Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Najua unayataka sana mafanikio, ndiyo maana unasoma hapa. Na najua unataka kwenda zaidi ya hapo ulipo sasa, ndiyo maana umekuwa mfuatiliaji mzuri wa mafunzo mbalimbali ninayotoa.
Pia najua kuna madhaifu yako binafsi ambayo umekuwa unayaona ni kikwazo kwako kufanikiwa. Kwa sababu ya madhaifu hayo, umekuwa unakwama mara nyingi, kiasi cha kuona madhaifu hayo yamekushinda.
Umekuwa unajifunza kuhusu umuhimu wa kuamka asubuhi na mapema, ili uweze kupangilia na kufanya mambo yako muhimu. Unaweka kabisa alamu kwenye simu yako ili ipige kelele muda wa kuamka unapofika. Lakini wewe mwenyewe umekuwa unajua kinachotokea, alamu inaita, unaizima kwa kujiambia unalala dakika chache tu. Unakuja kushtuka tayari umechelewa kuamka. Hapa unajiambia una udhaifu kwenye nidhamu ya kuamka mapema.
Ni mara ngapi umepata wazo zuri sana la kitu ambacho ni muhimu. Ukajiambia utakumbuka wazo hilo wakati unafanyia kazi kitu hicho. Lakini unapofika wakati unahitaji kukumbuka wazo hilo, inashindikana. Unakazana sana kuvuta kumbukumbu, lakini haziji kabisa. Hapa utajiambia una udhaifu wa kumbukumbu.

Rafiki, hiyo ni mifano michache kati ya mingi uliyonayo, ya jinsi ambavyo unakwama kwenye mambo unayopanga wewe mwenyewe, kwa sababu zako mwenyewe. Kwa wingi wa mambo ya aina hiyo, ni rahisi kushawishika kwamba madhaifu uliyonayo yanakuzuia kufanikiwa.
Lakini, vipi kama nikikuambia kwamba hayo hayo madhaifu uliyonayo ndiyo uimara wako wa kufanikiwa? Ndiyo, namaanisha hicho unachoona ni kikwazo kwako kufanikiwa, unaweza kutumia kuwa sababu ya kufanikiwa.
Hilo ndiyo unakwenda kutoka nalo kwenye barua hii, ili usikwamishwe tena na madhaifu uliyonayo. Karibu ujifunze kugeuza kile unachokiona udhaifu kwako kufanikiwa kuwa uimara utakaokupa mafanikio makubwa unayoyataka.
1. Usishindane Na Udhaifu.
Moja ya mafunzo yasiyo sahihi ambayo wengi tumepewa na yakawa kikwazo wetu ni kufanyia kazi madhaifu tunayokuwa nayo. Tumekuwa tunashauriwa tuyajue madhaifu yetu, kisha tuyafanyie kazi ili tuweze kuwa bora kwenye maeneo hayo.
Tunapofanya hivyo, tunaishia kuwa na madhaifu ambayo ni imara zaidi. Yaani unakuwa na madhaifu yenye nguvu ya kukukwamisha zaidi. Unapokabiliana na madhaifu yako, kwa lengo la kuyageuza kuwa uimara, unayafanya kuwa madhaifu yenye nguvu zaidi ya kukukwamisha.
Unaweza kuyadharau madhaifu yako, kwa sababu unayaona ni madhaifu, lakini utakapojaribu kuyakabili ndiyo utajua jinsi yalivyo na nguvu kubwa kwenye kukukwamisha. Kadiri unavyoweka nguvu na umakini kwenye maeneo ambayo ni dhaifu, ndivyo unayapa nguvu ya kukukwamisha.
Kinachofanya tuhangaike na madhaifu ni kudhani tuna utashi wa kutosha kupambana na madhaifu hayo. Lakini utashi tulionao huwa unachoka kadiri tunavyopambana na kitu.
Kwa mfano, kama unataka kuacha tabia fulani, halafu ukawa kwenye mazingira yanayochochea ile tabia, unaweza kukazana kujizuia kufanya tabia hiyo. Lakini unapokuwa kwenye hali ya uchovu au msongo, unajikuta umerudi kwenye hiyo tabia.
Katika hali ya kawaida unajikuta ukiweza kutumia utashi kuzuia tabia au udhaifu mwingine. Lakini katika hali ya msongo au uchovu, utashi unakosa nguvu ya kutosha kupambana.
