Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kuna maswali unaweza kuulizwa, wakati mwingine kwa utani tu, lakini yakakufanya ufikiri kwa kina na kulazimika kubadili namna unavyofanya mambo yako.
Moja ya maswali hayo ni; Hivi uko ‘siriazi’ kweli na hili jambo? Hili ni swali ambalo mtu aliniuliza, japo kwa utani, kwenye jambo ambalo hata halina maana sana, lakini swali likanifanya nitafakari zaidi kuliko nilivyowahi kufanya kwenye jambo hilo.
Nilipoona swali hilo rahisi limenitafakarisha sana, nikaona kuna fursa kubwa ya kulitumia kwenye barua ninazoandika kama njia ya kukufanya wewe rafiki yangu uyatafakari kwa kina zaidi machaguo ya maisha yako.
Kitu kimoja ambacho nimejifunza kwenye hii safari ya kujenga mafanikio makubwa ni kile ambacho watu wanapanga na kuongea, na kile hasa wanachofanya ni mbingu na ardhi. Ni vitu viwili ambavyo hakuna namna vinaweza kuja kukutana. Na hilo ndiyo kikwazo kikubwa mno kwenye mafanikio kuliko sababu na visingizio ambavyo wengi wanatoa.
Kwa kifupi, na hili nalisema kwa uchungu sana, watu wengi wanaosema wanataka mafanikio makubwa, hawapo ‘siriazi’ na mafanikio hayo. Na sitaki nikuhukumu kwamba wewe ni mmoja wao, bali nataka nikuulize hilo swali, ujitafakari wewe mwenyewe kwa kina kisha uone kama kweli unamaanisha au unatania na kujidanganya.
Nataka barua hii ikufanye ukae chini, uzichunguze njia zako zote na uone nini hasa kinakukwamisha mpaka sasa kupata mafanikio makubwa unayoyataka. Sitaki tena uendelee kujidanganya wewe mwenyewe au kufuata tu mkumbo kwa sababu umeona wengi wanaongelea swala la mafanikio makubwa.
Ondoka kwenye barua hii ukiwa umefanya maamuzi unayomaanisha kweli. Kama upo siriazi na mafanikio makubwa basi ufanye kile kitakachokupa mafanikio hayo. Na kama haupo siriazi, kitu ambacho pia siyo kibaya, basi uache kujidanganya wewe mwenyewe. Na zaidi, kama unafurahia kujidanganya, basi ujue unajidanganya ili usijipe matumaini hewa.

Mafanikio Makubwa Hayataki Ushujaa, Bali Yanataka Msimamo.
Ni mara ngapi umesoma kitabu, au kushiriki semina au mafunzo ya mafanikio, ukajifunza mambo unayopaswa kufanya ili ufanikiwe. Ukatoka hapo na hamasa kubwa sana ya kwenda kufanya mambo hayo, na kweli ukaanza kuyafanya, tena kwa ukubwa sana? Ukiwa mkweli kwako, ni mara nyingi hilo limekuwa linatokea.
Sasa swali la msingi ni hiyo hamasa kubwa na hatua kubwa ambazo umekuwa unachukua, huwa unafika nazo mbali kiasi gani? Twende taratibu, jikumbushe tu mara ya mwingi kupata hamasa na msukumo na ukachukua hatua kubwa, halafu jiangalie sasa yale unayofanya, kuna mfanano?
Kuna udhaifu wetu sisi binadamu, ambao kama hatutaujua na kuufanyia kazi, utatukwamisha sana kwenye safari yetu ya mafanikio makubwa.
Udhaifu huo ni kutaka ushujaa utupe mafanikio. Udhaifu huo ndiyo unaotusukuma tuanze mambo makubwa kuliko tunavyoweza kuhimili.
Unajifunza umuhimu wa kufanya mazoezi, halafu siku ya kwanza unataka ukimbie kilomita 5, wakati hujawahi kukimbia hata kilomita 1. Unajifunza umuhimu wa kusoma vitabu, unatoka na hamasa ya kusoma kitabu kimoja kila wiki, wakati hujawahi kusoma hata kitabu kimoja kwa mwaka. Unajifunza umuhimu wa kuwafikia wateja wengi ili ukuze mauzo na siku ya kwanza unataka ufikie wateja zaidi ya 100, wakati hujawahi kufikia hata 10 tu.
