Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Inashangaza jinsi ambavyo watu wengi wanahangaika kupata siri za maisha na mafanikio, wakati kuna kitu cha msingi sana ambacho bado hawajajua. Yaani ni sawa na mtu anayehangaika kutaka kujua atapaka nyumba yake rangi gani, wakati hata tofali moja hajajenga.
Siyo kwamba hivyo vitu vya juu havina umuhimu, ila vinakosa maana kama vitu vya msingi havitafanyiwa kazi kwanza. Na hilo limekuwa linajidhihirisha kwa jinsi watu wanahangaika na maisha na bado hawapati kile wanachotaka.
Kosa kubwa linaanzia kwenye kutokujijua wao wenyewe kwanza. Hivyo chochote wanachohangaika nacho kinakuwa hakiwafai wala kuwaridhisha, kwa sababu hakiendani na wao.
Kwa umuhimu wa mtu kujijua yeye mwenyewe kwanza, Wagiriki wa kale walikuwa na mwongozo mkuu wa kifalsafa uliochapwa kwenye maeneo yote muhimu. Mwongozo huo ulisema; “Know Thyself”, ikimaanisha Jijue Mwenyewe. Walitambua nguvu ya kujitambua kwenye maisha, kwani hilo likikosekana, mengine yote yanakosa maana.

Kwenye mafunzo mengi ambayo nimekuwa natoa, kupitia vitabu kama UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA na barua nyingi ambazo nimeshashirikisha hapa, nimekuwa nasisitiza kuhusu uwezo mkubwa ulio ndani ya kila mtu. Watu wanasoma hayo, wanatikisa vicha kukubali, wanaweka maoni kwamba wamejifunza, lakini bado wanabaki pale pale.
Wengi wanaposhindwa kupiga hatua licha ya kujifunza, wanaona labda maarifa hayafanyi kazi au wao wana utofauti ambao maarifa hayo hayajauelewa. Lakini ukweli unabaki pale pale, tatizo la kwanza, ambalo ndiyo la msingi kabisa ni watu kutokujijua wao wenyewe.
Kwa sababu hawajajijua, wanajikuta wanafanya mambo kama ambavyo wamezoea kufanya, lakini hilo linakuwa kikwazo kwao kupata matokeo ambayo wanayataka.
Ndiyo maana kwenye barua hii nimeona turudi kukumbushana mambo ya msingi sana. Mambo ambayo nimekuwa nakuambia, lakini hapa nataka kusisitiza na kuweka mkazo zaidi.
Madhumuni yangu ni unaposoma barua hii, na kuweka maoni yako kwa kile ulichojifunza, ukaweke kwenye matendo kweli bila kujikwamisha kwa namna yoyote ile.
Sehemu Tatu Za Akili Yako.
Kwenye somo la baiolojia, huwa tunafundishwa sehemu tatu za ubongo. Ubongo wa chini, wa kati na wa juu. Kila ubongo ukiwa na kazi zake, wa chini ukiwa wa kuhakikisha uko hai, wa pili wa tabia na wa tatu wa kufikiri na kufanya maamuzi.
Ubongo ni kama nyumba, ambayo tayari ina vyumba, hivyo haviwezi kubadilika. Akili ni kama umeme unaopita kwenye nyumba, hivyo akili inakuwa kwenye ubongo, lakini ni kitu kisichoonekana. Mtu akifanyiwa upasuaji, ubongo utaonekana, lakini akili haitaonekana. Kama ambavyo unaweza kuona nyaya za umeme, lakini huwezi kuona umeme wenyewe.
Akili tulizonazo ndizo zinazotufanya sisi kuwa binadamu. Akili ndiyo inafikiri, kufanya maamuzi na kutusukuma kuchukua hatua tunazochukua.
Tumekuwa tunachukulia akili kama ni moja, na hapo ndipo tumekuwa tunakwama kwenye kupata matokeo tunayotaka. Kwa kudhani akili yetu ni moja, tunashindwa kuitumia vizuri na pia kushindwa kuvuka mitego tunayowekewa na akili yetu.
Akili yetu wanadamu imegawanyika kwenye sehemu tatu, kila sehemu ikiwa na kazi yake na mchango wake kwenye matokeo tunayopata kwenye maisha. Ni kwa kujua sehemu hizo za akili na jinsi ya kuzitumia ndiyo tunaweza kujenga aina ya maisha tunayoyataka.
Kwenye barua hii tunaenda kujifunza kwa kina sehemu hizo tatu za akili, jinsi kila akili inavyofanya kazi na namna bora ya kuitumia sehemu hiyo ya akili kupata mafanikio makubwa tunayoyataka.
