Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Tarehe 4 mwezi Julai mwaka 1776, kikundi cha wanasheria, wafanyabiashara na wakulima wa nchini Marekani walijiamulia jambo lililokuwa hatari sana kwao.
Walitoa tamko kwamba Marekani ni taifa huru, linalojiamulia mambo yake lenyewe na linaloongozwa kwa misingi ya kila mtu kuwa na haki ya maisha, uhuru na kujitafutia furaha.
Wakati huo Marekani ilikuwa koloni la taifa la Uingereza, ambalo lilikuwa na nguvu kubwa duniani. Uingereza ilikataa kabisa tamko hilo na kuliita ni kitendo cha uasi.
Ilichukua miaka 7 ya mapambano makali mpaka Uingereza kuwa tayari kuipa Marekani uhuru wake. Angalia hapo kati ya kujitangaza ni taifa huru mpaka kuja kuwa huru kweli, ilichukua miaka 7.
Kikundi kilichotoa tamko la uhuru wa Marekani, muda mrefu kabla hata ya kupata uhuru wenyewe, kilifanya jaribio kubwa ambalo halikuwahi kutokea duniani tangu kipindi hicho mpaka sasa. Waliamua kwamba serikali itakuwa inatokana na watu na kwa ajili ya watu, wakati serikali zote kwa wakati huo zilikuwa za kifalme, ambapo watu hawakuwa na uhuru wa kuchagua viongozi, bali walirithi au kupindua.
Waliamua kwamba kila mtu anao uhuru wa kuendesha maisha yake vile anavyotaka na kujipatia mali kwa kadiri ya uwezo na matakwa yake. Kitu ambacho hakikuwahi kuwepo, kwani mataifa yote yalikuwa na matabaka ambapo mtu alibaki kwenye tabaka alilozaliwa.
Miaka 250 baadaye, jaribio hilo limeendelea kuwa lenye mafanikio makubwa. Marekani imeendelea kuwa taifa lenye mafanikio makubwa duniani, taifa lililoleta uvumbuzi wa teknolojia nyingi ambazo zimefanya maisha kuwa bora.
Katika kuchunguza nini kimefanya taifa la Marekani kuwa lenye mafanikio makubwa duniani, Lee Kuan Yew, aliyekuwa kiongozi wa Singapore na aliyeleta mapinduzi makubwa ya kimaendeleo, aliona kitu cha kipekee kabisa.
Lee aliandika; “Utamaduni wa Marekani ni tunaanzia chini na tutakushinda. Walikuwa wanazidiwa na mataifa kama Japan na Ujerumani, lakini wakaja na teknolojia mpya kama kompyuta na intaneti na kuwa kinara duniani.”
Lee aliendelea kuandika; “Ni sehemu ya historia ya Wamarekani, walienda kwenye bara lililokuwa tupu na kuligeuza kuwa taifa lenye mafanikio. Waligawana bara hilo kwa kuambiana wewe ni jaji, wewe polisi, wewe mkulima, mimi mfanyabiashara na mwingine polisi, tuanze. Walianza hivyo na kupata mafanikio na mpaka sasa wana hiyo imani ya kuweza kujenga chochote.”
Lee anasisitiza zaidi kwamba Marekani imeweza kuyashinda mataifa mengine kwa sababu ya uhuru mkubwa ambapo kila tabia ina nafasi ya kuonyeshwa na hilo kuchangia ubunifu na uvumbuvu wa vitu vingi vipya.
Kwa maneno mengine, Marekani limekuwa ni taifa ambalo watu wanaweza kujiamulia mambo bila kukwamishwa na yeyote na kuyageuza mambo hayo kuwa uhalisia. Hicho ni kitu ambacho mpaka sasa kipo na kimelifanya kuendelea kuwa taifa linaloongoza kwa mafanikio duniani.

