Rafiki yangu Mpendwa
Kuna maeneo mengi ambayo ‘unazingua’, na watu wanajua unazingua, ila wewe unajiona uko sawa tu. Tatizo kubwa ni kwamba watu hawakuonyeshi kama wanajua unazingua. Wanaenda na wewe kama unavyowapeleka, lakini wanajua kabisa kwamba unazingua.
Wewe unawaona wanakuelewa, na kujisifia kwa hilo kwamba umeweza kuwasomesha watu mpaka wakakuelewa. Lakini ukweli ni hawajakuelewa kwa ulichowasomesha nacho, bali wamekuelewa kwa uhalisia wako na wamekuweka mahali tofauti na unavyodhani wewe.
Kuna mbinu ambazo umekuwa unazitumia kujitetea na kujieleza kwa watu. Watu wanakusikiliza na kuonekana kukubaliana na wewe. Unaona mbinu hizo zinafanya kazi. Lakini ukweli ni mbinu hazifanyi kazi, watu wanakupuuza tu.
Unaweza kusema kwa nini nayasema haya kwako, wakati wewe ni mtu makini na unayeheshimika na kukubalika na watu. Hilo nalo ni tatizo, kuheshimika na kukubalika na watu haimaanishi kwamba uko sahihi.
Nakuambia hili moja kwa moja kwa sababu najua unataka kufika mbali zaidi ya hapo ulipo sasa. Kwa sababu hapo ulipo sipo unapopaswa kuwepo. Lakini juhudi zako za kukutoa hapo ndiyo zimekuwa zinanitia mashaka. Kuna namna ungeweka juhudi kubwa zaidi ya unazoweka sasa, ungekuwa mbali zaidi ya hapo ulipo sasa.
Ambacho nimekuwa nachunguza ni kwa nini huweki juhudi za kutosha na bado unaridhika? Na ndiyo nimegundua ni kwa sababu unajidanganya na kufikiri wengine nao wanadanganyika kama wewe.
Kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kuweka wazi jinsi ambavyo umekuwa unajidanganya ili uache na upige hatua kubwa. Kwa sababu hakuna tena anayenunua uongo wako, kwa mahali ambapo umefika sasa.

1. Kulaumu Wengine.
Kama wazazi wangefanya hivi, basi ningekuwa mbali sana.
Kama serikali ingefanya vile, ningekuwa nimepiga hatua kubwa.
Kama isingekuwa kwa watoto ninaosomesha, ningekuwa na maendeleo zaidi ya hapa.
Kama, kama, kama ….
Ulipokuwa na miaka 20, watu waliziamini hizo kama zako.
Lakini miaka 30, 40, 50, duh, mpaka 60, wanakusikiliza tu. Lakini ndani yao wanajua kabisa kwamba umezingua na unaendelea kuzingua.
Lakini hawawezi kukuambia wazi wazi kwamba unazingua,
Kwa sababu ni kweli, wazazi wako hawakukusomesha,
Ni kweli, serikali imejaa wala rushwa na walioharibu fursa nyingi.
Na ni kweli kabisa, una watoto wanne na wote umewasomesha kwa gharama kubwa.
Watu watakuelewa kwa hizo sababu, lakini wanajua unazingua. Ni vile tu hawawezi kukuambia kwa sababu hawataki ujisikie vibaya, ukose cha kujifariji nacho.
Hasa ukiangalia kwamba kuna ambao hawakusomeshwa na wazazi wao na wako mbali kuliko wewe.
Kwenye serikali hiyo hiyo mbovu, kuna wenzako wamepiga hatua ambazo ni kubwa.
Na kuna wenzako wanasomesha watoto wengi kuliko wako, kwa shule za gharama kubwa kuliko ulizosomesha wewe, na bado wana maendeleo makubwa kuliko wewe.
Kama unataka kuendelea kujifariji na hizo sababu, huku miaka ikienda, endelea. Lakini jua tu wazi kwamba hakuna anayedanganyika tena.
Kama hujapata unachotaka, huna yeyote wa kumlaumu ila wewe mwenyewe. Na kama unataka watu wakuheshimu, acha kulaumu na anza kupambania unachotaka. Hata kama umri umeenda kiasi gani, wewe pambania unachotaka. Hilo lina afadhali kuliko kukaa na kulaumu vitu ambavyo wewe mwenyewe umezingua.
Kama unalaumu wazazi waliokaa na wewe mpaka unafika miaka 20, kwa nini usijilaumu wewe mwenyewe kwa kukaa na wewe kwa miaka zaidi ya hiyo na hujaweza kutoboa? Sijui unanielewa hapo?
2. Kutetea Tabia Zako Mbaya.
Umekubaliana na mtu mkutane saa mbili kamili asubuhi.
Wewe unafika saa tatu, na kusema foleni imekuwa kubwa na imekukwamisha.
Na ni kweli kabisa, umekutana na foleni na imekukwamisha.
Watu wanasema sana na mnaendelea.
Na wewe unaona umeeleweka, kwa sababu kila mtu anajua jinsi foleni ilivyo kali.
Lakini watu wanajua unazingua, kama ungewahi kutoka, ungefika mapema hata kama kungekuwa na foleni kali kiasi gani.
Kwa sababu maeneo ambayo lazima ufike kwa muda huwa unafika, licha ya foleni kuwepo.
Na hivi foleni ni jambo la dharura kweli?
Una tabia mbaya, ya kushindwa kusimamia muda wako vizuri, lakini unajitetea kwa foleni. Hujali muda wako, unaweza kuupoteza tu jinsi unavyotaka. Na sasa unataka kupoteza na muda wa wengine. Hakuna mtu makini atakayekubaliana na hilo. Ndiyo maana ikishakuwa tabia yako sugu ya kuchelewa, watu wanakunyima fursa ambazo zinataka watu ambao wako makini na muda.
Hilo la foleni ni mfano mmoja tu, lakini kila eneo la maisha una tabia ambazo umekuwa unazitetea kwa kutafuta visingizio vingine.
Unaingia kwenye madeni kwa kusema kipato hakitoshelezi, lakini una tabia ya matumizi mabaya, ambayo hiyo hutaki kuiangalia na kuirekebisha.
Umekuwa unadanganya watu, na wanajua kabisa kwamba unadanganya, lakini unaona ni sawa kwa sababu kila mtu anadanganya.
Tabia zako mbaya watu wanazijua na wanazitumia kuamua waendeje na wewe. Hakuna unayemdanganya kwa kuzitetea tabia hizo.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK102; Hakuna Mtu Anayedanganyika Tena Na Hizi Mbinu Zako