Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Unapochagua safari ya mafanikio, iwe ni kwenye maisha, fedha na hata biashara, ushindani utaibuka juu yako.
Kwanza kabisa watu wanaanza kukupinga, kwa kukuambia mafanikio makubwa unayoyataka hayawezekani. Na kwa sababu safari hiyo ya mafanikio inakutaka ufanye mambo makubwa na ya tofauti, wanakuona kama umepotea.
Wengi huwa wanaishia hatua hiyo ya mwanzo kabisa, kwa kupingwa na watu wa karibu wanaona hakuna sababu ya kuendelea na safari yao ya mafanikio makubwa.
Ukifanikiwa kuvuka hicho kikwazo cha kwanza na ukafanyia kazi mkakati wako, siyo kwamba mambo yanakuwa rahisi. Badala yake ugumu unaongezeka.
Unapofanya kile ulichopanga kufanya na ukapata matokeo mazuri, unakaribisha ushindani. Kwa kuwa ulichofanya kimeleta matokeo, watu wanaanza kukuiga ili wapate matokeo mazuri kama unayopata wewe.

Hilo litakuumiza, ukizingatia ulivyopitia magumu na sasa watu wanataka kujinufaisha kirahisi tu. Unashawishika kushindana na wale wanaokuja kwenye hilo eneo lako, ili wasichukue fursa yako.
Lakini hilo ni kosa kubwa sana unaloweza kufanya. Kushindana moja kwa moja na wale wanaofanya unachofanya ni njia ya uhakika ya kushindwa.
Hiyo ni kwa sababu unakuwa umeuacha mchezo wako na kuingia kwenye mchezo wao.
Njia pekee ya kuwashinda wale wanaoshindana na wewe ni kutokushindana nao moja kwa moja. Lakini hilo halimaanishi kwamba utawaachia tu wachukue fursa yako.
Badala yake kuna mambo utayafanya, ambayo yatawafanya kushindana na wewe iwe kitu kigumu sana kwao. Hayo ndiyo mambo unayokwenda kujifunza kwa kifupi kwenye makala hii. Halafu kwa kina zaidi unaenda kuyapata kwenye #BaruaYaKocha.
Jinsi ya kuwashinda watu bila kushindana nao moja kwa moja.
1. Cheza Uwanja Wa Nyumbani.
Kwenye michezo, unajua kwamba, timu inayocheza uwanja wa nyumbani inakuwa kwenye nafasi kubwa ya kushinda kuliko inayocheza kwenye uwanja wa ugenini.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye ushindani. Uwanja wa nyumbani ni yale maeneo ambayo wewe una uimara kuliko wengine. Uwanja wa ugenini ni maeneo ambayo wengine wako imara kuliko wewe.
Ili uweze kushinda ushindani bila kushindana moja kwa moja, mara zote cheza uwanja wa nyumbani. Fanya yale ambayo wewe una ubora kuliko wengine wote. Fanya ambayo watu hawawezi kukuiga na wakafanya kwa ubora kama wewe.
Kwa kucheza uwanja wa nyumbani, unawaweka kwenye nafasi ngumu kwao kushinda, japokuwa hushindani nao moja kwa moja.
2. Wafanye Wajutie Kuingia Kwenye Mchezo Wako.
Huwezi kuwazuia watu kufanya kile unachofanya, tupo kwenye soko huria, hivyo soko ndiyo linapaswa kuamua.
Ila unaweza kuwafanya wajutie kuingia kwenye mchezo wako. Na utafanya hivyo kwa kuhakikisha huachi nafasi yoyote kwa ushindani kupata nafasi ya kuingia. Maana yake unatawala kabisa kile unachofanya kiasi kwamba hakuna kasoro ambayo wengine wanaweza kuitumia kama fursa.
Kuwa kila mahali kiasi kwamba wakijaribu kuingia, wanaona ngoma ni ngumu kwao. Kwa njia hiyo unaondokana na ushindani bila hata kushindana moja kwa moja.
Na njia ya kukamilisha hilo ni kufanya kwa viwango vya juu sana chochote unachofanya. Hakikisha wale unaowahudumia, wakienda kwingine wanaona kama wanapoteza tu. Uzuri ni kwamba hilo liko ndani ya uwezo wako.
3. Usife Haraka.
Ushindani unaweza kuwa mkali kiasi cha kutishia kukuondoa kwenye mchezo. Kuna watu wanakuja kushindana na wewe kwa mbinu chafu. Kama ni kwenye biashara wanashusha sana bei kiasi cha kufanya biashara iwe ya hasara.
Wajibu wako siyo kukimbilia kushindana nao kwenye hizo mbinu zao chafu, bali kuhakikisha unaendelea kubaki kwenye mchezo kwa muda mrefu zaidi.
Washindani wanaotumia mbinu chafu huwa wanafanya hivyo kuwaondoa wengine kwenye mchezo ili wabaki wao wenyewe. Wewe ukiweza kudumu kwa muda mrefu zaidi, watajikuta wanakimbia wao wenyewe na kukuacha wewe.
Hili linahitaji ujipange vizuri na uweze kuvuka vipindi vigumu vya ushindani. Ukiweza kuvuka vipindi hivyo, unakuwa imara zaidi na ushindani hauwezi kukusumbua tena.
Kwenye #BaruaYaKocha, nimeenda kwa kina zaidi kwenye somo hili la kukabiliana na ushindani bila kushindana moja kwa moja.
Isome barua hiyo hapa; #BZK007; Jinsi Ya Kuvuka Ushindani Na Upinzani Kwenye Safari Ya Mafanikio Makubwa.
Rafiki, japokuwa huwezi kuwazuia watu kushindana na wewe, hupaswi kushindana nao moja kwa moja.
Badala yake unapaswa kuuelewa na kuupangilia vizuri mchezo wako kiasi cha kufanya ushindani wowote unaokuja uchoke wenyewe bila hata ya wewe kujua kama wanashindana na wewe.
Fanyia kazi haya uliyojifunza ili uweze kujenga mafanikio makubwa bila kuyumbishwa na yeyote.
Kocha
