Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Kama kuna maandiko ya dini yaliyotafsiriwa vibaya, basi ni yale yanayohusu fedha na utajiri. Yapo maandiko mengi, lakini hapa nitaweka mawili ambayo ndiyo maarufu zaidi.

Andiko la kwanza ambalo limetafsiriwa sana vibaya ni linalosema; ‘Fedha ndiyo chanzo cha maovu yote’.

Andiko la pili ambalo pia limetafsiriwa sana vibaya ni linalosema; ‘Ni rahisi kwa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia kwenye ufalme wa mbinguni’.

Hapa sitaingia kwenye mahubiri sana ya tafsiri sahihi na isiyo sahihi ni ipi, ila ninachotaka uelewe ni kwamba mtazamo mbaya ambao umeaminishwa kuhusu fedha siyo sahihi.

Na mtazamo mkubwa usio sahihi kuhusu fedha ambao umeaminishwa ni kwamba fedha haiwezi kununua furaha. Ni kama umewekwa njia panda, uchague kati ya fedha na furaha.

Lakini huo siyo ukweli kabisa, fedha inaweza kununua furaha. Na kadiri mtu unavyokuwa na fedha zaidi, ndivyo unavyoweza kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuwa na furaha.

Kama unabishana na hilo, nakuelewa kabisa, kwa sababu najua utakuwa kwenye moja kati ya makundi haya mawili.

Moja; Masikini uliyekata tamaa.

Ukiwa kwenye kundi la masikini aliyekata tamaa, unaona kitu pekee cha kujifariji nacho ni furaha. Unajiaminisha kwamba licha ya kukosa fedha, una furaha na wale waliokuzidi fedha hawana furaha.

Huo ni uongo ulioukumbatia, kwa sababu unakufanya ujisikie vizuri. Sasa iwe ni kweli kwamba waliokuzidi fedha hawana furaha, haiondoi umuhimu wa wewe kujijenga kifedha na kiutajiri.

Una wajibu wa kutoka kwenye umasikini na huhitaji kuhusisha wajibu huo na furaha.

Mbili; Tajiri wa kubahatisha.

Unaweza kuwa na fedha, lakini ukawa umezipata kwa njia ambayo unajua huwezi kuirudia tena na ukazipata. Labda umeshinda bahati nasibu, au umepata urithi au umewadhulumu watu.

Fedha unakuwa nazo, lakini huwezi kuzifurahia kwa sababu kila wakati una wasiwasi kama zikipotea huwezi kuzipata tena. Au una wasiwasi wale uliowadhulumu wanaweza kuchukua kilicho chao.

Katika hali hiyo, kuwa na fedha hakuwezi kukuletea furaha kabisa. Zaidi kunakuongezea hofu na wasiwasi mkubwa.

Jinsi ya kutumia fedha kununua furaha.

Umeona jinsi ambavyo hakuna uhusiano wa umasikini na furaha au utajiri na kutokuwa na furaha. Fedha ni fedha na furaha ni furaha, hivyo vitu havipaswi kuchanganywa kabisa.

Ili uweze kuwa na fedha na furaha kubwa kwenye maisha yako, kuna mambo muhimu sana ya kufanya. Matatu nitakushirikisha hapa, na mengine utaenda kujifunza kwenye #BaruaYaKocha nitakayokushirikisha.

1. Kuwa wewe.

Moja ya vitu vinavyosababisha watu wengi wasiwe na furaha kwenye maisha yao ni kuiga wengine na kufuata mkumbo. Wanafanya yale ambayo wengi wanafanya au wanayakubali.

Hata wanapopata matokeo, bado yanakuwa hayana maana kwao, kwa sababu haikuanzia ndani yao.

Chagua kuwa wewe, fanya yale yanayotoka ndani yako. Kwa njia hiyo utaridhika na maisha yako na kufurahia matokeo unayopata.

2. Toa thamani kwa wengine.

Kinachowafanya wengi wanaopata fedha wasizifurahie ni kwa sababu wanakuwa wamezichukua kwa wengine bila kuwapa thamani. Kama umedhulumu au kuchukua rushwa au kunufaika zaidi ya wengine, huwezi kufurahia ulichopata.

Ili kuondokana na hilo, hakikisha chanzo chako cha fedha ni kutoa thamani kwa wengine. Wajibu wako ni kuhakikisha unalipwa kwa kile unachotoa kwa wengine. Hilo litafanya ufurahie malipo unayopata, kwa sababu unajua kuna watu wamenufaika.

Epuka njia za mkato za kupata fedha, huwa zinakuja na gharama yake kwa upande wa furaha.

3. Anza na furaha.

Kama unafikiria ukipata fedha ndiyo utakuwa na furaha, tayari umeshapotea. Unatakiwa kuanza na furaha kwanza, ndiyo upate fedha.

Fedha huwa ina tabia ya kukuza kile ambacho tayari unacho. Kama huna furaha, ukipata fedha utaendelea kutokuwa na furaha. Na kama una furaha, ukiwa na fedha utakuwa na furaha zaidi.

Anza kwa kuyafurahia maisha yako kwanza, kabla hata hujapata fedha nyingi. Na utakapopata fedha nyingi, utazidisha hiyo furaha.

Kwenye #BaruaYaKocha, nimeeleza jinsi unavyoweza kutatua furaha na fedha. Hii siyo barua ya kukosa kusoma kama kweli unataka maisha bora na ya mafanikio.

Isome barua hiyo hapa; #BZK006; Je Ni Kweli Kwamba Mafanikio Na Utajiri Haviwezi Kununua Furaha?

Rafiki, kama ulivyoona, furaha na fedha siyo vitu ambavyo unatakiwa uchague kimoja. Bali ni vitu unavyoweza kwenda navyo pamoja. Fanyia kazi haya uliyojifunza ili uyabadili maisha yako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.


Pata kitabu hiki leo kwa ofa ya Shilingi elfu 5 tu. Bonyeza maandishi haya kukipata.