Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Mambo mengi tunayokazana kufanya kwenye maisha yetu, huwa yanaishia kuwa na matokeo ambayo ni kinyume na matarajio tuliyokuwa nayo. Na hiyo ni kwa sababu huwa tunapenda kufanya mambo ambayo ni rahisi, badala ya mambo ambayo ni sahihi.

Sheria moja ya maisha ambayo watu wengi huwa hawaizingatii sana ni hii; Rahisi Siyo Sahihi. Vitu ambavyo ni rahisi kufanya, huwa siyo vitu sahihi kufanya. Unaweza kuthibitisha hilo kwa kuyatafakari maisha yako. Angalia nyakati zote ambazo ulichagua kufanya vitu rahisi na kukwepa vigumu, uliishia kupata matokeo ambayo siyo uliyotaka.

Kuna mambo mengi ambayo tunayafanya kwenye maisha yetu, ambayo tunajua kabisa siyo sahihi, lakini ndiyo yanakuwa rahisi kufanya. Na hili lipo sana pale tunapojihusisha na watu wengine. Kuna mambo ambayo tunayafanya kwa ajili ya watu, ambayo tunajua hayana msaada kwao, wala kwetu, lakini tunayafanya ili tu kukwepa lawama.

Tumekuwa tunaendesha maisha yetu kwa kufanya mambo ambayo tunajua kabisa hatutaki kuyafanya, lakini tunayafanya kuwafurahisha na kuwaridhisha wengine. Na watu wameshajua jinsi ya kuwabana wengine wafanye mambo wanayotaka. Wanatumia jina la roho mbaya.

Ukiangalia sana watu wanaoitwa wana roho mbaya, siyo kwa sababu wamefanya mambo mabaya, bali tu wamekataa kufanya mambo ambayo wengine wanawataka wafanye na hayana tija kufanya. Sikatai kuna watu ambao ni waovu na wanafanya mambo mabaya, lakini hao wanaitwa moja kwa moja ni wahalifu.

Wale wanaoitwa wenye roho mbaya, wengi sana ni watu waliochagua kuyaishi maisha yao kwa masharti yao wenyewe. Wanafanya kilicho sahihi mara zote, hata kama ni kigumu na hata kama hakuna mwingine anayefanya.

Wanaowasema wengine wana roho mbaya wanakuwa na sababu mbili. Moja ni kukosa kile ambacho walikuwa wanakitaka kutoka kwa mtu. Na mbili ni wao kutamani kufanya hivyo lakini kushindwa, kwa kukosa ujasiri wa kusimamia kilicho sahihi.

Kwenye barua hii tunakwenda kujifunza jinsi tunavyoweza kuwasaidia watu kwa kuwa na roho mbaya. Na hii siyo kuwatesa au kuwaumiza watu, bali kuishi kwa uhalisia na kwa kanuni ambazo zinawapa watu funzo sahihi bila kuwaonea huruma. Tunaona jinsi ambavyo hii ndiyo njia sahihi ya kuishi maisha yako na kujihusisha na watu walio sahihi kwako.

1. Huruma Siyo Malezi

Hii ni kauli ambayo ni maarufu, lakini umaarufu wake umekuwa kwenye maneno tu na siyo vitendo. Huwa ni rahisi sana kukosoa aina ya ulezi ya watu wengine, kwa kuwaona wanawadekeza wale wanaowalea, iwe ni watoto, wanafunzi, wafanyakazi au wafuasi.

Walezi wa sasa tunakwama sana kwenye kutoa malezi mazuri kwa sababu ya kutafuta kupendwa badala ya kuheshimiwa. Tunataka wale tunaowalea watupende na hivyo tunakazana kufanya vitu ambavyo vitawafurahisha. Hapo ndipo matatizo yote ya malezi yanapoanzia.

Tunapaswa kuelewa kwamba, tunapopewa nafasi ya malezi, tunapaswa kuwaongoza wale tunaowalea, ambao peke yao hawawezi. Tunapofanya mambo ambayo yatawafurahisha, ni kama wao wanatuongoza sisi jinsi ya kuwalea. Kwa maana nyingine ni kama wanajilea wao wenyewe. Sasa kwa mtu ambaye anahitaji malezi kujilea mwenyewe, ni lazima apotee.

Huwasaidii watu kwa kuwaonea huruma, unawasaidia kwa kuwapa mwongozo sahihi, hata kama siyo kitu wanachofurahia. Dunia ina kanuni zake, mtu hawezi kuruka juu kama ndege na asianguke chini. Mtu hawezi kugusa moto na asiungue.

Tunapopewa nafasi ya malezi, tuitumie kutoa malezi ya kweli, ambayo ni mwongozo sahihi kwa wale tunaowalea. Tusifanye mambo kuwaridhisha wale tunaowalea, au kuwaonea huruma. Dunia haina huruma, huwa inaenda kwa kanuni zake za asili, lazima malezi yetu yaonyeshe hilo.

Hii haimaanishi tuwatese na kuwaumiza watu ili tu tusionekane tuna huruma. Inachomaanisha ni kufanya kile ambacho ni sahihi na kina manufaa kwa tunaowalea. Cha kutuongoza ni usahihi na manufaa ya kila tunachofanya, ili kuwaongoza vyema wale tunaowalea.

Ukifanya vitu ili upendwe, unaishia kudharauliwa, kwa sababu hakuna utakachokuwa unasimamia. Lakini ukifanya vitu vilivyo sahihi, unaweza usipendwe, lakini utaheshimiwa. Na heshima inazaa upendo na manufaa zaidi kwa pande zote.

2. Toza Gharama

Kama kuna kitu ambacho kina gharama ambayo watu wanapaswa kulipa ili kukipata, na kukawa na watu ambao wanakihitaji ila hawawezi kumudu gharama, unaweza kusukumwa kuwapa watu hao bila gharama. Utafanya hivyo kwa kuona unawasaidia, lakini unawaumiza zaidi na kupoteza thamani nzima inayokuwa kwenye kitu chenye gharama.

Kama mtu hawezi kumudu kitu, maana yake hajafika kwenye ngazi ya kuweza kutumia kitu hicho. Hivyo hata ukimpa kitu hicho bila gharama, bado hatakithamini. Hivyo tunapaswa kuepuka sana kuwaondolea watu gharama kwa kudhani tunawasaidia.

Tunapaswa kutoza gharama sahihi kwa kila mtu, kama njia ya kuwasaidia waone thamani ya kitu na hata kukitumia. Kadiri kitu kinavyopatikana kwa gharama, na hapa siyo tu ya fedha, bali muda, nguvu na rasilimali nyingine, ndivyo kinavyoheshimiwa.

Mifano mingi na mizuri kwenye hili ipo eneo la fedha. Mtu akipata fedha kwa urahisi, kama kushinda bahati nasibu, kupata urithi au fidia, huwa zinaisha haraka pia, kwa mambo yasiyo na tija. Lakini mtu akipata fedha kwa kufanya kazi ngumu, anaiheshimu na kuitumia vizuri, na hivyo kuleta tija.

Hivyo ndivyo unavyopaswa kufanya kwenye maeneo yote, usiwaepushe watu na gharama wanayopaswa kulipa ili kupata kitu. Unaweza kudhani unawasaidia, lakini unawanyima fursa ya kuthamini kitu na kukitumia kwa manufaa makubwa kwao.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK080; Wasaidie Watu Kwa Kuwa Na Roho Mbaya