Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Ushauri ni kitu kimoja ambacho watu wengi sana huwa wapo kukitoa bure kabisa, hata kama hawajaombwa kufanya hivyo. Imezoeleka kutoa na kupokea ushauri kwenye kila fursa inayojitokeza.

Huwa nasema wazi kwamba gharama ya ushauri wa bure utaiona pale utakapoanza kuufanyia kazi. Ni katika wakati huo ndiyo utajua kwa nini ulipewa ushauri huo bure au kwa urahisi sana.

Changamoto ya ushauri kutokufanya kazi haipo tu kwenye ushauri wa bure, upo pia ushauri wenye gharama na bado haufanyi kazi. Na aina hiyo ya ushauri imewapoteza wengi, kwa sababu wanapata ushauri huo kwa watu wanaowaamini kama wataalamu na wabobezi kwenye eneo wanalowashauri.

Katika hali hizo, tunapaswa kuwa na umakini mkubwa kwenye kila ushauri tunaopokea. Ule tunaopata bure tunapaswa kuuepuka sana, kwa sababu huo madhara yake ni makubwa.

Na ule tunaopata kwa gharama zozote zile, iwe ni za fedha, muda au nguvu, tunapaswa kuuchuja kwa usahihi ili uwe na manufaa tunayoyataka.

Kwa vyovyote vile, hupaswi kupokea ushauri wowote bila kuuhoji na kuuchakata kuona kama unaendana na hali yako. Kwa sababu, mara nyingi ushauri huwa unatolewa kwa hali za jumla, wakati tatizo au hali yako siyo ya jumla, bali inayokulenga wewe moja kwa moja.

Kwa kuwa wewe ndiye unayejijua kwa undani zaidi, kila ushauri unaopewa lazima uuchakate kuendana na hali yako maalumu.

Ushauri Ukishakuwa Mwingi, Jua Haufanyi Kazi.

Huwa kuna kauli ambayo huwa inatumiwa kama utani kwenye eneo la dayati, lakini kama ulivyo utani, huwa una ukweli ndani yake. Kauli hiyo inasema; “Kama dayati zingekuwa zinafanya kazi, ingekuwepo moja tu.”

Unapotafakari kauli hiyo, unaona ukweli ambao nakuambia hapa, kwamba, kadiri ushauri unavyokuwa mwingi, maana yake hakuna hata mmoja unaofanya kazi. Kama kungekuwa na ushauri mmoja unaofanya kazi, kusingehitajika kuwa na ushauri mwingine, tena unaopingana na huo unaofanya kazi.

Hivyo basi, moja ya njia za kupima ufanisi wa ushauri unaopokea ni kuangalia kama kuna aina nyingine nyingi za ushauri tofauti kwenye eneo hilo. Tena pale kunapokuwa na ushauri mwingi na unaopingana, na zote zinakubalika na watu, ni kiashiria kikubwa kwamba hakuna hata mmoja ambao ni sahihi.

Kinachofanya ushauri uwe mwingi, licha ya kutokufanya kazi ni tabia ya watu kutaka kusikia kile wanachotaka kusikia. Na wale wanaotoa ushauri, wanachagua kuwaambia watu kile wanachotaka kusikia na siyo kuwaambia kilicho sahihi.

Huo ni mtego unaopaswa kuukwepa sana unapopokea ushauri wowote ule. Jiulize unapokea ushauri kwa sababu ndiyo wa msingi kwenye kufanya kazi au kwa sababu ndivyo unavyotaka kusikia?

Kwenye barua hii tunaenda kuangalia ushauri wa msingi kabisa kwenye maeneo muhimu ya maisha yetu. Ushauri ambao umenyooka na unaofanya kazi, iwe unapenda kusikia au hupendi. Huo ndiyo ushauri wa kufanyia kazi, hata kama huupendi, kwa sababu unachotaka ni matokeo.

1. Ushauri Sahihi Wa Muda Ni Hapana (Vipaumbele).

Chet Holmes kwenye kitabu chake cha The Ultimate Sales Machine anasema alikuwa ametingwa na majukumu mengi na hana muda kabisa. Akaamua kujiunga kwenye darasa la kusimamia vizuri muda. Siku ya kwanza ya darasa, mkufunzi akawapa zoezi la kwenda kufuatilia matumizi ya muda wao kwa wiki tatu. Waandike kila wanachofanya kwenye kila muda na kuja kuripoti. Chet anasema baada ya kuondoka hakurudi tena, kwa sababu kama angekuwa na muda wa kufuatilia muda wake kwa wiki tatu, asingekuwa na uhitaji wa kujiunga na darasa hilo.

