Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Wakati naanza kwenye hii tasnia ya uandishi, ukufunzi na ukocha, nilijifunza kitu kimoja ambacho kilinishangaza sana. Awali nilikuwa nadhani watu wengi wanaogopa kushindwa na ndiyo maana hawachukui hatua zilizo wazi kabisa kwao kufanikiwa. Hicho ni kitu kinachoweza kueleweka, hasa ukizingatia ugumu wa safari yenyewe ya mafanikio.
Lakini nilichokuja kujifunza na kikanishangaza sana, ni jinsi ambavyo wengi hawafanikiwi, kwa sababu wanaogopa kufanikiwa. Sijui unanielewa hapo, siyo kuogopa kushindwa, bali kuogopa kufanikiwa. Na kinachowafanya wengi kuogopa kufanikiwa ni kuona wakishakuwa juu, watashambuliwa na wengine. Na hata wasiposhambuliwa, wana nafasi kubwa ya kuanguka na wakishaanguka hawawezi kurudi tena juu.
Ni vigumu kuamini, lakini ndivyo saikolojia yetu binadamu ilivyo. Mara nyingi tunakikataa kitu sisi wenyewe, kwa sababu tunaona tukikipata kitatupa wajibu mkubwa ambao hatuutaki. Na kwa kuwa mafanikio yanakuja na wajibu mkubwa, utajiri unakuja na changamoto zake na biashara kubwa inakuja na hatari kubwa, wengi wanaepuka hizo hatua.
Kama unavyonijua mimi rafiki yako, nimejipa wajibu wa kutafuta majibu ya mambo yote yanayotukwamisha kupata mafanikio makubwa tunayoyataka. Na ili upate majibu, lazima ujue tatizo hasa ni nini. Maana wengi tunakwama kwenye majibu kwa sababu hatujui hata tatizo lenyewe.
Baada ya kuchunguza na kutafiti kwa kina, nimeona tatizo linalopelekea wengi kuogopa mafanikio ni kujiona hawajakamilika. Hilo ndiyo tutakalokwenda kuangalia jinsi ya kulitatua kwenye barua hii. Lakini kabla ya kuingia kwenye suluhisho, tulielewe vizuri kwanza tatizo lenyewe, ambalo chanzo ni kujiona ‘tapeli wa mafanikio.’

Tapeli Wa Mafanikio.
Kwenye mafanikio, kuna hali huwa inaitwa ‘imposter syndrome’ ambayo kwa Kiswahili rahisi tutaiita kujiona tapeli wa mafanikio. Kwa hali hii, mtu unajiona hustahili mafanikio unayokuwa umepata, kwa kuona kama ni bahati tu au kuna makosa yamefanyika. Hali hii inakuwa mbaya zaidi pale mtu anapoamini bahati itaisha au ukweli utakuja kujulikana na kuyapoteza mafanikio hayo.
Kila mtu amewahi kupitia hali hii, kwa viwango mbalimbali. Inaweza kuwa ni shuleni, ambapo ulipata ufaulu na ukasikia mtihani unaweza kurudiwa na ukahofia kwamba hutaweza tena kupata ufaulu kama huo. Au ni kwenye kazi ambapo umepandishwa cheo na kuhofia kuna siku wataona huna uwezo na kukuondoa kwenye nafasi hiyo.
Kwenye biashara ndiyo ipo zaidi, unakuwa umefanikiwa kufanya mauzo ambayo ni makubwa sana kuliko ulivyowahi kufanya, na kuhofia hutaweza tena kufanya mauzo kama hayo. Au mteja atabadilisha mawazo na kurudisha alichonunua.
Hali hii ipo hata kwenye mahusiano baina ya watu, unaona mtu au watu wamekukubali kwa sababu hawajakujua vizuri, wakikujua hawataendelea kuwa na wewe.
Ni kweli kuna watu ambao ni matapeli wa mafanikio, ambao wanaigiza na kulaghai kwenye mambo yao na kupata matokeo. Hao siyo tunaowazungumzia hapa. Hapa tunazungumza kuhusu wewe, ambaye umeweka juhudi kubwa sana na zikakupa matokeo, lakini bado ndani yako unaona kama hustahili matokeo hayo.
Hii ni hali ambayo imekuwa inamkuta kila mtu, hata unaowaona wamefanikiwa sana na wanajiamini, bado hizi fikra huwa haziwezi kufutika kabisa. Kinachowatofautisha watu ni kuweza kuitambua hali hiyo na kuhakikisha haiwakwamishi kufanikiwa zaidi.
Hicho ndiyo kitu ambacho nataka utoke nacho hapa rafiki, kwa sababu usipolielewa hili vizuri, kuna namna utaendelea kujihujumu wewe mwenyewe ili usifanikiwe zaidi. Kwa sababu kadiri unavyofanikiwa na watu wanavyokusifia, ndivyo unavyojiona ni tapeli na siku moja watu watajua utapeli wako na utaaibika sana.
Karibu sasa tujifunze jinsi ya kujenga ukamilifu utakaotupa kujiamini ili tuyapende mafanikio, tuyapate na tudumu nayo bila kuhofia au kukwamishwa na kitu chochote.
1. Hakuna Anayezaliwa Mkamilifu; Ukamilifu Hujengwa Kila Siku.
Sifa yetu moja sisi binadamu ni siyo wakamilifu. Wote tunazaliwa tukiwa hatuna ukamilifu. Mambo yote kuhusu maisha tunakuja kujifunza hapa duniani, tena kwa kipindi kirefu.
