Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Tunaposoma historia yetu binadamu, tunaona jinsi ambavyo tumepitia zama mbalimbali hapa duniani. Kwa kipindi kirefu binadamu tumekuwepo hapa duniani, mamilioni ya miaka. Lakini kwa sehemu kubwa sana ya muda huo hatukuweza kupiga hatua kubwa.
Ni ndani ya kama miaka elfu 5 iliyopita ndiyo binadamu tumeweza kufanya mambo makubwa na kuibadili kabisa dunia. Hilo limetokea siyo kwa sababu binadamu wa zama hizi tumekuwa na uwezo mkubwa kuliko wa kipindi cha nyuma, bali kwa sababu tumeweza kufanya vitu ambavyo huko nyuma havikufanywa.
Kitu kikubwa kilichotufanya binadamu kuweza kuibadili dunia ni uwezo wa kujenga vitu. Ni asili yetu binadamu kujenga, na hicho ndiyo kinachotutofautisha na viumbe wengine. Wanyama wengine, hata ambao tunakaribia kufanana nao, huwa wanaishi kwenye mazingira waliyoyakuta bila kuyabadili. Ni sisi binadamu pekee ndiyo tumekuwa tunayabadili kabisa mazingira yetu na kuwa vile tunavyotaka sisi.
Kwa zama za karibuni, binadamu tumeweza kufanya makubwa zaidi kwa sababu tumeweza kujenga kwa ukubwa zaidi. Uwezo wa kujenga kwa ukubwa umetokana na kuweza kugundua na kutengeneza zana zilizotumika kwenye ujenzi.

Ugunduzi wa moto na chuma ndiyo zana na teknolojia ambazo zimeleta mapinduzi makubwa sana hapa duniani. Ndiyo zana kuu mbili ambazo zimeweza kujenga kila kitu tunachokiona leo. Moto ndiyo umekuwa chanzo cha nishati kwenye kila shughuli tunayofanya. Kuanzia kupika mpaka kuendesha injini, moto umekuwa na mchango mkubwa.
Na chuma ndiyo mhimili wa kila kitu kinachojengwa na binadamu. Kuanzia nyumba, injini na vifaa vingine vyote, chuma inahusika kwa kiasi kikubwa.
Maendeleo na hatua zote ambazo binadamu tumepiga ni kutokana na kutumia rasilimali na zana kujenga. Hakuna chochote ambacho kimewahi kutokea bila watu kujenga.
Kwa historia yetu binadamu, maendeleo yamekuwa yanaenda mbele na siyo kurudi nyuma. Kila wakati vitu vipya vimekuwa vinakuwa bora kuliko vya nyuma, kwa sababu ya hali yetu ya kujenga.
Lakini sasa tupo kwenye zama za tofauti, zama ambazo teknolojia mpya zinatishia kuondoa hali ya maendeleo endelevu. Hiyo inatokana na teknolojia hizo kuondoa ile hali yetu ya binadamu kuwa wajenzi. Teknolojia zinatufanya tubweteke na kuona tunaweza kupata maendeleo na mafanikio bila kujenga.
Hii ndiyo hatari ambayo imeanza kuwaathiri wengi na kuwazuia kupata mafanikio wanayoyataka, bila wao kujua ni nini hasa kinachowakwamisha. Kwenye barua hii tunaenda kuangalia hilo na kupata umuhimu wa kurudi kwenye ujenzi ili kupata mafanikio makubwa na yatakayodumu.
Hatupaswi kuruhusu teknolojia yoyote kuathiri kile kinachotutofautisha sisi binadamu na viumbe wengine. Hatupaswi kuhadaika kwamba kuna namna tunaweza kujenga mafanikio makubwa na ya kudumu bila kujenga.
1. Tumekuwa Wafanyaji Badala Ya Wajengaji.
Tangu tumeingia kwenye zama za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), mambo mengi sana yamerahisishwa. Vikwazo vilivyokuwa vinawazuia wengi kupiga hatua kwenye maisha yao vimeweza kuondolewa kabisa. Kwa mfano, huko nyuma ilimhitaji mtu kuwa na mtaji mkubwa na eneo ndiyo aweze kuanzisha biashara. Lakini kwa zama hizi, mtu anaweza kuanza biashara kwa simu yake tu, bila kuwa na mtaji wala eneo.
Maendeleo haya ya teknolojia ambayo yameleta urahisi wa kufanya mambo, yamewafanya watu kubweteka na kubaki kwenye kufanya badala ya kujenga. Kwa sababu teknolojia hizi mpya zimerahisisha kufanya, sasa kila mtu amekuwa mfanyaji. Na ufanyaji unawapa watu matokeo, lakini hawapigi hatua, kwa sababu wanabaki kwenye kufanya na hawaendi kwenye kujenga.
Kufanya kunaweza kuleta matokeo, lakini mafanikio makubwa na yanayodumu hayawezi kuletwa na kufanya. Hayo yanatokana na kujenga kitu kwa muda mrefu, ujenzi ambao unaendelea kukua kwa mkusanyiko kadiri muda unavyokwenda.
Kwa sababu watu wanapofanya wanapata haraka matokeo wanayoyataka, wanabweteka na kubaki kwenye kufanya. Ujenzi unahitaji gharama zaidi, kwa muda, nguvu na fedha, huku matokeo yake yakihitaji muda mrefu ndiyo yatokee. Kwa kutaka uharaka wa matokeo, wengi wamebaki kwenye kufanya na kuachana na kujenga.
