Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Imegundulika kwamba watu huwa wanaweka malengo yake yale, kila mwaka kwa mpaka miaka 10 bila kutekeleza. Yaani imekuwa ni kama fasheni, kila mwanzo wa mwaka watu wanaweka malengo na kuamini mwaka huo wanaenda kufanya makubwa.

Lakini muda unavyokwenda, malengo mengi yanasahaulika na kutokutekelezwa. Baadaye mtu anaona muda umeenda na kusubiri mwaka mwingine mpya ili aweke upya malengo yake. Hivyo ndivyo watu wamekuwa wanayaendesha maisha yao na kushangaa kwa nini hawafanikiwi.

Hivyo ndivyo tunapata watu wanaosema kila mwaka wataanza biashara au kukuza na hawafanyi hivyo. Kila mwaka wanasema wataanza kuweka akiba na kuwekeza kwa msimamo bila kuacha, lakini hawafanyi.

Najua wewe ni mmoja wa watu ambao hurudhiki na namna unavyoenda na malengo unayojiwekea. Najua umeshakazana sana kuweka malengo, lakini mengi umekuwa huyatimizi kama ambavyo umekuwa unayaweka.

Hilo siyo tatizo lako tu, ni tatizo la kila mmoja wetu. Na tatizo hilo linachangiwa na namna tunavyoyachukulia malengo. Kwenye barua hii tunaenda kuangalia tatizo la malengo na mbadala wake ili tuweze kupata mafanikio makubwa tunayoyataka.

1. Tatizo La Malengo

Kama tunaweka malengo tukiwa na nia njema kabisa ya kuyafikia na kama malengo tunayokuwa tumeweka ndiyo yaliyo muhimu kwetu kufanikiwa, inakuwaje tunashindwa kuyatimiza? Kuna matatizo tunayoweza kuwa nayo kwa upande wetu sisi wenyewe, hasa ya uvivu na uzembe, lakini bado siyo kwamba tunakuwa tumekaa tu hatufanyi chochote. Kuna vitu tunafanya, lakini siyo kutekeleza malengo tunayokuwa tumejiwekea. Na hapo ndipo tunapoona matatizo ambayo yapo kwenye malengo yenyewe, kiasi cha kutukwamisha kuyatimiza.

Tatizo la kwanza ni malengo kuonekana kitu cha baadaye, ambacho itapendeza kama tutaweza kukitimiza. Malengo tunayoweka hayawi kitu ambacho ni lazima tukitekeleze mara moja la sivyo maisha yetu yataathirika. Tunayachukulia malengo kama kitu cha ziada, ambacho tutakifanyia kazi baada ya kumalizana na mambo ya kila siku tunayoyafanya. Sasa kwa sababu mambo ya kila siku huwa hayaishi, malengo hayapati nafasi ya kufanyiwa kazi kwa uhakika.

Tatizo jingine la malengo ni wingi wake. Kama tu jina lilivyo, kila mtu anakuwa na malengo na siyo lengo. Tunapanga vitu vingi sana vya kufanya kiasi cha kushindwa kujua kipi ndiyo muhimu zaidi na kukiwekea rasilimali zetu zote. Kwa kugawa rasilimali chache tulizonazo kwenye malengo mengi, hatupigi hatua yoyote ya maana.

Unajionea wazi hapa kwa nini inakuwa rahisi kuweka malengo, lakini kuyatimiza inakuwa vigumu. Ndiyo maana nataka tubadili hilo la malengo na kuwa na kitu ambacho tutalazimika kukitimiza.

2. Unachokisubiri, Kinakusubiri Wewe.

Tumeanza na matatizo ya malengo, lakini sisi wenyewe tumekuwa na tatizo kubwa zaidi inapokuja kwenye kutekeleza malengo tunayojiwekea. Tumekuwa tunaenda kinyume na vile inavyopaswa kuwa, na ndiyo maana hata kwa kurudia malengo yale yale, tunashindwa kuyatimiza.

Unaweka malengo, lakini inapofika wakati wa kuyatekeleza unasubiri, kwa kuona bado hujawa tayari. Unasubiri mambo yakae sawa ndiyo uanze utekelezaji wa malengo yako. Usichojua ni kwamba mambo nayo hayatakaa sawa mpaka utakapotekeleza malengo uliyoweka.

Wakati wewe unasubiri mambo yakae sawa ndiyo utekeleze malengo, mambo nayo yanakusubiri wewe uanze kutekeleza malengo ndiyo yakae sawa. Haijalishi utasubiri muda mrefu kiasi gani, hakuna kitakachobadilika. Na hilo linajidhihirisha kwa muda mrefu ambao umekuwa unaweka malengo na huyafikii.

Hakuna wakati wowote utakaojiona umekamilika kwa kila kitu ndiyo uanze kutekeleza malengo uliyojiwekea. Ni kwa kuanza kutekeleza, hata kama unajiona hujawa tayari, ndiyo utakamilisha yote unayosubiria yakamilike.

Kwa sababu umeshayazoesha malengo kwenye kusubiria, inabidi uachane na malengo kwa muda na ufanye kitu ambacho kitakulazimu kuchukua hatua bila ya kusubiri chochote.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK085; Kama Huwa Unaweka Malengo Na Huyatimizi, Achana Na Malengo Na Fanya Kitu Hiki