Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Huwa kuna kauli inayosema hakuna kitu kipya kabisa chini ya jua. Yote ambayo tunayaona sasa, yamewahi kuwepo. Mengi kwa namna yalivyo sasa na machache kwa namna ya tofauti.

Kauli hiyo ni ya kweli na yenye nguvu sana. Kwani licha ya mabadiliko makubwa ya teknolojia ambayo dunia imepitia kwa karne mbili sasa, bado mambo mengi ni yale yale, yamejivika tu sura mpya.

Hiyo ndiyo sababu dini na falsafa za kale mpaka leo zina mafundisho yanayotunufaisha, licha ya mambo hayo kufundishwa na kuandikwa kwa miaka mingi iliyopita.

Moja ya vitabu ambavyo huwa nasoma kwa kurudia rudia ni barua zenye mafunzo bora ambazo zimewahi kuandikwa na watu mbalimbali. Kwenye falsafa ya Ustoa, barua za Seneca ni moja ya maandiko yenye mafunzo makubwa kwenye maeneo mengi ya maisha.

Kuna barua za Rockefeller kwa kijana wake, ambazo zina mafunzo mengi sana kwenye kujenga biashara na utajiri. Kuna barua ambazo watu waliandika kwa watu wao wa karibu na hata kwa wengine pia. Nina vitabu kadhaa ambavyo ni mkusanyiko wa barua.

Moja ya kitabu hicho ni cha Barua Za Napoleon, aliyekuwa mtawala wa Ufaransa na aliyefanya mambo makubwa na ya kipekee. Napoleon alipenda sana kuwasiliana kwa barua na kitabu chenye mkusanyiko wa barua zake nyingi kinaitwa Mind Of Napoleon.

Katika kusoma barua hizo, nimekutana na barua moja ambayo Napoleon alimwandikia mdogo wake Jérôme, aliyekuwa Mfalme wa Westphalia. Barua hiyo aliiandika mwaka 1808 na ilikuwa na ushauri ambao una manufaa makubwa sana kwetu mpaka sasa.

Ushauri huu unaendana kabisa na yale tunayofanyia kazi kwenye Jumuia Ya Washirika Wa Mafanikio, kwenye kujenga Mafanikio, Utajiri na Biashara zisizotutegemea.

Napoleon alimshauri Jérôme vitu vitatu ambavyo ni;

Moja; heshima, shukrani na uaminifu kwake na kwa watu wa Ufaransa ambao kwao ana deni kubwa la kulipa.

Mbili; kuwa na uchumi mkali zaidi ili kuondoa tofauti yake na anaowatawala. Na hapa kwenye uchumi alimwelekeza namna anavyopaswa kugawa kipato chake, nusu kiende kwenye matumizi ya msingi, robo akiba ya dharura na robo uwekezaji.

Tatu; kutumia muda wake kujifunza vitu asivyojua, kama kujenga jeshi na utawala wa haki na fedha.

Napoleon alimwambia Jérôme, atakapotimiza hayo matatu ndiyo atastahili heshima yake, ya watu wa Ufaransa na ya wale anaowatawala.

Hakuishia hapo, alimweleza kabisa namna ya kukamilisha yote matatu, kwa kujitafakari (reflections), kuleta mageuzi (reforms) na kubadili njia zake binafsi.

Rafiki, unapoyaangalia kwa kina mambo hayo matatu, na kuangalia kwa undani mambo ya kwenye uchumi, utaona ndiyo mambo ambayo tumekuwa tunashauriana na kupeana miongozo kupitia barua hizi na mafunzo mengine tunayoshirikishana.

Kwenye #BaruaYaKocha, nimeyaeleza kwa kina mambo hayo matatu na jinsi ya kuyatekeleza kwenye safari yetu ya mafanikio makubwa.

Nameyageuza mambo hayo kutoka barua ya Napoleon kwenda kwa Jérôme na kuwa #BaruaYaKocha kwenda kwa Wanamafanikio. Karibu ujifunze kwa kina na kwenda kuyafanyia kazi kwa uhakika kwenye safari ya mafanikio.

Karibu uisome barua hiyo hapa; #BZK035; Ushauri Huu Uliotolewa Miaka 218 Iliyopita, Bado Unakufaa Zaidi Leo.

Rafiki, kama inavyosemekana kwamba hakuna kitu kipya chini ya jua, ushauri huu uliotolewa miaka 218 iliyopita, unafanya kazi vizuri sana hata sasa. Kama ukijifunza kwa kina na kuutumia ushauri huo kwenye maisha yako ya sasa, lazima utapiga hatua kubwa.

Ipo ndani ya uwezo wako kuyabadili maisha yako kwa namna unavyotaka wewe mwenyewe. Fanyia kazi ushauri huu na uyaone maisha yako yakibadilika kwa namna unavyotaka wewe.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.