Rafiki yangu Mpendwa

Mambo mengi ninayokuambia kwenye hizi #BaruaZaKocha ni mambo ambayo huwa siwaambii watu waziwazi. Kwa sababu nikiwaambia kama ninavyoyasema hapa, watanichukia sana.

Na siyo kwamba naogopa kuchukiwa, hilo halina tofauti yoyote kwangu. Nisichotaka ni kuanza kujieleza eleza kwa watu ambao hata hawawezi kuelewa. Muda wangu ni wa thamani sana kuutumia kuwaelewesha watu vitu ambavyo viko wazi kabisa.

Kuna siku mtu alikuwa ananiambia habari kubwa iliyokuwa inaendelea mtandaoni, habari ya mtu aliyekusanya pesa za watu wengi na kupotea nazo. Watu wakawa wanalalamika jinsi walivyomwamini na kumpa pesa lakini amewatapeli.

Haraka sana nilijikuta najibu; “Safi sana, huyo mtu ana akili sana.” Niliyemjibu hivyo aliniangalia kana kwamba mimi ni mtu mwenye roho mbaya sana na nisiyejali matatizo ambayo wengine wamepitia.

Sikuwa natania kwa jibu hilo, nilikuwa namaanisha kabisa. Hebu fikiria tu, mtu anatuma pesa zake kwa mtu ambaye hata hajawahi kukutana naye, amemwona mtandaoni tu na kumwamini. Hapo nani wa kulaumiwa?

Nikifikiria jinsi ambavyo tunatumia nguvu nyingi kuwapa watu elimu ya fedha, na majibu ya kejeli ambayo wengi huwa wanayatoa, nikisikia mtu katapeliwa fedha huwa nafurahi sana. Sifurahi kwa sababu nina roho ngumu ya kutokujali, nafurahi kwa sababu inazidi kuonyesha jinsi ambavyo elimu tunayoitoa ni muhimu.

Hebu fikiria, hata kama ingekuwa ni wewe, unamfundisha mtu kuhusu elimu ya msingi tu kuhusu fedha, ambayo hajawahi kuipata kokote. Halafu jibu lake linakuwa; “Mambo ya pesa wanatakiwa wafundishe matajiri wakubwa kama Mo na Bakhresa, nyie ni njaa tu hamna lolote.” Halafu unakutana na mtu huyo huyo analalamika ametapeliwa. Kuna namna tu utasema safi sana.

Sawa, mimi niko na wewe, ndiyo maana sitaki upoteze kizembe. Na kuna watu umekuwa unawaamini sana, tena kwa haraka na ndiyo wamekuwa wanakukwamisha. Kwa sababu kazi yangu ni wewe, leo nataka nikuonyeshe hao watu ili uweze kuwaepuka na kuwazuia wasikukwamishe.

Kwenye hii #BaruaYaKocha tutazama kwa undani zaidi, kufunua ngozi za kondoo ambazo watu wamejivika wakati ndani ni mbwa mwitu. Baada ya barua hii ukikwamishwa ni wewe tu utakuwa umetaka.

1. Watu Ambao Ukiwapa Nafasi Ya Kuwasililiza Hasira Zote Zinaisha.

Kuna watu ambao wanakukwaza sana, kiasi cha kukasirika. Unakuwa umejipanga kuwakabili na kuwaeleza jinsi ambavyo wamekukwaza, kwa kushindwa kutimiza kile ulichotegemea.

Lakini unapowapa watu hao nafasi ya kujieleza, hasira zote zinaisha na unajikuta ukiwaonea huruma. Tena unajikuta unaingia gharama zaidi kuwasaidia kwa yale ambayo wamekueleza.

Unaweza kudhani watu hao wanamaanisha wanayosema, lakini ndiyo michezo yao. Na kama utachelewa kuwajua, watakukwamisha sana.

Tatizo linakuja pale unapowaamini watu hao na kuendelea kushirikiana nao, huku ukiwategemea kwa mambo ambayo hawawezi kuyafanya.

Wanachokuwa wanaweza ni kujieleza kwa hisia na kunasa hisia zako. Unapaswa uwatambue watu hao haraka sana na kuacha kuwategemea.

Na hawa wala huhitaji kugombana nao, kama mtu amekukwaza, kwa kushindwa kutimiza kitu ambacho ulikuwa unakitegemea sana. Lakini ukimpa sababu ya kujieleza unajikuta umesahau jinsi alivyokukwaza, shtuka haraka sana. Huo ni mchezo wake na usiendelee kumwamini.