Rafiki, barua hii siyo historia ya taifa la Marekani, wala kutaka kuonyesha ukuu wake. Bali ni mfano mzuri wa kitu muhimu sana kinachohitajika kwenye kupata mafanikio makubwa.
Kama ambavyo kichwa cha barua hii kinasema, huwezi kupata mafanikio makubwa na ya kipekee kama hutakuwa mtu wa kujiamulia mambo. Na kujiamulia mambo siyo tu kupanga na kuamka, bali kunahitaji kupambania kwa ukubwa ili kupata matokeo ambayo mtu unayataka.
Kwenye barua hii tunakwenda kujifunza mambo muhimu ya kuzingatia kwenye kujiamulia mambo ili kuweza kupata mafanikio makubwa kadiri tunavyotaka.
1. Tamka Kabla Haijawa.
Mafanikio makubwa huwa yanaanzia kwenye fikra kabla hayajaonekana kwenye uhalisia. Watu wengi wanashindwa kufanikiwa siyo kwa sababu hawawezi kufanikiwa, bali kwa sababu hawajawahi kujiona wakifanikiwa kwenye fikra zao.
Wengi wanasubiri mpaka wayapate mafanikio ndiyo waamini wanaweza kufanikiwa. Wakati kiuhalisia inapaswa mtu uamini kwanza unaweza kufanikiwa ndiyo uyapate mafanikio.
Kujiamulia mambo kwenye mafanikio makubwa ni kutoa tamko la mafanikio yako makubwa kabla hata hujayapata. Kama ambavyo Wamarekani walitamka wao ni taifa huru, miaka 7 kabla ya kuupata uhuru wenyewe, ndivyo na wewe unapaswa kutamka umefanikiwa hata kabla hujayaona mafanikio yenyewe.
Kwenye tamko lako la mafanikio husemi kwamba utafanikiwa, bali unasema tayari umefanikiwa. Wamarekani hawakusema watakuwa huru, bali walisema wao ni huru.
Watu wengi wamejikwamisha kufanikiwa kwa sababu wanasubiri mpaka wapate au wapewe kile wanachotaka ndiyo wawe wamefanikiwa. Kwenye hii dunia, hayupo wa kukupa mafanikio yoyote unayoyataka. Hicho ni kitu ambacho mtu unapaswa kujipa wewe mwenyewe.
Na utajipa kwa kujiamulia, kwanza kwa tamko kwamba umeshafanikiwa, kisha kupambana mpaka mafanikio unayoyataka yaje kwenye uhalisia.
Kama bado hujajipa tamko la mafanikio, jipe tamko hilo sasa. Usiendelee kusoma barua hii kabla ya kujipa tamko hilo.
Andaa tamko lako la mafanikio kwa mwongozo ufuatao; ‘Mimi …. (taja majina yako kamili), natamka ya kwamba nina mafanikio makubwa ya …… (taja ndoto zako kubwa), ambayo nimeyajenga kwa msingi wa nidhamu kali ya kuamua na kufanya kwa msimamo bila kuacha.’
2. Usisubiri Mpaka Uwe Na Kila Kitu.
Kitu kikubwa ambacho kimekuwa kinawazuia watu kufanikiwa ni kusubiri mpaka wawe na kila kitu ndiyo waanze safari ya kufanikiwa. Lakini kwa historia ya taifa la Marekani, na hata mpaka sasa, tunaona jinsi ambavyo watu waliopata mafanikio makubwa sana wakianzia chini kabisa, bila ya kuwa na kitu chochote.
Marekani ndiyo taifa ambalo limekuwa na watu matajiri zaidi duniani, kuanzia mamilionea enzi hizi, baadaye mabilionie na sasa matrilionea. Na wengi sana walianzia chini, wakiwa hawana kitu chochote. Lakini kwa kuamini wanaweza kufanya makubwa, walianza na matokeo yamekuwa historia kubwa.