Njia ya kugeuza madhaifu yako kuwa uimara ni kuyatambua, kisha kuacha kabisa kupambana nayo kwa namna yoyote ile. Usitumie nguvu kujizuia kwenye madhaifu, wala usitake kuwa imara kwenye madhaifu hayo. Yajue, kisha fanya kinachofuata hapo chini.
2. Tengeneza Mazingira Yanayovuka Udhaifu.
Kwa kuwa tumeona utashi, pamoja na nia yake njema huwa unashindwa, namna pekee ya kugeuza madhaifu kuwa uimara ni kutengeneza mazingira yanayovuka madhaifu tunayokuwa nayo. Kila madhaifu uliyonayo huwa yana mazingira yanayochochea madhaifu hayo kupata nafasi. Kwa kutengeneza mazingira yanayozuia hilo, unakuwa umeyageuza madhaifu kuwa uimara.
Tukiangalia mifano miwili tuliyoanza nayo, umekuwa unaweka alamu ya kukuamsha, halafu unalala nayo karibu. Alamu inapoita, unaweza kuifikia na kuizima, kitu kinachofanya uendelee kulala. Lakini kama utaweka alamu mbali kiasi kwamba unalazimika kuamka kwenda kuizima, hilo litaondoa ushawishi wa kuendelea kulala.
Kadhalika kwenye mawazo mazuri unayopata na kujiambia utayakumbuka, kama ukiwa na utaratibu wa kuwa na mahali pa kuandika mawazo mazuri unayoyapata, huna haja ya kujilazimisha kukumbuka. Kwa kuwa umeandika mawazo yako mazuri, ni rahisi kurejea pale unapokuwa unayahitaji.
Kwa tabia yoyote ile unayotaka kuondokana nayo, tengeneza mazingira yanayoizuia tabia hiyo kupata nguvu. Kama unayaka kuacha kutumia vitu vya aina fulani, hakikisha mazingira yako hayana vitu hivyo. Mfano, kama unataka kuacha pombe, usikae na pombe ndani. Unaweza kudhani una utashi wa kujizuia, lakini siku umevurugwa utajikuta unakunywa.
Na kwa tabia mpya unazotaka kujijengea, fanya mazingira yawe yanachochea tabia hiyo. Ifanye tabia mpya unayotaka kujenga kuwa rahisi na haraka kwako kuitumia pale unapokuwa kwenye hatua ya kufanya hivyo. Kwa mfano, kama unataka kufanya mazoezi unapoamka, hakikisha mavazi na vifaa vyote vya mazoezi vipo tayari na karibu.
Mazingira yana nguvu kubwa kuliko utashi ulionao. Mazingira yanabaki vile vile hata pale utashi wako unapokuwa umechoka. Ili kugeuza udhaifu wako kuwa uimara, tengeneza mazingira ambayo udhaifu ulionao haupati nguvu kabisa.
Kama una udhaifu wa kutumia sana mitandao ya kijamii badala ya kusoma vitabu, tenga mazingira ambayo hutatumia kabisa simu na mnadala pekee kuwa kusoma. Hapo unaweza kutenga eneo fulani ambali ukiwa hapo ni majukumu muhimu tu, wakati huo simu ikiwa eneo la mbali kabisa na hapo.
Tengeneza mazingira yanayokupa wewe upendeleo wa kufanya kile unachotaka na kuepuka vishawishi vinavyokukwamisha. Hivyo ndivyo unavyogeuza udhaifu wako kuwa uimara.
Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha kuna mambo matatu ya ziada kwako kufanyia kazi ili uweze kugeuza udhaifu unaokuzuia kufanikiwa kuwa uimara utakaokupa mafanikio makubwa unayoyataka.
Karibu usome barua hiyo hapa; #BZK038; Huu Udhaifu Unaokuzuia Kufanikiwa, Ndiyo Uimara Utakaokupa Mafanikio Makubwa.
Kitu kimoja unachopaswa kutoka nacho hapa ni kwamba, tayari unazo rasilimali za kukutosha kupata mafanikio yoyote unayoyataka. Unachohitaji ni kujua jinsi ya kutumia rasilimali hizo ulizonazo ili kujenga maisha unayoyataka.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.