Rafiki yangu Mpendwa,

Nimeweza kudumu kwa muda mrefu kwenye tasnia hii ya uandishi, ukufunzi na ukocha kwa sababu ya ubishi mmoja ambao nimekuwa nao.

Ubishi huo, ambao mara nyingi umekuwa unaishia kunigharimu ni kuamini kila mtu anaweza na anapaswa kufanikiwa.

Kuhusu kila mtu kuweza kufanikiwa hilo halina shaka, inajulikana kabisa kila mtu ana uwezo mkubwa ndani yake, ambao akiutumia, ataweza kufanya makubwa kuliko anavyokuwa anafanya.

Kuhusu kupaswa kufanikiwa, hapo ndipo tatizo kubwa lilipo. Nimekuwa nikiamini kila mtu anapaswa kufanikiwa, kitu ambacho kwa asili hakipo.

Na hakipo kwa sababu watu wengi hawataki kufanikiwa. Hata wale wanaosema wanataka mafanikio, ukiwachimba ndani hasa, unagundua hawataki mafanikio kama wanavyotaka.

Badala yake wanatamani mafanikio, au wangefurahi kama wangeyapata mafanikio. Na hayo siyo sawa na kutaka kuyapata mafanikio.

Nimekuwa nikisema udhaifu mkubwa nilionao kwenye hiki ninachofanya ni kutaka mtu afanikiwe kuliko anavyotaka yeye mwenyewe. Na nilikuja kugundua udhaifu huo pale mtu mmoja aliponiambia dhahiri kwamba alichopata kimemtosha, kwa nini namsukuma zaidi?

Hapo ndipo macho yangu yalifunguka na kuona wazi kwamba kuna watu nawasumbua bure tu. Pale walipo tayari panawatosha, wakati mimi naona wanapaswa kwenda mbali zaidi.

Tangu hapo nimejifunza nani wa kumsukuma kwenda mbali zaidi na nani wa kutokumsukuma kwa sababu alipo panamtosha.

Na hilo halimaanishi mtu asiyetaka kwenda mbali zaidi simthamini, hapana, nampenda na kumthamini kila mtu. Lakini inapokuja kwenye kutoa rasilimali zangu, naangalia kitu kimoja; ‘usiriazi’.

Kuna nukuu moja nimekutana nayo siku za karibuni, ambayo imenisaidia sana kwenye huo mpango ambao nimekuwa nautekeleza. Kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukushirikisha nukuu hiyo na jinsi ya kujikagua kama upo siriazi au la.

1. “Nawapenda, lakini hampo siriazi.”

Nimekutana na hiyo nukuu, ambayo mwandishi anaeleza imetoka kwenye tamthilia inayoitwa Succession. Tamthilia hiyo inahusu mzazi tajiri ambaye anatamani watoto wake ambao tayari ni watu wazima waweze kuendeleza utajiri aliojenga.

Anawapa dili moja kubwa ambayo wanapaswa waikamilishe, ambayo itakuwa na manufaa kwao. Lakini kwa makusudi, watoto wake wanafanya uzembe ili kuipoteza dili hiyo. Wanafanya hivyo kama kulipa kisasi kwa baba yao, ambaye kwa kipindi kirefu cha maisha yao tangu wakiwa wadogo walikuwa hawapati muda wake, kwa sababu alikuwa anapambana kujenga utajiri.

Kwa ukubwa wa dili hiyo, baba anaamua kujishusha na kuwaomba radhi kwa hayo aliyoyafanya na kuwataka wawa watu wazima na wasonge mbele. Pamoja na baba kujishusha kiasi hicho, bado watoto hao wanabaki na msimamo wao.

Hapo ndipo baba alipoona hana namna ya kuwabembeleza tena na akajikuta akisema kwa ukali; “Yesu …. ninyi ni watu wajinga sana. Ninyi siyo watu makini. Nawapenda, lakini hampo siriazi.”

Niliposoma hiyo nukuu, ilinisukuma sana na kunifanya nianze kuangalia ni maeneo gani ambayo kuwapenda watu kumekwamisha kupata matokeo ambayo yalipaswa kufanyika.