Upo hapo ulipo sasa kwa sababu ya vitu ambavyo bado unaendelea kusubiri vitokee. Badala ya wewe kuanza na kufanya vitu vitokee, unasubiri vitu vitokee ndiyo uanze. Hilo limekukwamisha kwa kiasi kikubwa sana.
Kujiamulia mambo kwenye mafaniko makubwa ni kuanza hata kabla hujawa na kila kitu unachotaka uwe nacho ndiyo ujione unafaa kuanza. Ni kuanzia pale ulipo na kutumia kile ulichonacho kupiga hatua. Kisha kutumia kila matokeo unayoyapata kuendelea kupiga hatua zaidi.
Ukisubiri mpaka uwe tayari kabisa ndiyo uanze kamwe hutaanza, kwa sababu hakuna wakati utajiona umeshakuwa tayari kabisa. Ukisubiri mpaka mazingira yawe na kila unachohitaji ndiyo uanze kamwe hutaanza, kwa sababu kila wakati kuna vitu vitakuwa vinakosekana.
Alichokieleza Lee Kuan Yew kama kinachowatofautisha Wamarekani, kwa kuanza na eneo lisilokuwa na kitu na kuweza kujenga kila kitu, ndicho tunapaswa kufanya kwenye maisha yetu. Tunapoanzia sipo tunapotaka kuwa, lakini pia tunakuwa hatuna njia za uhakika za kutufikisha kule tunakotaka kufika. Namna pekee ya kufika huko ni kuamua kwamba tutafika, kisha kutumia kila tulichonacho na kinachopatikana.
Hannibal, aliyekuwa kamanda mkuu wa jeshi la Carthaginian aliambiwa na makamanda wengine kwamba hataweza kuvuka milima ya Alps kwenda Italy wakati wa vita ya pili ya Punic, miaka 218 kabla ya Kristo. Hannibal aliwajibu akisema; ‘Ni labda nitapata njia au nitaitengeneza.’ Aliweza kuvuka na kushinda vita hiyo, na ndiyo maana historia inamkumbuka.
Je, wewe ni maeneo gani ambayo umeshawishiwa huwezi kwa sababu hakuna njia? Je upo tayari kuanza, kwa kutafuta njia au kutengeneza? Maana hicho pekee ndiyo kilichopo kati ya hapo ulipo sasa na mafanikio makubwa unayotaka kuyapata kwenye maisha yako.
Usisubiri mpaka uwe na kila kitu, anza na kile ulichonacho. Usisubiri mpaka njia ipatikane, tafuta njia au tengeneza mpya. Hayo yote yako ndani ya uwezo wako, usijikwamishe kwa namna yoyote ile.
Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha kwa kina mambo mengine matatu ambayo unapaswa kuyajua ili uweze kujiamulia mambo na kujenga mafanikio makubwa. Hapa umeyapata mawili, kwenye barua yapo matano na yote ni muhimu sana.
Kujifunza yote matano, fungua barua hapa; #BZK037; Mafanikio Makubwa Yanataka Uwe Mtu Wa Kujiamulia Mambo.
Rafiki, mafanikio yangekuwa ni kitu kinachogawiwa, wote waliorithi mafanikio wangekuwa nayo. Lakini wengi waliorithi mafanikio au kupata fursa nzuri kwa bahati, wameishia kupoteza.
Mafanikio yanakutaka uwe mtu wa kujiamulia mambo kwa kutoa tamko la mafanikio yako. Kisha kupambana kutetea tamko hilo dhidi ya wote watakaokupinga na kukukwamisha. Halafu unachagua kuwa wewe, pamoja na utofauti mkubwa ulionao, huo ndiyo unaokupa matokeo ya tofauti.
Usisubiri kuamuliwa ufanye nini, usisubiri upewe ruhusa ya kuwa vile unavyotaka. Jiamulie mafanikio yako, huo ndiyo wajibu namba moja wa maisha yako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.