Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna kitendawili kimoja kwenye maisha ambacho huwa hata sikielewi. Unakuta watu ambao wangepaswa kufanya kitu ambacho kitawapa matokeo, hawakifanyi kabisa. Huku wale ambao hata hawahitajiki sana kufanya ndiyo wanakifanya.

Utaliona hilo kwenye fedha, matajiri, ambao tayari wana fedha za kuwatosha, huwa wanafanya kazi kwa juhudi zaidi ili kupata fedha zaidi. Japo hata wasipofanya kazi, bado wana fedha za kuwatosha kuendesha maisha yao.

Upande wa pili, masikini, ambao wanahitajika kufanya kazi zaidi ili waondoke kwenye umasikini wao, ndiyo wanakuwa wanakwepa kazi hizo wanazohitajika kufanya. Matokeo yake wanabaki kwenye hali yao ya umasikini.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye upande wa kujifunza. Watu ambao wangetakiwa wajifunze sana, ndiyo wanajiona tayari wanajua kila kitu na hawana cha kujifunza. Wakati wale ambao wanaonekana wanajua, bado wanakuwa na kiu kubwa ya kujifunza.

Socrates, baba wa falsafa na mmoja wa watu wenye busara sana kuwahi kuishi hapa duniani, aliulizwa swali; Inakuwaje wewe unajua sana kuliko wengine? Jibu lake lilikuwa rahisi; ‘Ninachojua ni sijui, hivyo kila wakati nahoji na kujifunza’.

Kama umekuwa unatafuta siri ya mafanikio kwa muda mrefu na hujawahi kupata, ndiyo hiyo hapo, JUA HUJUI. Ukiacha tu ujuaji na ukawa tayari kujifunza, nakuhakikishia utapata mafanikio makubwa unayoyataka.

Unaweza kudhani kwamba unajifunza na hujifanyi unajua. Lakini nikuulize tu swali rahisi, unapokutana na mtu ambaye mmekua pamoja, mmesoma pamoja na wote mlianzia chini, lakini sasa yeye ana mafanikio makubwa kuliko wewe. Nini cha kwanza kinakuja kwenye akili yako?

Je unajiuliza ni kitu gani yeye anajua ambacho wewe hujui na kuwa tayari kujifunza kwake. Je unakubali kwamba kuna vitu anajua na wewe hujui, hivyo kumwomba akufundishe?

Ukiwa mkweli na nafsi yako, sivyo unavyolikabili hilo. Unachofanya ni kuanza kuangalia wapi alipata bahati au fursa ambayo wewe hukupata. Utaanza kuangalia kama alipewa msaada fulani ambao ulimfanya apige hatua.

Utatafuta vitu vingi ili tu uone kwamba kilichompa mafanikio ni kitu fulani alichopata kwa upendeleo, ambao wewe umeukosa.

Huo ndiyo ujuaji ambao umekuzuia kufanikiwa kwa kipindi kirefu cha maisha yako. Ujuaji huo unakuzuia kuwa tayari kujifunza kutoka kwa kila mtu ili uweze kubadili hali uliyonayo sasa.

Rafiki, nataka nikuhakikishie kitu kimoja, kila mtu unayekutana naye kwenye maisha yako, kuna kitu anakijua na wewe hukijui. Na kama utakijua kitu hicho, hutabaki hapo ulipo sasa, kuna namna kitakusogeza mbele zaidi ya hapo ulipo sasa.

Hukwami kwa sababu hakuna ya kujifunza, unakwama kwa sababu unajifanya unajua na hivyo umegoma kujifunza.

Wajibu wangu kama rafiki yako ni kukutoa kwenye huo mtazamo ambao umekukwamisha kwa muda mrefu. Haijalishi umepiga hatua kiasi gani, kuna mambo mengi ambayo bado hujayajua. Kuwa mnyenyekevu na ujifunze.

Na hata kama watu umewazidi kwenye mambo mengi, bado wana mambo mengi wanayoweza kukufundisha, kama utakuwa mnyenyekevu na kujifunza.

Uzuri ni kuwa tayari kujifunza hakupunguzi chochote ulichonacho, zaidi kunaongeza yale uliyonayo. Sasa kwa nini uwe na kiburi cha kukataa kujifunza endelevu?

Kwenye #BaruaYaKocha nimekuonyesha jinsi ambavyo kujua kidogo huwa ni sumu kwa mafanikio makubwa unayoweza kupata. Pia nimekuonyesha jinsi ambavyo kiburi cha mafanikio madogo kimewaangusha wengi waliogoma kuendelea kujifunza.

Isome barua hiyo hapa; #BZK008; Kujua Hujui Ni Silaha Isiyoisha Makali Kwenye Safari Ya Mafanikio

Rafiki, kuna siri muhimu sana ya mafanikio ambayo umetoka nayo hapa; KUJUA HUJUI. Kama utauishi msingi huu kila siku, kwa kuwa tayari kujifunza na kufanyia kazi unayojifunza, huwezi kubaki hapo ulipo sasa.

Vunja kiburi cha ujuaji, kila wakati kuwa tayari kujifunza na unapojifunza fanyia kazi. Hivyo ndivyo kanuni yetu ya mafanikio inavyosema; MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.

Kocha