Na hapo ndipo nikaona jinsi ambavyo upendo na heshima kwa watu na usiriazi wa watu ni vitu ambavyo vinapaswa kutenganishwa mapema sana. Bila hivyo kila upande utaumia, upande unaotaka matokeo hautayapata na upande usiotaka matokeo utaona unasumbuliwa.

Je wewe unajiona ukiwa upande ambao ni siriazi? Endelea kusoma barua hii uone uko upande gani.

2. Je, Unajua Kufanya Hicho Unachofanya?

Kocha John Wooden alipopewa timu ambayo ilikuwa haifanyi vizuri, watu walitegemea atafanya mambo mapya na ya kimuujiza. Badala yake yeye alianza kuifundisha timu hiyo vitu vya msingi kabisa. Alifundisha vitu kama jinsi ya kuvaa soksi, kufunga viatu kwa usahihi, kupiga mpira kwa usahihi n.k.

Wengi walishangazwa na hilo, kwa kuona ni vitu ambavyo tayari kila mchezaji anavijua. Ni mpaka timu ilipoanza kupata ushindi ambao ilikuwa haipati huko nyuma ndiyo watu walielewa nguvu ya kufanya kwa usahihi vitu vidogo vidogo.

Eneo lolote ambalo hupati matokeo, unaweza kuhangaika na vitu vikubwa sana, ambavyo kila wakati unashindwa kuvitekeleza. Lakini kuna vitu vidogo vidogo ambavyo unavifanya mara kwa mara, na hujui kuvifanya kwa usahihi.

Tukianza na mafanikio binafsi, umekuwa unakula chakula kila siku, je umewahi kujifunza jinsi ya kula kwa usahihi? Jinsi ya kula ambayo haitakuwa kikwazo kwako kwenye mambo unayofanya? Vipi kuhusu kulala na kuamka? Si unafanya kila siku, je umeshajifunza jinsi ya kufanya kwa usahihi ili ulale na kuamka ukiwa na nguvu ya kutekeleza mambo uliyopanga? Sasa kama vitu vya msingi kama hivyo, ambavyo unavifanya kila siku unafanya kwa kubahatisha, vipi makubwa unayohangaika nayo?

Kwenye eneo la fedha, tangu umekuwa mtu mzima umekuwa unashika fedha mara kwa mara kama siyo kila siku. Umekuwa unahangaika uongeze kipato chako, uweke akiba, ufanye uwekezaji na mengine. Lakini je umewahi kujifunza namna ya kufanya hayo kwa usahihi? Achana na kusoma kitabu au kuhudhuria mafunzo ambayo yanakupa maarifa. Hapa tunaongelea kujenga ujuzi wa kufanya kila kitu kwa usahihi. Je unaona unao ujuzi wa kutendea kwa usahihi eneo lako la fedha?

Kwenye biashara ndiyo kabisa nikigusa utalia, kwa sababu unaweza kuwa unalalamika hakuna wateja kwenye biashara yako. Swali ni je umewahi kujua kwa kina jinsi ya kupata wateja wa biashara yako? Achana na majibu mepesi kama tangaza, posti kwenye mitandao n.k. Unajua hasa wateja wa biashara yako, wapi wanapatikana na unawafikiaje kwa uhakika? Vipi kuhusu mauzo, je unayo skripti ya mauzo ambayo watu wote wa mauzo wanaifuata? Au unalalamika tu kwamba wateja wanatoa ahadi hewa?

Rafiki, kama uko siriazi, umeelewa nini nazungumzia hapa. Kinachokukwamisha usipate matokeo makubwa unayotaka, siyo mambo makubwa unayohangaika nayo. Ni mambo madogo madogo na ya msingi ambayo umekuwa unayafanya kila mara, lakini hujui jinsi ya kuyafanya kwa usahihi.

Kuwa siriazi ni kujua kwa usahihi kila unachokifanya, kwa sababu ndiyo njia ya kupata matokeo makubwa unayoyataka.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK101; Nawapenda, Lakini Hampo Siriazi.