Ukituangalia binadamu na kulinganisha na viumbe wengine, sisi binadamu ndiyo tunazaliwa tukiwa na mapungufu mengi sana. Wanyama wa mwituni, anapozaliwa anachukua muda mfupi sana kuanza kukimbia, la sivyo hatapona. Lakini sisi binadamu inatuchukua muda mrefu sana mpaka kuweza kujitegemea kimaisha, kwa vitu vyepesi tu kama kula chakula.
Kukosa ukamilifu siyo udhaifu, ni hali yetu binadamu, wote tunazaliwa hivyo na wote tunaanzia mahali fulani kwenye chochote tunachokuwa tunafanya.
Lakini kubaki kwenye hali ya kukosa ukamilifu inakuwa ni chaguo letu. Iko ndani ya uwezo wetu kujifunza na kuwa bora kwenye mambo yote tunayofanya kwenye maisha yetu.
Wajibu wetu namba moja kwenye maisha unapaswa kuwa ni kujiboresha. Maisha yetu yanatakiwa kuwa na kibao kinachosema matengenezo yanaendelea. Kama ambavyo ukipita kwenye barabara inayotengeneza unaona kibao cha aina hiyo, ndivyo maisha yetu yanapaswa kuwa.
Kila tunapopiga hatua na kupata wasiwasi kwamba tumebahatisha au kupewa tu, iwe ukumbusho kwetu wa kuendelea kujiboresha ili tuwe na ushahidi wa kuondoa kabisa huo wasiwasi.
Hii inanikumbusha nukuu maarufu ya mwandishi Henry David Thoreau kwenye kitabu chake kinachoitwa Walden, ambayo inasema: “Ukijikuta umejenga hekalu hewani, kazi yako haipaswi kupotea; hapo ndipo inapaswa kuwa. Sasa jenga msingi chini yake.”
Kauli hiyo imebeba maana nzima ya tunachojadili hapa, kuna mafanikio utakayoyapata na kuona kama umebahatisha, licha ya kwamba kuna juhudi umeweka. Sasa kwa sababu hali hiyo huwezi kuifuta kabisa, itumie kujenga kile ambacho kitafanya mafanikio uliyopata yasipotee.
Kubali kwamba hujakamilika, lakini usiruhusu kutokukamilika kwako kupoteze mafanikio uliyopata. Badala yake unafanya kazi ya kujiboresha ili utunze mafanikio yoyote unayoyapata.
2. Noa Vipaji Vyako, Tabia Zako Na Akili Yako Bila Kuacha.
Abraham Lincoln amewahi kunukuliwa akisema; ‘Kama nina masaa sita ya kukata mti, nitatumia masaa manne ya kwanza kunoa shoka.’ Kauli hiyo inaweza kutafsiriwa kama uvivu, iweje mtu atumie muda mwingi kunoa kifaa kuliko kufanya kazi yenyewe. Lakini ipo dhahiri kwamba, kifaa kikali kinakamilisha kazi kwa haraka kuliko kifaa butu.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kujenga ukamilifu wa kukupa mafanikio yanayokuja na kujiamini na kudumu kwa muda mrefu. Mafanikio yanakuja na wasiwasi mkubwa pale yanapokuwa nje ya uwezo wako. Ili kuhakikisha mafanikio yanakuwa ndani ya uwezo wako, lazima unoe vitu hivi vitatu;
Cha kwanza ni vipaji vyako. Huu ni uwezo wa kipekee ulio ndani yako, unapounoa na ukawa umechangia kwenye mafanikio yako, utajiamini na kudumu na mafanikio hayo kwa muda mrefu. Kwa sababu yanakuwa yametokana na uwezo wa kipekee unaokuwa ndani yako.
Cha pili ni tabia zako. Unapokuwa na tabia zinazoendana na mafanikio unayopata, unaweza kuyaendeleza mafanikio hayo bila kuhofia kuanguka na kushindwa kurudi kwenye mafanikio hayo. Kitu kikishakuwa tabia kwako, unaweza kukifanya bila kutumia nguvu kubwa.
Cha tatu ni akili yako, ambayo inaona na kufanyia kazi fursa za kufanikiwa na kudumu kwenye mafanikio. Akili inapokuwa imenolewa, inakuwa na ukali wa kuziona fursa bora za kujenga na kudumu kwenye mafanikio makubwa. Akili bora inakupa kujiamini, kwamba hata ukipoteza mafanikio, unaweza kuyapata tena.
Kwa kunoa vitu hivyo vitatu, unajenga mafanikio na kujiamini. Kamwe huwezi kuona umebahatisha au kuwa na wasiwasi kwamba ukianguka hutaweza tena kuanguka.
Huwa kuna usemi kwamba ndege anapotua kwenye tawi la mti, siyo kwa sababu anaamini uimara wa tawi hilo, bali anaamini uwezo wake wa kuruka. Ili upate na kudumu kwenye mafanikio, hupaswi kuamini kwenye fursa iliyokufikisha kwenye mafanikio hayo, bali kwenye uwezo wako wa kutumia fursa nyingine nyingi na kupata mafanikio ya aina hiyo.
Noa vipaji, tabia na akili na utaweza kuyarudia mafanikio makubwa wakati wowote unaotaka. Na ukishayapata unaweza kuyatunza kwa muda mrefu.
Kwenye #BaruaYaKocha unakwenda kujifunza maeneo mengine matatu ya kujenga ukamilifu ili uweze kujijengea mafanikio makubwa na yanayoweza kudumu.
Soma barua hiyo hapa; #BZK051; Jinsi Ya Kuwa Mkamilifu Ili Ujenge Mafanikio Yasiyoangushwa Na Chochote.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.