1. Akili ya Chini ya Ufahamu (Subconscious Mind)
Hii ni akili isiyofikiri moja kwa moja, lakini yenye nguvu ya kufanya maamuzi na kuchochea kuchukua hatua. Akili hii ni nguvu inayotekeleza kile inachoambiwa, lakini haiwezi kuamua yenyewe. Hii ndiyo akili inayofanya kazi kwenye sehemu kubwa ya yote tunayofanya, na inafanya kwa mazoea.
Akili Isiyofikiri huwa ni kama mtumwa mwaminifu, yenyewe inatekeleza kile inachoambiwa na akili inayofikiri. Na inachukulia chochote ambacho mtu anafikiria kwa muda mrefu kama kitu muhimu zaidi na hivyo kukitekeleza. Akili hii huwa inatekeleza yenyewe bila kusubiri kuambiwa.
2. Akili ya Ufahamu (Conscious Mind)
Hii ndiyo akili inayofikiri na kufanya maamuzi yote kwenye maisha yetu. Akili hii huwa inaona uhalisia wa dunia kama ilivyo. Hii ni akili ambayo inaendeshwa kwa mantiki na ushahidi halisi. Akili hii huwa inahitaji taarifa, inazichakata na kufanya maamuzi.
Akili hii ndiyo inayoongoza maisha yetu kwenye mambo yote tunayoyafanya. Lakini pia ndiyo akili inayotengeneza ile isiyofikiri, kupitia yale ambayo inayafikiria mara kwa mara. Fikra zinazokaa kwenye akili inayofikiri ndiyo zinachukuliwa na akili isiyofikiri kama amri ya kutekeleza.
3. Akili ya Juu ya Ufahamu (Superconscious Mind)
Hii ni akili ya juu, ambayo mtu huwezi kuitumia kufikiri, lakini huwa inaleta kwako fikra za vitu gani unapaswa na unaweza kufanya. Akili hii ni ya Kiungu, ambayo ina nguvu ya kimiujiza ya kukuonyesha vitu ambavyo haviwezi kufikiriwa kwa akili ya kawaida.
Kwenye vitabu vya imani imeelezwa kwamba mwanadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu. Sasa ile akili ya Mungu, akili ya uumbaji, ndiyo inatuingia binadamu kupitia akili hiyo ya juu ya ufahamu. Hii ni akili ambayo huwa inakuwa ya kipekee kwa mtu na huwa haipo kwenye udhibiti wetu.
Ni akili ambayo mtu anaweza kuifikia kupitia njia zinazofunga akili inayofikiri na isiyofikiri. Njia kama maombi, tafakari za kina, tahajudi na nyingine zinazotuweka kwenye utulivu, huwa zinafungua akili hiyo kwetu.
Rafiki, hapa nimekueleza kwa ufupi kuhusu akili hizo tatu. Jinsi ya kutumia akili hizo kujenga mafanikio makubwa nimeeleza kwenye #BaruaYaKocha. Unapaswa kuisoma barua hiyo kwa kina ili uweze kutumia vizuri akili yako.
Karibu usome barua hiyo hapa; #BZK036; Zijue Akili Zako Tatu Na Jinsi Ya Kuzitumia Kujenga Maisha Unayoyataka.
Kwa muhtasari, tumia akili zako tatu hivi;
Kwa kuwa akili pekee ambayo tuna udhibiti nayo kwa asilimia 100 ni inayofikiri, hiyo ndiyo tunayopaswa kuitumia kufikia akili nyingine mbili zinazotupa matokeo.
Kwanza tunatumia akili inayofikiri kuweka fikra, picha na hisia za matokeo tunayoyataka. Hilo linapeleka amri kwenye akili isiyofikiri na kuhakikisha inatekelezwa kuwa uhalisia.
Pili, tunaituliza akili isiyofikiri na kuondoa usumbufu, ili iweze kusikia na kupokea zile fikra zinazoletwa kwetu na akili ya ufahamu wa juu. Mara nyingi akili hiyo huwa inazungumza na sisi, lakini sisi tunakuwa tumevurugwa na usumbufu mwingi hivyo hatuisikii.
Kwa kuwa na udhibiti mzuri kwenye akili yetu inayofikiri, tunajikuta tukidhibiti akili sisyofikiri na akili ya ufahamu wa juu. Ni kwa njia hiyo ndiyo tunaweza kutengeneza maisha yoyote tunayotaka, tukawa na mafanikio, utajiri na uhuru wa kifedha.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.