Unaweza kumwelewa kwa maelezo yake, lakini mwondoe kwenye watu ambao unawategemea kwenye matokeo unayotaka kupata. Hiyo ndiyo njia pekee ya kutokukwama kwenye matokeo unayotaka.

Watu ambao ni wazuri sana kwenye kujieleza, ambao hata uwe umejipanga kiasi gani watapata tu njia ya kukushawishi, siyo watendaji. Kwa bahati mbaya sana huwa wanaaminika kwa maneno yao na hisia kali wanazoibua wakati wa kujieleza.

Salama yako ni kuwatambua haraka na kuwaondoa kwenye watu unaowategemea. Shirikiana nao kwenye mambo mengine, lakini kwenye yale unayotaka kupata matokeo, epuka kabisa.

2. Watu Ambao Wanatumia Majina Ya Watu Wakubwa Wanaojuana Nao.

Hakuna mtu asiyependa kuwa karibu na watu wenye mamlaka na madaraka makubwa. Iwe ni ya kifedha, vyeo au wadhifa, watu wenye mamlaka makubwa wanaweza kurahisisha mambo mengi ambayo watu wanafanya.

Kuna watu wanajua jinsi ya kucheza na hilo hitaji la watu, wanakuwa ni watu wa kawaida, ila wana ukaribu na watu hao wakubwa. Na kwa ukaribu huo wanaokuwa nao, wanautumia kuwaaminisha watu vitu ambavyo siyo sahihi.

Watu hao huwaaminisha watu kwamba watawaunganisha na watu hao wakubwa, au jambo lao wamelipeleka kwa hao wakubwa. Watu wanakuwa na imani kwamba watapata suluhisho la kile wanachohangaika nacho. Lakini kwa bahati mbaya sana, hao wakubwa wanakuwa hata hawajapewa taarifa hizo.

Watambue kwa haraka sana watu wanaokushawishi kwa kutumia majina ya watu wakubwa ambao unatamani sana kuwafikia. Watu hao wanaweza kukudanganya na kukuaminisha vitu ambavyo havipo kabisa.

Na wewe mwenyewe unajua hili, umeshapita kwa wengi ili uwafikie watu wakubwa unaotaka kuwafikia, na umeishia kuzungushwa tu.

Kama mtu anataka umwamini atakuunganisha na mtu mkubwa unayetaka kumfikia, afanye hivyo moja kwa moja. Atengeneze mkutano ambao atakukutanisha moja kwa moja na yule unayetaka kumfikia.

Kama mtu anakuambia atafikisha jambo lako kwa mkubwa, usiamini. Hata kama hutamwambia huamini, wewe usiamini. Mwambie akufikishe kwa huyo mkubwa, ambacho ni kitu rahisi kama kweli ana ushawishi kwa huyo mkubwa. Kama ameshindwa kukufikisha moja kwa moja, chochote anachokuambia ni cha kukufurahisha tu.

Hili ni muhimu hata kwenye mambo ya kawaida kama mauzo. Unauza kitu kwa mtu, anakuambia ataenda kuongea na mhusika, na wewe unakubali. Umepotezwa hapo, wa kuongea na mhusika ni wewe na siyo mtu mwingine yeyote.

Kama unataka matokeo, hakikisha unamfikia mtu ambaye unataka kumfikia, kwa njia zozote utakazoweza kutumia kumfikia. Na hakikisha ni wewe mwenyewe umemwambia mtu huyo ni nini unachotaka kwake na yeye akijibu kama anaweza kukusaidia au la.

Usikubali maneno yoyote ya mtu wa kati ambaye anakuambia anashughulikia jambo lako na kulifikisha kwa wahusika. Hayupo wa kufikisha jambo lako kwa wahusika kwa usahihi kama ambavyo utafanya wewe.

Na kama kwa juhudi zako umeshindwa kumfikia mhusika, kwa nini uamini mwingine anaweza kumfikia kwa niaba yako? Kama kweli mtu anaweza kumfikia mtu kwa niaba yako, anaweza pia kukufikisha kwa mtu huyo moja kwa moja.

Acha kuamini watu ambao wanatumia majina makubwa kukuaminisha vitu ambavyo havipo, unajikwamisha mwenyewe kwa kufanya hivyo.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK103; Hawa Watu Unaowaamini Sana Ndiyo Wanaokukwamisha Kufanikiwa