Leo hii ukiingia mtandaoni na kutafuta kuhusu ushauri wa kusimamia muda na kuongeza uzalishaji na ufanisi, utakutana na ushauri mwingi sana, tena ambao unakinzana. Kuna mbinu nyingi sana za kuokoa muda, ambazo mtu tu kuzifanyia kazi ni upotevu wa muda. Kuna mifumo na programu nyingi za kusimamia muda.

Pamoja na kelele zote hizo kuhusu muda, ushauri sahihi na ulionyooka kwenye muda ni rahisi sana. Na ni neno moja tu; HAPANA.

Ushauri sahihi kuhusu muda unahusisha mtu kuweka vipaumbele, ambavyo ni mambo machache na yenye tija kwenye kile unachofanya. Baada ya hapo unasema HAPANA kwa mengine yote ambayo hayapo kwenye vipaumbele hivyo.

Ushauri huo hauhitaji utumie gharama zozote kubwa ndiyo uweze kuutekeleza. Hauhitaji utenge muda wa kufuatilia ndiyo uweze kutekeleza. Ni wewe kuandika vipaumbele vyako kisha kufanya hivyo tu, vingine vyote ni HAPANA.

Pamoja na kujifunza hili hapa, bado utaendelea kuhangaika na njia nyingi za kuokoa muda, na kuishia kupoteza muda mwingi kwenye kufanya hivyo. Ukisema tu hapana, tayari unaokoa muda na ukiupeleka kwenye mambo machache, inaleta tija.

2. Ushauri Sahihi Wa Fedha (Bajeti) Ni Matumizi Yasizidi Kipato.

Eneo la fedha nalo ni la moto sana kwenye kuwepo kwa ushauri mwingi na unaopingana. Kuna mafunzo na ushauri mwingi kuhusu matumizi ya fedha na mtu apangilieje bajeti yake. Kuna ubishi mwingi wa matumizi yapi ni muhimu na yapi siyo muhimu.

Watu wanapenda kubishana kwenye mambo hayo ya fedha, wasijue kwamba mahitaji ya watu yanatofautiana. Ambacho ni muhimu kwa mmoja, kinaweza kuwa anasa kwa mwingine.

Tofauti hizo za hali na uhitaji wa kifedha hazifanyi kusiwe na ushauri sahihi wa fedha, unaoweza kuwapa watu matokeo ya uhakika. Upo ushauri sahihi wa kifedha, ambao unaweka pembeni hizo tofauti ambazo watu wanazo kifedha.

Ushauri sahihi wa fedha ni kuhakikisha matumizi hayazidi kipato. Haijalishi nini muhimu au siyo muhimu kwako, unapaswa kuhakikisha matumizi yako hayazidi kipato unachoingiza.

Huo ndiyo ushauri unaofanya kazi mara zote na kwa watu wote, bila kuhitaji kubishana kipi ni muhimu na kipi siyo muhimu.

Hata kama utachagua kutumia fedha yako kwa starehe zozote unazotaka, kama matumizi hayajazidi mapato, uko vizuri. Na kama umejiambia una matumizi muhimu tu na huna anasa kabisa, lakini matumizi yanazidi kipato, uko vibaya.

Uzuri wa ushauri huu unafanya kazi sehemu zote mbili, ya kwanza ni kupunguza matumizi ili yasizidi kipato. Na ya pili ni kuongeza kipato ili kiweze kukidhi matumizi.

Washauri na waelimishaji wa fedha (Certified Financial Educators – CFE) tumekuwa tunalalamikiwa kuwafundisha watu wajitese kifedha ili waweze kuweka akiba na uwekezaji. Hiyo ni kwa sababu mafunzo ya wengi yameegemea eneo la kubana matumizi na kuweka akiba.

Lakini kwa ushauri huu ulionyooka kuhusu fedha, haukufungi upande mmoja. Kama hutaji kujitesa kubana matumizi, hakuna tatizo, pambana uongeze kipato chako. Kwa njia hiyo, utakuwa na maisha unayoyataka, huku pia ukiwa vizuri kifedha.

Kwenye #BaruaYaKocha unakwenda kujifunza aina nyingine tatu za ushauri sahihi na ulionyooka, ambao ukifanyia kazi utapata mafanikio kwa uhakika. Hapa umepata ushauri wa sehemu mbili, muda na fedha. Kwenye barua kuna ushauri wa ulaji (dayati), ufanyaji kazi (tija) na kujitoa kikamilifu kwenye mafanikio (umajinuni). Hayo ni maeneo muhimu sana kufanyia kazi kama unataka mafanikio makubwa.

Soma barua hiyo hapa; #BZK050; Ushauri Unaofanya Kazi Umenyooka, Na Usiofanya Kazi Ni Mwingi Na Unapoteza.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.