Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Wengi wanashindwa kwenye maisha siyo kwa sababu ya kutokujua cha kufanya, bali kwa sababu ya kutokufanya kile wanachopaswa kufanya ili wafanikiwe. Na wanashindwa kufanya siyo kwa makusudi, bali kwa nia njema kabisa, ya kusogeza mbele kile wanachopaswa kufanya.
Mtu anakuwa anajua kabisa kile anachopaswa kufanya na anapanga jinsi atakavyokifanya, lakini muda wa kutekeleza anaweka wa mbele zaidi. Kitu ambacho kingeweza kufanyika leo kinapelekwa kesho na ambacho kingeweza kufanyika sasa kinapelekwa baadaye.
Tatizo haliwi kwenye muda wa mbele unaowekwa, bali tatizo ni pale muda huo unapofika, unaendelea kusogezwa mbele zaidi. Kesho inapofika inahamishiwa kwenye kesho nyingine. Na baadaye inapofika pia inapelekwa kwenye baadaye nyingine.
Kwa kifupi ni kwamba, kunapokuwa na kitu kinachopaswa kufanya, lakini ukashindwa kuanza kukifanya mara moja, ni nadra sana ukaweza kuja kuanza kukifanya baadaye kama unavyokuwa umepanga. Kama kitu ni muhimu kweli na ni lazima kifanyike, hakuna sababu yoyote ya kukipeleka muda wa mbele.
Kwenye barua hii tunaenda kuangalia jinsi tunavyoweza kuanza mara moja mambo yote muhimu tunayopaswa kufanya ili kupata mafanikio makubwa tunayoyataka. Tukishaweza tu kuanza mara moja yale tunayopaswa kufanya, tunakuwa hatua ya mbele zaidi kwenye utekelezaji wa mambo muhimu na kujiweka kwenye nafasi ya kufanya makubwa.

1. Kama Kitu Lazima Kifanyike, Haina Haja Ya Kukisubirisha.
John von Neumann aliyekuwa mwanahisabati mashuhuri, wakati wa mvutano wa vita baridi kati ya taifa la Marekani na Urusi alinukuliwa akisema; “Kama unasema kwa nini tusiwashambulie kwa mabomu kesho, mimi nasema kwa nini isiwe leo? Kama utasema leo saa kumi na moja jioni, mimi nasema kwa nini isiwe saa saba mchana?”
Kauli hii imetoa muhtasari muhimu sana kuhusu muda muafaka wa kufanya jambo ambalo ni lazima lifanyike. Kama kuna jambo muhimu na ambalo lazima lifanyike, hakuna sababu yoyote ya kusubirisha jambo hilo. Linapaswa kufanywa haraka iwezekanavyo, kwa sababu kuendelea kulisubirisha siyo tu kuchelewa, bali pia ni kujiweka kwenye hatari ya kutokulifanya kabisa.
Mambo yote unayopanga kufanya kwenye safari yako ya mafanikio ni mambo muhimu na ambayo yana mchango kwenye matokeo unayotaka. Utapata matokeo hayo kama tu utafanya mambo hayo. Kujisubirisha na usianze kufanya mara moja ni kujikwamisha kupata matokeo unayotaka.
Hata pale unapokuwa na machaguo mengi ya mambo ya kufanya, usikubali kupoteza muda mwingi kuchambua nini ufanye na nini usifanye. Badala yake chagua kimoja na anza kufanya na kadiri unavyopata matokeo, tathmini na boresha au badili unachofanya.
Matokeo unayopata yanategemea uharaka wako wa kuchukua hatua kwenye mipango unayoweka. Mipango mizuri bila ya utekelezaji haina tofauti na kutokuwa na mipango kabisa. Anza kutekeleza mara moja yale yote unayopanga na utaona jinsi mwenendo wako utabadilika kwa haraka.
2. Ifanye Kesho Kuwa Leo.
Hakuna kitu rahisi kama kusema nitafanya kesho. Na hakuna kitu kigumu kama kutekeleza ahadi hiyo ya kufanya kesho. Kwa sababu kila kesho ina kesho yake. Na leo ni kesho ya jana.
Kitu chochote ambacho unajua unapaswa kufanya, lakini ukajiambia utafanya kesho, maana yake unakuwa umejiambia kitu hicho siyo muhimu zaidi na kinaweza kusubiri. Ukishakipa kitu hadhi ya kwamba siyo muhimu zaidi, hakuna namna utakipa kipaumbele sahihi kwenye kukifanya.
Ndiyo maana utaendelea kusema kesho, mpaka pale unapolazimika kufanya kwa sababu hakuna tena kesho nyingine. Ndiyo maana unakuta watu wengi wakichukua hatua kwenye jambo, pale inapokuwa ndiyo siku ya mwisho ya kuchukua hatua.
Huwezi kujenga mafanikio makubwa kwa kutekeleza mambo pale yanapokuwa yamefikia muda wa mwisho wa kuyatekeleza. Hutayafanya kwa viwango vilivyo bora na hivyo kujikwamisha kupata matokeo mazuri.
Kila unapofikiria kusema utafanya kitu kesho, jiulize kwa nini usikifanye leo. Jiulize kama ni kitu ambacho lazima ukifanye na pia jiulize kina umuhimu kiasi gani. Kuliko ujidanganye utafanya kitu kesho, wakati unajua siyo lazima ukifanye na hakina uharaka wa kufanya, ni bora tu ujiambie ukweli kama hicho siyo kitu muhimu kwako kufanya.
Kama haupo tayari kufanya leo, jiambie hutaki kufanya kabisa kitu hicho. Kisha tathmini ni kwa namna gani hilo litaathiri matokeo unayotaka kufanya. Kama kutokufanya hakuna athari, unakuwa umeokoa muda wako. Lakini kama kutokufanya kunaathiri matokeo unayotaka, unapaswa kufanya leo na siyo kupeleka kesho kama ambavyo umekuwa unafanya.
Siyo mara zote kusema utafanya kesho ni kubaya. Wakati mwingine ni ishara sahihi ya nini ambacho ni muhimu na siyo muhimu kwenye ufanyaji. Kitu kikishakuwa muhimu, hakipaswi kusubiri kwa muda mrefu kwenye kufanywa kwake.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK084; Kwa Nini Kesho Isiwe Leo, Kwa Nini Baadaye Isiwe Sasa?