Matokeo ndiyo tunayoyaona sasa, watu wanafanya sana, wametingwa sana, wanachoka mno, lakini wanajikuta wakisukuma tu maisha na siku ziende. Wanapofika mwisho wa maisha yao, wanakuwa hawajaacha alama yoyote hapa duniani, kwa sababu hakuna cha kudumu walichokuwa wamejenga.
Huwa kuna hali ya kuchekana baina ya waajiriwa na wafanyabiashara, wafanyabiashara wakiwaambia waajiriwa kwamba hawawezi kuwarithisha watoto wao ajira walizonazo. Lakini hata wengi wanaofanya biashara, hawawezi kuwarithisha watoto wao biashara hizo na zikadumu. Kwa sababu wanafanya kosa ambalo ndiyo waajiriwa wanalifanya, hawajengi biashara, wanafanya biashara.
Kuna tofauti kubwa ya kufanya biashara na kujenga biashara. Kufanya kunakutegemea uwepo wako, kwa sababu ni kufanya. Chochote ambacho lazima uwepo ndiyo kiweze kwenda, siyo biashara, bali ni aina ya tofauti ya ajira. Kujenga kunahitaji kuweka misingi imara, kisha biashara inaweza kwenda hata kama wewe haupo. Hapo ndiyo unakuwa mmiliki na kuwa huru, huku ukiweza kurithisha biashara hiyo kwa wengine.
Kuelewa vizuri hili, tuangalie upande wa makazi. Lazima uishi kwenye nyumba, na kuna njia mbili za kupata nyumba ya kuishi, kupanga na kujenga. Kupanga kunakupa matokeo ya haraka, kwa gharama kidogo, lakini hakukupi umiliki, unaoweza kurithisha wengine. Kujenga kunahitaji gharama kubwa, ya fedha, muda na nguvu na inachukua muda mrefu kukamilisha, lakini inakupa umiliki na kuweza kurithisha.
Kadiri teknolojia mpya zinavyokuja, ndivyo zinaondoa kabisa hitaji la kujenga na kutuweka kwenye kupanga na kufanya. Chukua mfano wa teknolojia ya taksi mtandao (Uber, Bolt) na makazi mtandao (air bnb), siyo tu huhitaji kujenga, bali pia inakuwa rahisi kupata kwa simu na mtandao.
Wakati huko nyuma ilikutana umjue dereva unayekodi gari lake, sasa unaweza kuita gari kwa mtandao, humjui kabisa dereva na ukakamilisha safari. Wakati zamani ilitaka uwe na vitu vya ndani hata kama unapanga nyumba, sasa unapanga nyumba ina kila kitu cha ndani. Wewe unaingia tu na mavazi yako kama unaenda hotelini.
Ni maendeleo makubwa ya teknolojia, lakini yanakuja na hatari kubwa sana. Maendeleo haya yanatufanya wote kuwa wafanyaji, kuwa wapangaji na kuwa wasanii. Yanatuondoa kwenye kile chenye tija zaidi, ambacho ni kujenga.
Ujio wa akili mnemba (AI) ndiyo umefanya hali ya ujengaji kuwa mbaya zaidi. AI imemwezesha kila mtu kufanya, sasa hata wale wachache waliokuwa wanajenga, wamerudi kwenye kufanya. Unakuta kwenye biashara mtu alikuwa anajenga biashara kwa kuwa na timu inayofanya vitu ambavyo hawezi, mfano kutengeneza tovuti, picha za matangazo n.k.
Lakini sasa AI inamwezesha kufanya hayo bila kutegemea wengine, na kujikuta anatumia muda mwingi kufanya vitu hivyo. Mtu anakuwa amerudi nyuma, kutoka kujenga biashara ambayo majukumu yanatekelezwa na timu na kurudi kuwa mtekelezaji wa majukumu, kwa sababu tu AI inamwezesha kufanya hivyo.
Kama hatutashtuka haraka na kurudi kwenye ujenzi, wote tutaishia kuwa wafanyaji na tutakwama kujenga mafanikio makubwa na yanayodumu.
Kuna namna watu wachache wanatengeneza hii hali ya watu kufanya badala ya kujenga, ili wanufaike zaidi wao. Ukiangalia, kampuni kubwa ya usafirishaji duniani, haimiliki hata gari moja. Mitandao mikubwa ya kijamii, haina kabisa maudhui yake yenyewe. Ni kama watu wote tumegeuzwa kuwa wapangaji hapa duniani, bila hata ya kujua.
Wajibu wetu mkubwa kwenye maisha ni kujenga vitu tunavyomiliki, ambavyo vinaweza kutupa matokeo bila ya sisi kufanya moja kwa moja. Na hilo ndiyo tunalofanya kwenye programu yetu kuu ya JUMUIA YA WASHIRIKA WA MAFANIKIO. Kwenye ushirika huu kila mmoja anajenga Mafanikio, Fedha na Biashara. Tunaenda kuangalia ujenzi wa maeneo hayo matatu kwenye vipengele vinavyofuata hapo chini.
Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza mambo manne ya ziada kwenye eneo la kujenga ambayo unapaswa kuyajua na kuyafanyia kazi ili uache kuwa mfanyaji na kuwa mjengaji. Kwa kuyajua mambo hayo, utabadili kabisa namna unavyoyaendea maisha yako na kubadili matokeo unayopata.
Karibu usome barua hiyo hapa; #BZK052; Turudi Kwenye Ujenzi Ili Tujenge Mafanikio Makubwa Na Ya Kudumu.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.