Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Hii ndiyo hadithi ambayo nimeona ikijirudia kwenye safari ya mafanikio ya watu wengi.

Mtu anaanzia chini kabisa, hana mafanikio. Hilo linampa hasira na msukumo wa kubadili maisha hayo aliyonayo.

Msukumo huo unampelekea afanye mambo kwa namna ya tofauti kabisa na wanavyofanya wengine.

Kwa aliyeajiriwa anawahi kazini na kutimiza majukumu yake kwa viwango vikubwa. Anajituma sana kwenye kila anachofanya na kuzalisha matokeo mazuri.

Kwa aliyejiajiri au anayefanya biashara anajituma kweli kweli. Anawahi kwenye shughuli zake, anachelewa kutoka, anawahudumia vizuri sana wale anaowalenga. Muda wake mwingi unakuwa kwenye hizo shughuli zake, kitu kinacholeta matokeo makubwa kwake na kwa wale anaowahudumia.

Kutokana na msukumo huo ambao watu wanaanza nao, na matokeo wanayozalisha, wanaanza kupiga hatua kutoka kwenye hali duni waliyoanzia. Wanaanza kupata uhuru wa kuwa na vitu ambavyo huko nyuma hawakuweza kuwa navyo.

Watu wanaanza kuona maisha yamekuwa na ahueni na kuyafurahia. Na hapo ndipo hatari kubwa zaidi inapoibuka, hatari inayowapelekea kushindwa kukua zaidi na kuanza kuanguka.

Watu wengi wanapopata mafanikio kidogo, wanaridhika na kuona tayari wameshamaliza kazi kubwa waliyokuwa nayo. Wengi wanaona hawana tena haja ya kuendelea kujitesa kama awali, kwa sababu wameshatoka kwenye hali duni ambayo walikuwepo.

Hilo ndiyo kosa kubwa sana na ambalo limewaangusha wengi waliokuwa wameanza kuona mwanga. Kitendo cha kulegeza yale yaliyowapa mafanikio madogo, wanakuwa wamejizuia kabisa kupata mafanikio makubwa.

Kuna mambo mawili makubwa ninataka utoke nayo kwenye makala hii, ambayo ukiyafanyia kazi utaweza kujenga mafanikio makubwa endelevu.

Moja; Mambo Yanapokuwa Mazuri, Ongeza Zaidi Unachofanya.

Mambo yanapoanza kuwa mazuri, ndiyo wengu hushawishika kupunguza kasi. Badala ya kukanyaga mafuta ili kuongeza kasi, wanakanyaga breki ili kuipunguza.

Wengi wanafanya hivyo kwa sababu washawishika kulinda mafanikio kidogo waliyopata, kitu ambacho ni sumu kubwa.

Kuanzia sasa wewe kuwa mtu wa kuendelea kuongeza kasi kadiri unavyopata matokeo mazuri. Usilinde ushindi wowote unaoupata, bali tumia ushindi huo kutafuta ushindi mkubwa zaidi.

Kile kinachokupa matokeo mazuri, kifanye kwa ukubwa zaidi. Na kile kisichokupa matokeo mazuri, kiboreshe mpaka kikupe matokeo.

Wewe jua kwenye hii safari ya mafanikio, utaendelea kufanya, haijalishi umepata matokeo gani. Matokeo mazuri unazidisha kufanya na matokeo mabaya unaboresha unachofanya.

Mbili; Siku Unayoona Umemaliza, Ndiyo Siku Unayoanza Kuanguka.

Unapoanzia chini unakuwa huna chochote, hilo linakusukuma kupambana. Unapoanza kupata chochote kitu, unaanza kuona umemaliza kazi kubwa uliyokuwa nayo. Unaona kama matokeo unayopata unastahili kuendelea kuyapata, bila kusumbuka tena.

Hapo ndipo anguko la wengi linapoanzia. Unapoona tu kwamba huhitaji kujitesa tena, ndiyo unaanza kupoteza hata kile ambacho ulikuwa umeshapata.

Safari ya mafanikio ni sawa na kusukuma jiwe kubwa kupanda mlima, ukiacha tu, jiwe linarudi mpaka chini na kuhitajika kuanza tena upya.

Safari ya mafanikio ni kupanda mlima mmoja, halafu ukifika kwenye kilele, unaona milima mingine mingi unayopaswa kuipanda.

Kama utachagua safari yako iishie kwenye mlima mmoja, jua hutabaki kwenye hicho kilele, badala yake utaporomoka na kurudi ulikotoka.

Kwenye barua ya Kocha nimejadili kwa kina hali hii ya mafanikio kidogo kuwa kikwazo kwa mafanikio makubwa. Ni eneo muhimu sana kulielewa kwa kina na kulifanyia kazi ili ujenge mafanikio ya kudumu.

Isome barua hiyo hapa; #BZK005; Jinsi Ya Kubaki Na Njaa Kali Ya Mafanikio Hata Baada Ya Kupata Mafanikio.

Rafiki yangu mpendwa, umeona hii hadithi ikijirudia kwa watu wengi. Usidhani wewe ni wa kipekee sana kwamba haiwezi kutokea kwako.

Acha kufanya makosa ambayo wengi wamekuwa wanayafanya pale wanapopata mafanikio kidogo. Wewe endelea kubaki na njaa kali ya mafanikio, hata kama umeshatoka kwenye hali ya chini sana uliyoanza nayo.

Haijalishi umepata matokeo gani, endelea kufanya kwa njaa ile ile uliyoanza nayo. Hivyo ndivyo utakavyojenga mafanikio makubwa na endelevu.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.

Pata kitabu hiki leo kwa ofa ya Shilingi elfu 5 tu. Bonyeza maandishi haya kukipata.