Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Matatizo ni sehemu ya maisha. Na unapotaka mafanikio makubwa, ndivyo pia unavyokutana na matatizo makubwa. Kitu kimoja kuhusu matatizo ni huwa hayaondoki yenyewe mpaka yatatuliwe.
Hata uyakatae na kuyapuuza matatizo kiasi gani, yataendelea kuwepo na yataendelea kukusumbua mpaka utakapoyatatua. Kinachowakwamisha watu wengi kwenye mafanikio ni kutokuyakubali kwa haraka matatizo wanayokutana nayo. Hilo linawapelekea wajikwamishe kupata matokeo makubwa wanayokuwa wameyataka.
Kutatua matatizo kwa njia sahihi ni sehemu muhimu ya safari ya mafanikio. Kwa sababu mafanikio makubwa yanakuja na matatizo makubwa, ni muhimu kuyatambua na kuyatatua kwa haraka ili yasiwe kikwazo kwetu.
Kwenye barua hii tunakwenda kujifunza hatua tano za kuweza kutatua matatizo yoyote tunayokutana nayo kwenye safari yetu ya mafanikio. Kwa kujua na kufanyia kazi hatua hizo, kila tatizo linapata ufumbuzi na kutuwezesha kupiga hatua kubwa zaidi kuyaendea mafanikio makubwa tunayoyataka.

1. Tambua Chanzo Cha Tatizo
Watu wanapokutana na matatizo, wanachokiona ni dalili au matokeo ya tatizo husika. Kuhangaika na dalili au matokeo hayo hakuwezi kutatua tatizo, mpaka pale chanzo kitakapojulikana na kufanyiwa kazi.
Mfano mzuri ni pale mtu unaposikia maumivu, kama ya kichwa. Maumivu hayo siyo tatizo, bali ni dalili za tatizo linaloendelea. Ukinywa dawa za maumivu na yakatulia, hujatatua tatizo, bali umepunguza makali yake. Nguvu ya dawa ikiisha, maumivu yanarudi pale pale, kwa sababu tatizo linakuwa halijatatuliwa.
Hivyo ndivyo watu wengi wamekuwa wanayaendea maisha, wakihangaika na dalili za matatizo badala ya kujua chanzo halisi. Unachokiona kwenye tatizo siyo tatizo lenyewe, ni lazima uingie ndani na kujua chanzo hasa cha tatizo husika.
Huwa wanasema kujua chanzo cha tatizo ni nusu ya kulitatua tatizo hilo. Kauli hiyo ni ya kweli kabisa, kwa sababu huwezi kulitatua tatizo kama hujajua chanzo chake. Na ukishajua chanzo halisi, kutatua inakuwa rahisi.
Kwa mfano wa kichwa kuuma tuliouangalia hapa, unaweza kugundua chanzo cha maumivu hayo ni uchovu, au maambukizi yanayoendelea mwilini. Kwa chochote utakachojua kama chanzo, unakuwa na nafasi nzuri ya kutatua tatizo husika.
Njia ya kugundua chanzo cha tatizo ni kuuliza swali kwa nini. Unapoona dalili au matokeo ya tatizo, usikimbilie kutatua hayo. Bali jiulize kwanza kwa nini hayo yametokea. Majibu utakayopata endelea kuuliza kwa nini mpaka ufike kwenye kiini kabisa, ambapo hakuna tena majibu. Ukienda kwa maswali hayo ya kwa nini mara tano, utafika kwenye chanzo halisi cha tatizo.
Ukishafika kwenye chanzo halisi, ndipo sasa unaweza kuanza kutatua tatizo husika kwa njia ambayo italeta suluhisho la uhakika.
2. Tengeneza Suluhisho
Baada ya kujua chanzo halisi cha tatizo, hatua inayofuata ni kutengeneza suluhisho la tatizo hilo. Hii ni hatua muhimu ya kuja na mambo ya kufanya ili kuondoa tatizo lililopo.
Ili kutengeneza suluhisho litakalofanya kazi, unapaswa kuepuka kusukumwa na hisia. Mara nyingi, suluhisho la tatizo unalokuja nalo kwa haraka, hasa pale tatizo linapojitokeza huwa limesukumwa na hisia. Na mara nyingi vitu vinavyosukumwa na hisia huwa siyo sahihi.
Unapaswa kutuliza fikra zako na kuliangalia tatizo kwa mantiki. Unapaswa kuwa na njia mbadala za kulitatua tatizo, kisha kutathmini kila njia na kuona uwezo wake wa kulitatua tatizo.
Unaweza kutumia njia ya kuchambua faida na hasara za kila suluhisho unalofikiria na kisha kuchagua lile lenye faida nyingi kuliko hasara. Pia unaweza kuchambua kwa kuangalia uimara, udhaifu, hatari na fursa kwenye kila suluhisho unalokuja nalo. Lengo ni kuhakikisha umepata utulivu wa kufikiria kwa kina na kuchambua kila suluhisho ambalo umelipata.
Ukiwa umeshajua chanzo halisi cha tatizo, kuja na njia mbadala za kutatua chanzo hicho huwa siyo zoezi gumu. Ni kuhakikisha unapata muda tulivu wa kutafakari kwa kina na kupata majibu sahihi.
Wengi wamekuwa wanapotea kwenye hii hatua kwa kuiga suluhisho la watu wengine au la matatizo ya nyuma na matokeo yake ni kushindwa kutatua matatizo wanayokuwa nayo. Kila tatizo lina utofauti na upekee wake, hivyo suluhisho pia linapaswa kuwa la kipekee. Usipoteze muda kuiga suluhisho la wengine au la nyuma. Tengeneza suluhisho la tatizo linalokuwa mbele yako kwa muda huo.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK083; Tumia Hatua Hizi Tano Kutatua Tatizo Lolote Kwa Uhakika