Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kauli mbiu yetu kuu kwenye Jumuia ya Washirika Wa Mafanikio ni ‘Nidhamu kali ya kuamua na kufanya kwa msimamo bila kuacha.’ Kauli mbiu hiyo inasisitiza nidhamu kali kwa sababu ndiyo hitaji la msingi sana kwenye safari ya kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha.
Ukiwaangalia watu wachache walioweza kujijengea mafanikio makubwa na ukawalinganisha na wengi ambao hawajaweza kufanikiwa, huoni tofauti kubwa kwa nje. Wengi unakuta wameanzia mahali panapofanana. Lakini baada ya muda tofauti inaonekana. Nidhamu kali ndiyo inayowatofautisha watu.
Watu wamekuwa wanadhani nidhamu ni kitu ambacho mtu anazaliwa nacho pekee. Hivyo imekuwa inaonekana kama wachache wenye nidhamu wana bahati kwa kuzaliwa nazo na wengi wanaokosa nidhamu ni bahati mbaya kwao.
Lakini kiuhalisia, nidhamu ni tabia inayoweza kujengwa kama tabia nyingine. Kwa maana hiyo, kila mtu anayetaka, anaweza kujijengea nidhamu kali inayohitajika ili kupata mafanikio makubwa.
Kwenye barua hii tunakwenda kujadili jinsi ya kujijengea nidhamu hiyo kali ili ikuwezeshe kujenga na kudumu kwenye mafanikio makubwa unayoyataka.

Nidhamu Ni Kanuni Na Siyo Mateso.
Sababu kubwa ambayo imekuwa inawazuia watu kujijengea nidhamu kali inayohitajika ni mtazamo walionao juu ya nidhamu. Nidhamu imekuwa inachukuliwa kama mateso, kujilazimisha kufanya vitu ambavyo hutaki kufanya.
Kwa mtazamo huo, watu wamekuwa wanashindwa kujijengea nidhamu kali kabla hata hawajaanza. Ni vigumu sana kufanya na kufanikiwa kwenye kitu ambacho unakichukulia ni mateso. Kama inabidi ujilazimishe kufanya kitu, hutaweza kudumu kukifanya kwa muda mrefu.
Nidhamu ni kanuni, ambayo haina kabisa nafasi ya mateso wala kujilazimisha ndani yake. Ni kanuni ambayo mtu akiielewa, inakuwa rahisi kwake kujenga nidhamu kwenye jambo lolote lile.
Kanuni kuu ya nidhamu ni kama ifuatavyo;
NIDHAMU = THAMANI + FURAHA – GHARAMA.
Ili kujenga nidhamu, unapaswa kufanya kitu ambacho kina thamani kwako, yaani kitu ambacho kina maana kwako kufanya.
Kwenye kufanya kitu hicho, lazima uwe unapata furaha, inayotokana na kupenda kufanya kitu hicho.
Halafu, gharama ya kufanya kitu hicho iwe ndogo, yaani kusiwe na ugumu kwako kwenye kufanya kitu hicho.
Umejionea hapo rafiki, hakuna kabisa sehemu ya mateso wala kujilazimisha kwenye kujijengea nidhamu kali.
Kwa kanuni hiyo ya nidhamu, mateso na kujilazimisha ni vitu ambavyo vinamzuia mtu kujijengea nidhamu. Kwani unapojilazimisha kufanya kitu, gharama yake inakuwa kubwa na hivyo kukwamisha nidhamu.
Kwa kanuni hii, kila mtu anayetaka anaweza kujijengea nidhamu kali na itakayomfikisha kwenye mafanikio makubwa.
Tutakwenda kuichambua kanuni hiyo ya nidhamu kwa kina na kuongeza mambo ya msingi kuzingatia ili kuhakikisha mtu unajijengea nidhamu kali na isiyoweza kuyumbishwa na chochote.
1. Anza Kwa Kuwa Mkweli Kwako.
Nidhamu inaanza na wewe mwenyewe kuwa mkweli kwako. Inakutaka ujitambue wewe mwenyewe na kuyaishi maisha yako badala ya kuiga maisha ya wengine. Hili linataka sana ujijue wewe ni nani na maisha yako yana kusudi gani.
Ni vigumu sana kuwa na nidhamu kwenye jambo lolote kama hujajitambua wewe mwenyewe. Kwa sababu kutokujitambua kutakufanya uendeshe maisha yako kwa kuiga na kufuata mkumbo.
Unapofanya mambo kwa kuiga na kufuata mkumbo, hupati msukumo mkubwa wa kuendelea nayo, hasa pale unapokutana na magumu na changamoto mbalimbali.
Kuna watu wanajilazimisha kuwa na nidhamu, wakati hawajajitambua wao wenyewe. Wanajilaumu pale wanaposhindwa kudumu kwa muda mrefu kwenye safari wanazoanzisha.
Kabla hujaendelea kuhangaika na nidhamu, anza kwa kujiuliza kama umeshajitambua wewe mwenyewe. Tafakari kama umeshajua wewe ni nani na uko hapa duniani kufanya nini. Hilo ndiyo jiwe la msingi, ambalo nidhamu inajengwa juu yake.
Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza kwa kina mambo matano yanayokamilisha kanuni hiyo ya nidhamu. Kwa kujua na kuyaishi mambo hayo matano, utaweza kujenga nidhamu ambayo siyo mateso. Yaani utakuwa unafurahia kile ambacho wengine wanaona ni mateso.
Na ukishaweza kufurahia ambacho kwa wengine ni mateso, mafanikio makubwa yanakuwa kitu cha uhakika kwako. Kwa sababu ushindani wako utakuwa mdogo sana.
Hakikisha unasoma barua hiyo sasa ili ujiweke kwenye nafasi ya kujenga mafanikio makubwa kadiri ya unavyotaka.
Soma barua hiyo hapa; #BZK041; Tumia Kanuni Hii Kujijengea Nidhamu Kali Itakayokupa Mafanikio Makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.