Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Maisha ni mchezo mmoja mkubwa sana na ambao tunapaswa kuucheza kwa mwendelezo. Ni mchezo ambao tunaucheza kwa mtindo wa ligi, ambayo inakuwa endelevu na siyo mashindano ya muda mfupi.
Kwenye mchezo unaoendeshwa kwa ligi, matokeo ya mchezo mmoja siyo yanayoamua ushindi. Timu inaweza kupoteza baadhi ya michezo na bado ikapata ushindi wa ligi nzima.
Moja ya sababu zinazopelekea wengi kutokufanikiwa kwenye maisha ni kuyachukulia kama mashindano ya muda mfupi. Wanapopoteza mchezo mmoja, wanaona ndiyo mwisho wa mashindano yote ya maisha.
Wengi wanaendesha mchezo wa maisha kwa mtazamo wa kucheza ili kumaliza. Hivyo inapotokea wameshindwa kwenye mchezo mmoja, wanavunjika moyo na kushindwa kuendelea vizuri.
Kiuhalisia, maisha ni mchezo usio na mwisho, kama upo hai, mchezo unaendelea. Hivyo wajibu wetu ni kucheza ili kuendelea kucheza na siyo kucheza ili kumaliza. Kwa kipindi chote unachokuwa hai, mchezo unaendelea.
Kinachopelekea wachache wanaopata mafanikio na kuishia kuanguka ni kuacha kucheza baada ya kupata matokeo mazuri, kwa kudhani wameshamaliza kila kitu. Na kinachowafanya wanaoshindwa kubaki wameshindwa ni kuacha kucheza kwa sababu ya matokeo mabaya, kwa kudhani hawawezi kuyabadili.

Watu wamekuwa wanahangaika sana kutafuta njia za mkato za kushinda kwenye huu mchezo wa maisha, lakini hazijawahi kuwepo. Wengi wanahangaika na mbinu na siri ambazo zinaweza kufanya kazi kwa muda mfupi, lakini hazina madhara wala matokeo ya muda mrefu.
Namna pekee ya kuathiri mchezo wa maisha na kuwa na udhibiti kwenye ushindi ni kujenga tabia sahihi za ushindi. Unapojenga tabia za ushindi, unakuwa na uhakika wa kupata ushindi, hata kama matokeo ya mchezo mmoja mmoja siyo mazuri kama mtu unavyotarajia.
Kwenye barua hii unakwenda kujifunza kuhusu eneo hilo la tabia za ushindi, utaona kwa nini inakubalika kupoteza matokeo lakini haikubaliki kamwe kupoteza tabia.
1. Matokeo Hayahami, Ila Tabia Zinahama.
Unaposhindwa kwenye mchezo, matokeo uliyopata hayawezi kuhama kwenda kwenye mchezo mwingine unaofuata. Lakini tabia unazokuwa nazo kwenye mchezo huo, utaendelea kuwa nazo kwenye michezo mingine inayofuata. Hili linatuonyesha ni kwa namna gani tabia zilivyo muhimu na zenye nguvu kuliko matokeo ambayo unayapata.
Matokeo hayapo ndani ya udhibiti wako. Kuna mambo mengi sana yanayoweza kuathiri matokeo yako, ambayo huna udhibiti nayo wa moja kwa moja. Unaweza kufanya kila unachopaswa kufanya, lakini bado matokeo yakaja tofauti na ulivyotegemea yaje.
Tabia zako ni kitu ambacho kipo ndani ya udhibiti wako. Namna unavyopokea matokeo unayopata na namna unavyoendea mchezo unaofuata ni vitu vilivyo ndani ya uwezo wako kudhibiti.
Wajibu wako mkubwa kwenye maisha ni kuhakikisha unajenga na kulinda tabia sahihi za mafanikio. Unapaswa kulinda tabia hizo dhidi ya matokeo unayoyapata, zisiathiriwe kabisa. Iwe umepata matokeo mazuri au mabaya, tabia zako zinapaswa kuwa vile vile wakati wote.
Tabia ni mazoea ambayo yanarudiwa bila hata kufikiria. Ukiruhusu matokeo unayopata kuathiri tabia, utaishia kupata matokeo mabovu mara zote. Wakati ukijenga tabia ambazo ni imara, matokeo mabovu unayopa nyakati fulani hayawezi kuendelea kila wakati.
Kwa sababu hatuwezi kuathiri matokeo, unapaswa kufanyia kazi kitu unachoweza kukiathiri moja kwa moja, ambacho ni tabia zako. Jenga tabia imara ya kufanya kwa ubora mara zote bila kujali matokeo uliyoyapata. Tabia hiyo imara utaenda nayo mara zote, wakati matokeo unaweza kuyaacha nyuma.
2. Matokeo Ni Ya Muda, Tabia Ni Za Kudumu.
Unapochukua hatua, unazalisha matoke. Ukichukua hatua nyingine, unazalisha matokeo mengine, ambayo yanafuta yale matokeo ya nyuma. Hivyo matokeo unayoyapata ni ya muda tu, yanakuja kufutwa na matokeo mengine. Na kwa sababu maisha ni mchezo wenye mashindano endelevu, kila siku kuna matokeo mapya.
Tabia ni tofauti kabisa na matokeo, kwa sababu huwa ni za kudumu. Kila unapoifanya tabia, ndiyo unazidi kuiimarisha zaidi. Kadiri unavyorudia rudia tabia ndivyo inavyokuwa imara kwako.
Kwa kujua uzito huo wa tabia, tunapaswa kuzilinda sana zisiathiriwe na matokeo ya kupoteza. Ukipoteza matokeo fulani, unaweza kubadili hilo kwenye matokeo yanayofuata. Lakini ukipoteza tabia, unaendelea kubaki kwenye tabia hiyo ya kupotea kwa muda mrefu.
Kataa kabisa matokeo unayopata kuathiri tabia zako, kwa sababu athari hiyo itadumu muda mrefu kuliko matokeo yaliyosababisha. Unajuka kujikuta muda mrefu ujao una tabia zilizosababishwa na matokeo ambayo ulishayasahau kabisa.
Tenganisha kabisa matokeo unayopata na tabia zako, ili kuzuia kitu cha muda mfupi kisiwe na athari za muda mrefu kwako. Usiwe kama mtu anayetangaza ndoa kwenye mtoko wa kwanza na mchumba, uchumba ni kitu cha muda, ndoa ni kitu cha kudumu. Siyo kila unayekuwa naye kwenye uchumba anaweza kuwa mwezi wa kudumu.
Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha kuna mambo matatu ya ziada kwako kufanyia kazi ili uepuke kupoteza tabia pale unapopoteza matokeo. Hayo ni mambo ya msingi sana kwako kufanyia kazi ili uache kujikwamisha kwa kuruhusu matokeo kuathiri tabia.
Karibu usome barua hiyo hapa; #BZK039; Inakubalika Kupoteza Matokeo, Haikubaliki Kamwe Kupoteza Tabia.
Umekuwa unapambana sana kupata matokeo unayoyataka, kitu ambacho kinakuwa na athari kubwa kwenye tabia zako pale matokeo yanapokuwa tofauti. Ni wakati sasa ujijengee tabia imara, ili ujihakikishie mafanikio hata kama utapoteza baadhi ya matokeo.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.