Sijui unaipata picha hapo rafiki yangu? Unapata hamasa na msukumo mkubwa, unaona kabisa inawezekana na unataka kufanya kwa ukubwa, ili uonekane shujaa. Na matokeo yake, unashindwa pale unapoanza.
Mafanikio makubwa hayataki ushujaa, bali yanataka msimamo. Yanataka msimamo wa kufanya mambo kwa kurudia rudia kufanya kwa muda mrefu bila kuacha. Yanataka mtu anayedumu kwenye kitu kwa muda mrefu. Kwa sababu ni kwa njia hiyo ndiyo mtu anabobea kwenye kitu na kuweza kupata matokeo mazuri.
Huu ndiyo ujumbe wa msingi ambao mafunzo mengi ya mafanikio yamekuwa hayausisitizi, na hilo kupelekea wengi kujipoteza wao wenyewe kwa kuhangaika na ushujaa badala ya msimamo.
Swali la msingi sana unalopaswa kupata majibu yake ni unawezaje kuachana na ushujaa na kwenda kwenye msimamo ambao utakupa mafanikio? Hilo ndiyo unakwenda kupata majibu yake kwenye barua hii, ambayo ukiyafanyia kazi, kweli utakuwa ‘siriazi’ na mafanikio makubwa unayoyataka.
Karibu ujifunze namna ya kufanya mambo kwa msimamo ili uweze kujenga mafanikio makubwa unayoyataka.
1. Weka Malengo Madogo Sana, Ambayo Kushindwa Inabidi Uwe Mgonjwa.
Kwa kuwa tumeona kikwazo cha mafanikio makubwa ni kutaka ushujaa, wa kuanza na malengo makubwa na kushindwa, hatua ya kwanza ni kubadili hilo. Badala ya kuanza na malengo makubwa kwenye kile unachofanya, unaweka malengo madogo sana kiasi kwamba kushindwa inabidi uwe mgonjwa.
Ninaposema madogo, namaanisha madogo kweli kweli. Yaani madogo kiasi kwamba huhitaji kubadili chochote ndiyo uweze kuyatekeleza. Na hata uwe katika wakati mgumu kiasi gani, uweze kuyatekeleza. Kwa sababu tumeona kinachohotajika ni kufanya kwa msimamo bila kuacha. Ili hilo liwezekane, unaanza na malengo madogo sana.
Kwa chochote kile unachotaka kufanya, anza na hatua ya chini kabisa, ya chini mno kiasi kwamba ukishindwa kuitekeleza ni labda unaumwa kiasi cha kulazwa hospitali au haupo to ‘siriazi.’ Kwa mfano kama lengo ni kufanya mazoezi, anza na kutembea hatua 10 tu za mazoezi. Kama lengo ni kusoma vitabu, soma kurasa moja tu kwa siku, kama ukurasa ni mrefu, soma hata sentensi moja tu.
Kama lengo ni kuongeza mauzo, anza na kuongea na mteja mmoja tu mpya kila siku. Kama lengo ni kuandika, anza kwa kuandika sentensi moja tu.
Nafikiri unapata picha hapo, unachohitaji ni hatua ndogo mno, ambayo hakuna namna unaweza kushindwa kuitekeleza. Huwezi kusema upo ‘bize’ kiasi cha kushindwa kusoma sentensi moja tu ya kitabu.
Lengo la malengo haya madogo sana ni kuhakikisha unafanya bila kuacha na kama utaacha basi ujue wazi kwamba haupo ‘siriazi’. Ambacho sitaki ni wewe kujidanganya kwenye hii safari yako ya mafanikio makubwa.
Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza kwa kina mambo matano ya kufanya ili kweli uwe ‘siriazi’ na mafanikio yako makubwa. Ni kwa kuzingatia mambo hayo ndiyo utaweza kujenga mafanikio makubwa unayoyataka, bila kuishia njiani.
Karibu usome barua hiyo hapa; #BZK040; Hivi Uko ‘Siriazi’ Na Mafanikio Makubwa Kweli?
Rafiki, mafanikio makubwa yanahitaji umakini mkubwa kwenye vitu vidogo vidogo sana, ambavyo wengi huwa wanavidharau. Wewe hupaswi kuwa kama wengi wanaotafuta ushujaa kwenye makubwa, wakati madogo yanawashinda. Bobea kwenye madogo kwa umakini mkubwa na makubwa yatakuja yenyewe.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.