lakini usiyepata matokeo.
Soma #BaruaYaKocha upate mambo yote matano muhimu kwako kujua ili uache kujidanganya na kujikwamisha kufanikiwa.
Soma barua hiyo hapa; #BZK062; Acha Kujidanganya, Hutaki Hicho Unachosema Unataka.