Rafiki yangu Mpendwa,

Nikikuuliza kwa nini mpaka sasa hujapata mafanikio makubwa unayoyataka, utanipa sababu nyingi sana. Utanipa orodha ndefu ya kila ambacho kimekukwamisha kufanikiwa.

Utakuwa unaamini kabisa kwenye orodha uliyoitoa na kuamini kwamba vikwazo hivyo vikiondoka, basi mafanikio unayoyataka yanakuwa uhakika kwako.

Labda tukubaliane na wewe kwa muda juu ya hivyo ambavyo unaona vinakukwamisha. Lakini turudi kuangalia watu wengi ambao wameweza kupata mafanikio makubwa kuliko wewe. Ambao wengi walianzia kwenye hali ngumu kuliko zako, wakikwamishwa na mengi kuliko hata yanayokukwamisha wewe.

Unaelezeaje hali hiyo? Unaelezeaje watu wengine kuweza kupata matokeo makubwa kuliko ambayo unapata, licha ya wote kuwa na changamoto zinazofanana?

Ukiwa mkweli kwako, utaona kwamba kinachokukwamisha kupata matokeo unayotaka ni wewe mwenyewe. Ndiyo, sababu na vikwazo vipo, lakini kama kwa wengine wenye vikwazo hivyo wamepata matokeo, hapo tatizo linakuwa ni wewe.

Ingekuwa tatizo ni hivyo vikwazo, watu wote wenye navyo wasingepaswa kuwa wamefanikiwa. Lakini uwepo wa watu wenye vikwazo kama vyako na wamefanikiwa kuliko wewe, inaonyesha kwamba wewe ndiye unayejikwamisha.

Kama kichwa kinapata moto, kwa kushindwa kujua unajikwamishaje, ndiyo lengo la hii #BaruaYaKocha. Hapa unaenda kuona wazi jinsi ambavyo wewe mwenyewe umekuwa unajikwamisha kupata zaidi na hatua za kuchukua ili kukomesha hilo mara moja.

1. Taka Zaidi Ya Unachopata.

Sheria ya kwanza ya kupata zaidi ya ulichonacho sasa, ni kutaka zaidi ya hicho, kuuliza zaidi, kuomba zaidi. ‘Pangu pakavu, tia mchuzi.’

Kuendelea kupokea unachopata sasa, bila kutaka zaidi, kwa kuanzia ndani yako, ni kuiambia dunia kwamba umetosheka. Na dunia inafurahi kuona wewe umetosheka, inaenda kuhangaika na wale ambao wanataka zaidi. ‘Chuma kinachopiga kelele ndiyo kinawekewa kilainishi.’

Ni lini mara ya mwisho umetaka matokeo makubwa zaidi kutoka kwako wewe mwenyewe?  Na siyo tu kusema unataka matokeo makubwa, bali kufanya kweli kwa utofauti na ukubwa.

Ni lini mara ya mwisho umetaka kuwa na tabia bora kuliko ulizonazo sasa? Na siyo tu kujifunza tabia na ukasema ni nzuri. Bali kuchukua hatua za makusudi za kujenga tabia hizo mpya?

Ni lini mara ya mwisho umetaka kuongeza kipato chako, siyo kwa kusema, bali kwa kutoa thamani kubwa sana, ambapo dunia haina budi bali kukulipa zaidi?

Nadhani unaanza kupata picha kwa nini umekwama kwenye hayo matokeo unayopata sasa. Kwa sababu pamoja na kuyalalamikia, hakuna hatua kubwa na za makusudi, tena za kukuumiza wewe ambazo umechukua.

Dunia inaona uko sawa, inakuacha uendelea na mambo yako. Ukiumia kiasi cha kutosha kwa hapo ulipo sasa, utatoa kelele, na dunia itakusikiliza na kukupa unachotaka. Swali ni lini utainuka na kutoa hiyo kelele kwa ukubwa?

2. Unastahili Kupata Zaidi.

Tatizo jingine la wewe kutokupata zaidi ni kuona ni kama bahati kwako kupata hata hicho unachopata sasa. Huamini kwa mtu wa aina yako, na yote uliyopitia unastahili kupata unachopata. Kwa hiyo unaona bora uwe mtulivu, ili usije ukakosa hata hicho kidogo unachopata sasa.

Huo ni mtazamo wa kidumavu, ambao umekuwa unakuzuia wewe kupata makubwa ambayo yapo ndani ya uwezo wako na unastahili kuyapata. Chochote unachopata sasa, ni kwa sababu una thamani ya kukipata. Na unastahili kupata zaidi ya hapo, ni vile tu wewe umekuwa hujiamini.

Chochote unachofanya sasa na kinakuingizia kipato, kuna thamani unaitoa ndiyo maana unapata kipato hicho. Hupewi tu kama hisani, hakuna mwenye fedha za kupoteza kwa kuwapa watu ili wajisikie vizuri.

Kama watu wanakuwa tayari kukulipa wanachokulipa sasa, basi watakuwa tayari kukulipa zaidi ya hicho wanachokulipa sasa. Swali ni je wewe unataka kulipwa zaidi ya unavyolipwa sasa? Maana hicho tu ndiyo kinachokukwamisha.

Kwa kuanza na thamani ambayo unawapa watu na wanakulipa sasa, ukikazana kuwapa thamani kubwa zaidi ya hiyo, halafu ukawaambia unataka wakulipe zaidi, unadhani watakataa? Yaani kama kuna matatizo yao makubwa ambayo umeyatatua, halafu ukawataka wakulipe zaidi, wataacheje kwa mfano?

Huo ni mfano mmoja tu wa eneo la kipato. Kwenye kila eneo la maisha yako, unaweza na unastahili kupata zaidi ya unavyopata sasa. Tatizo ni wewe umechagua kuendea kila eneo kwa mazoea, kama hapo ndiyo mwisho.

Usikae kinyonge hata kidogo. Dunia haiheshimu chochote ambacho n kinyonge. Ni lazima upambanie kile unachotaka, kwa sababu unastahili kupata zaidi.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK097; Ni Wewe Mwenyewe Unayejikwamisha Kupata Zaidi Ya Unachopata Sasa.